Baada ya kuripotiwa kupatikana kwa kirusi kinachofuta data zote kwenye mifumo ya kopyuta (Wiper) katika shambulizi la hivi karibuni, serikali ya Ukraine inasema “Shambulizi hili ni la kiwango cha tofauti kabisa”. Sasa leo tuone kwa undani vita vya kimtandao kati ya Urusi na Ukraine (Cyber Warfare) kwa sababu ni jambo linaloathiri hali ya uchumi ya kila mwanadamu aishie duniani kwa sasa. Vilianza lini na vinaathiri vipi uchumi na maendeleo ya Teknolojia? Twende sambamba mpaka mwisho wa makala hii.
Jumatano ya tar 23 February, 2022 tovuti (websites) za benki kadhaa na idara za serikali nchini Ukraine hazikupatikana hewani, ambapo kampuni ya usambazaji wa huduma za internet (ISP) ya Netblocks ilidai kutokea kwa shambulizi la DDoS (Distributed Denial of Services). Agalia hii tweet yao hapa..

Lakini hii si mara ya kwanza kuripotiwa mashambukizi ya Kimtandao ambayo yanadaiwa kufanywa na Urusi.
Mashambukizi ya Kimtandao ambayo yalishawahi kufanywa hapo awali na Urusi:
Mwaka 2008 wakati Urusi inaondoa majeshi yake nchini Georgia, Rais Vladimir Putin aliongoza jitihada za kuliimarisha jeshi lake kisasa katika upande wa vita za kimtandao na mbinu zake kijasusi. Ikumbukwe Rais Putin ni ex-KGB. So ni Jasusi mbobevu kabisa kwenye uga huu.
Hivyo kwanzia hapo Urusi imekua ikitumia mashambulizi ya kimtandao kuvuruga na kubomoa taarifa na mifumo ya kimtandao ya adui. Hii imekua ni mbinu mtawalia katika medani za kivita kwanzia hapo na zimekuwa zikiratibiwa na Idara kuu ya Ujasusi jeshini iitwayo GRU.
Hii GRU kwa kifupi ni Glavnoye Razvedyvatelnoye Upravlenie (inasomwa ivyo ivyo kama inavyoandikwa). Jaribu kusoma kwa sauti tuone..
Hii ni Idara ya Ujasusi Jeshini huko Urusi. Kwa huku kwetu tungeiita Millitary Intelligence (MI). Huku ndo Ujasusi haswa unapofanyika.
Idara hii haina uhusiano wa moja kwa moja na shirika kongwe la Ujasusi la KGB kwa kuwa shirika lile lilishakufa na badala yake likazaliwa shirika la FSB ambalo kazi yake kuu kimsingi ni kukusanya taarifa za kijasusi kuhusu watu, miundombinu, usalama ndani ya nchi na mipakani n.k.
Kwa kirefu kuhusu mashirika haya ya kijasusi na namna yanavyofanya kazi tafuta kitabu cha UJASUSI WA KIDOLA NA KIUCHUMI kilichoandikwa na @YerickoNyerereT pamoja na kile cha @habibu_anga kiitwacho OPERESHENI ZA KIJASUSI. Wacha tuendelee na mada yetu tuloanza nayo.
MASHAMBULIZI KATIKA VITA VYA KIMTANDAO KATI YA URUSI NA UKRAINE (CYBER WARFARE)
- December 2015, idara ya GRU ilishambulia mitandao ya mifumo ya viwanda nchini Ukraine kwa virusi haribifu (malwares). Hii ilisababisha kukatika kwa umeme kwa zaidi ya masaa 6 katika maeneo ya Magharibi ya Ivano-Frankivsk. Hali hii iliathiri nyumba za makazi takriban 700,000.
Shambulizi hili pia lilifanywa December 2016 ambapo Urusi ilidaiwa kutengeneza kirusi kilichoitwa Crash Override ambacho kilielekezwa kwenye Gridi ya Umeme ya Ukraine. Madhara ya shambulizi hili yaliathiri takriban 1/5 (moja ya tano) ya uwezo wa jiji la Kiev kusambaza umeme.

Sababu inayodhaniwa kusababisha shambulizi hili kutekelezwa inatajwa ni majaribio ya kuharibu vinu vya Nyuklia kwa kutumia mitandao ya kompyuta. Hii ni kwasababu Vinu vya Nyuklia kwa kiasi kikubwa hutumia Nguvu za Umeme na Huduma za Mitandao ya Kompyuta katika kujiendesha kwake.
Hivyo kushambulia Gridi ya Umeme kwa mafanikio kutafanya uwezekano wa kushambulia Kinu cha Nyuklia kuwa rahisi kupitia Shambulizi la Kimtandao. Umeona watu walivyo na akili apo sasa.
2. Mwaka 2020 Marekani iliwakamata maafisa 6 wa GRU kwa tuhuma za kusambaza shambulizi lililoitwa NotPetya ransomware. Shambulizi hili liliathiri mifumo ya kompyuta dunia nzima na lilisababisha hasara ya 1 Billion dola za Kimarekani.

Shambulizi hilo linatajwa kama “SHAMBULIZI LA KIMTANDAO HARIBIFU ZAIDI KUWAHI KUTOKEA KATIKA HISTORIA” Fuatana na makala kuhusu Mashambulizi ya Kimtandao kufahamu zaidi.
3. Haijatosha hiyo, January 2021, Urusi iliandaa shambulizi lingine ambalo lililenga servers za Microsoft Exchange. Shambulizi hili liliwapa wadukuzi uwezo wa kuingia kwenye akaunti za emails za watu dunia nzima, lakini target yao ilikua ni Ukraine, Marekani na Australia.
KUMBUKA HAYA KATIKA VITA VYA KIMTANDAO KATI YA URUSI NA UKRAINE (CYBER WARFARE):
Katika uwanja wa kivita, wahusika huwa wanajulikana wazi wazi. Lakini katika Vita vya Kimtandao ni ngumu sana wahusika kujitaja hadharani. Hicho ndo kinachoendelea ambapo Urusi mara zote imekuwa ikikana kuhusika katika mashambulizi hayo. Hata China na Marekani huwa hawakubali.
Hii ni kwasababu Wadukuzi hutumia Kifaa kilichodukuliwa kama silaha kuendeleza mashambulizi. So Mdukuzi anaweza kuwa yupo Iringa akadukua compyuta iliyopo NewYork, halafu compyuta hio ikatumika kushambulia mifumo ya kimtandao iliyopo Berlin, Ujerumani. Umeona mambo hayo bwana..
Hivyo ku-trace-back mpaka kumpata mdukuzi halisi ni ngumu sana kwa kuwa mashambulizi haya hufanywa kwa kutumia mbinu za hali ya juu sana ya kijasusi na kiteknolojia. Ndio maana tunasema hapa kila siku, “Security is a myth“. Kwamba usijione upo salama sana uwapo mtandaoni.
Hata hivyo, makampuni ya kiteknolojia duniani huiba na kutumia taarifa za watu kwa sababu za kuimarisha biashara zao kwa kutumia Data Mining na Data Warehousing. Baada ya kupata taarifa hizo hutumia teknolojia mbalimbali mfano Artificial Intelligence katika kuboresha huduma zao.
Ufanyeje sasa ili uwe salama Mtandaoni?
Dunia ya leo inahitaji umakini sana ili kujiepusha na mazingira ambayo yanaweza kukupelekea kudukuliwa. Mazingira hayo ni pamoja na KUACHA tabia ya kuclick links au kufungua picha na video unazotumiwa na watu usiowafahamu, kuwa makini na tovuti unazotembelea pamoja na kuimarisha passwords zako.
Zaidi kuhusu namna bora ya kujilinda uwapo mtandaoni tayari tumeshakuwekea mbinu mbalimbali kupitia makala yatu hii hapa USALAMA WA VIFAA VYA KIELEKTRONIKI MTANDAONI.“
Tumeona Marekani na washirika wake wakiiwekea Russia vikwazo vya kiuchumi na kuwabana matajiri wa Kirusi. Je hatua hii itarudisha nyuma juhudi za Urusi katika kuimarisha ushawishi wake katika eneo la Ulaya Mashariki? vita vya kimtandao kati ya Urusi na Ukraine (Cyber warfare) itakuwa na mchango gani katika mgogoro huu?
Tusubiri tuone itakavyokuwa. Tutaendelea kukupa updates za kinachoendelea kwenye mgogoro huu wa Ukraine na Urusi hasa katika eneo letu mtambuka la Kiteknolojia, Biashara na Uchumi.
Rejea zimetoka https://bbc.com, https://www.theguardian.com/international, https://theconversation.com/global
Je umependezwa na makala zetu zilizomo katika website yetu hapa?
Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?
Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) na QR CODE ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.
Tumia LIPA NAMBA kwenye picha hapa muda wote 24/7.
