USAFIRISHAJI NA MIUNDOMBINU KATIKA USTAWI WA BIASHARA AFRIKA

Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.

Mtandao wa usafiri kwa njia ya nchi kavu barani Africa unajumuisha barabara na reli ambapo kwa wastani umechukua kilomita 6.2 kwa kila eneo la kilomita za mraba 100. Zaidi ya 60% ya mtandao mzima wa barabara haijatengenezwa kwa kiwango cha lami. Zaidi, pungufu ya 40% ya barabara za lami ndizo zilizo kwenye hali nzuri ya kupitika muda wowote. Sasa sekta hii ya usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika inatoa matumaini gani?

Mtandao wa njia za reli umeundwa kwa njia moja (single-track lines) ambazo huanzia maeneo bandarini kuelekea maeneo mbali mbali ya nchi/bara zikijumuisha viungio vichache tu njiani kuunga njia moja ya reli na nyingine (inter-linkages). Muundo huu wa reli zilizopo barani Afrika uliundwa nyakati za ukoloni na tangu wakati huo, ni marekebisho machache tu yameweza kufanyika ili kuwezesha treni ndefu zaidi zinazotumia dizeli kupita ambapo treni nyingi kati ya hizo hazitumiki tena kwa sasa.

Tukiangazia eneo la bandari, chini ya 50% tu ya matumizi ya bandari hutumika ikiwa ni pungufu ya mahitaji sahihi ya bandari hizo, jambo ambalo huchochewa na ucheleweshwaji wa mizigo na taratibu za forodha. Hali kadhalika, Afrika ndio inaongoza duniani katika ukuaji wa sekta ya viwanja vya ndege haswa kufuatia kuazishwa kwa soko huru lililoanzishwa baada ya makubaliano ya YD (Yamoussoukro Decision) yaliyofanyika mwezi November, 1999. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Afrika AU iliyotolewa mwaka 2014.

USAFIRISHAJI BARANI aFRIKA.
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.

Sasa changamoto; Je, sekta hii ya Usafirishaji na Miundombinu inaathiri vipi ukuaji wa biashara barani Africa? Na je, matumizi ya Teknolojia yana mchango gani katika kuboresha sekta hii ili kuinua biashara?

Kutokana na hali duni ya miundombinu na huduma za usafirishaji, gharama za kusafiri barani Afrika ni kati ya gharama ghali zaidi duniani, jambo ambalo linadhoofisha ushindani wa kibiashara katika masoko yote, ya ndani ya nchi na yale ya kimataifa.

Ripoti ya Tume inayoshughulikia Uchumi barani Afrika (ECA) imetaja kwamba nchi zisizo na bandari (landlocked countries) gharama za usafiri zinaweza kufikia robo tatu ya thamani ya bidhaa inayosafirishwa. Kwa mfano kusafirisha gari kutoka Japan mpaka Abijdan nchini Ivory Coast hugharimu US $1,500. Lakini kusafirisha gari hilo hilo kutoka kutoka jijini Abidjan hadi Addis Ababa hugharimu US $5,000. Kufahamu zaidi kuhusu mchango wa Teknolojia katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi kupitia link hii hapa yenye kichwa MAPINDUZI YA KITEKNOLOJIA KATIKA SEKTA YA USAFIRISHAJI NA UCHUKUZI. Ukimaliza hapo tuendelee na mada yetu ya leo.

Changamoto za Usafirishaji barani Africa.
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.

Gharama za usafirishaji zimetajwa kusababishwa na viwango vikubwa vya forodha, tozo za ucheleweshwaji, hasara zitokanazo na ajali pamoja na ukosekanaji wa fursa. Changamoto hizi huchagizwa zaidi na uduni wa miundombinu ya kiuchukuzi pamoja na huduma zinazotokana na nyanja hiyo.

Nayo programu ya maendeleo ya miundombinu barani Afrika (PIDA) katika ripoti yake imeainisha kwamba gharama za kiuchumi zinazosababishwa na changamoto za usafirishaji katika Mtandao wa Miundombinu ya Usafirishaji barani Afrika (ARTIN) zinazidi US $170 bilioni kwa mwaka kufikia mwaka 2014.

Changamoto hizo zimetajwa kusababishwa na;

•Kutokuwa na utendaji wa taratibu za kuwezesha biashara katika majukwaa ya ARTIN (kujumuisha bandari na vituo vya mipakani).

•Sera za nyanja ya usafirishaji ambazo zinapelekea kudhoofika na kuongezeka kwa gharama za usafirshaji kwa njia ya barabara pamoja na viwango duni vya barabara katika nchi nyingi barani Afrika.

• Sera za kiuchumi zinazozuia utendaji mzuri pamoja na utanuzi wa mifumo ya reli.

• Nyanja ya usafiri wa anga na Sera za kiuchumi zinazozuia uanzishwaji wa vituo vya anga vya kikanda, jambo linalotajwa kusababisha kuongezeka kwa gharama za usafiri huo.

Kufuatia changamoto hizo, Je, teknolojia ina mchango gani katika kuimarisha biashara na kupunguza gharama za uendeshaji?

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuelekea mapinduzi ya nyanja zote za kiuchumi. (Yaani tutaendelea kuwa juu kileleni😁). Mapinduzi katika matumizi ya simu kutoka simu za mezani mpaka simu za rununu (smartphones), huduma za kifedha kielektroniki (fintech), biashara za kielectroniki (ecommerce) na kadhalika vimekuwa sehemu muhimu sana katika kurahisisha utendaji wa kibiashara katika sekta ya miundombinu na usafirishaji.

Benki ya Dunia (WorldBank) inaripoti kwamba ubunifu wa kiteknolojia umewezesha sana muingiliano wa kibiashara kwa kuzingatia ongezeko la watumiaji wa Intaneti huduma za simu. Kipimo cha wiani (density) katika matumizi ya huduma za intaneti kwa kila watu 100 waliopo eneo la Kusini mwa jangwa la Sahara, ni watu 17 tu ndio wameonekana kuwa watumiaji wa intaneti katika mwaka 2015.

website inasaidia vipi kuimarisha biashara yako?
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika

Utafiti huo unakolezwa wino na shirika la kimataifa linalodhibiti mawasiliano ya simu GSMA ambapo kwenye ripoti yake ya mwaka 2018 limeangazia kwamba, eneo la kusini mwa jangwa la Sahara lilikua na kasi ya kupenya kwa matumizi ya simu ya 44% kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 kukiwa na watumiaji takriban 444 milioni sawa na 9% ya watumiaji wote wa simu duniani. Vile vile katika kipindi cha mwaka 2017-2022 watumiaji wa simu katika eneo hilo wataongezeka katika kiwango cha CAGR cha 4.8% ambayo ni zaidi ya mara mbili ya kiwango cha ongezeko kwa dunia nzima katika kipindi hicho hicho. Pia kasi ya kupenya kwa matumizi ya simu inatajwa kufikia 50% kufikia mwishoni mwa 2023 na 52% mpaka mwaka 2025.

Kufuatia uchunguzi huo, sekta ya usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara barani Afrika inatajwa kuongezewa nguvu na maboresho zaidi ili kuendana na kasi hio ya ukuaji katika ICT. Matumizi ya GPS katika usafiri wa taxi yamerahisisha zaidi gharama na muda wa kutoka sehemu moja na nyingine, huku maboresho ya miundombinu kama barabara na viwanja vya ndege yakichagiza kasi ya sekta hio.

Zaidi, mtandao wa huduma za Posta na EMS unajumuisha takriban ofisi 30,000 barani ambazo ni muhimu katika kuwezesha e-commerce trade. Kwa kuliona hilo kampuni kama DHL zimejitosa kuhakikisha teknolojia inabadili huduma za posta kuwa rahisi zaidi.

Mfanyabiashara, umejiandaa vipi na jambo hili?

Je umependezwa na makala yetu hii ya leo kuhusu usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika?

Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?

Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.

Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.

USAFIRISHAJI NA MIUNDOMBINU KATIKA USTAWI WA BIASHARA AFRIKA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *