UONGOZI vs UTAWALA KATIKA MIRADI/BIASHARA, KIPI KINAFAA ZAIDI?

Jan 15, 2021 Business Updates
Uongozi vs Utawala katika miradi/biashara, kipi kinafaa zaidi?

“Nafikiri Kiongozi mzuri ni yule anayewafanya watu wanaomzunguka kuwa bora zaidi.” Alinukuliwa Dana Brownlee (CEO Professionalism Matters). Vipi kuhusu hali ya kuwa Mtawala, inaathiri vipi biashara? Unadhani kati ya Uongozi vs Utawala katika miradi/biashara, kipi kinafaa zaidi? Fuatilia makala hii mpaka mwisho kufahamu zaidi.

Tunafahamu ilivyo, ukiwa mjasiriamali/mfanyabiashara huna budi kuvaa kofia nyingi, majukumu kila kona. Ukiwa mfanyabiashara jua unawajibika kujenga na kuimarisha masoko yako, kubuni/kusimamia miradi, kutunza hesabu nakadhalika.

Hata hivyo biashara inavyozidi kukua, vitu vya kusimamia pia vinaongezeka, hivyo mfanyabiashara/mjasiriamali makini lazima aanze kufikiria namna ya kuendesha biashara yake kwa urahisi bila kuathiri shughuli za kila siku. Unahitaji msaada kutoka kwa watu wengine. Wakati huu sasa ndipo anahitajika Kiongozi zaidi kuliko Mtawala, hasa katika biashara.

KIONGOZI ANA SIFA ZIPI?

i. ANAFANYA KAZI NA TIMU YAKE: Ukiwa Kiongozi hili ni jukumu muhimu sana. Usiishie tu kutoa amri na maagizo, hapo utakuwa Mtawala, tena asiyefaa. Kiongozi anafanya kazi bega kwa bega na timu yake, kila anapohitajika kuweka mchango wake anafanya hivyo. Katika biashara za kisasa hii ina maana Kusaidia hatua za uzalishaji zizidi kuwa bora, kuboresha maudhui ya mtandaoni ya kampuni, kuhamasisha viwango katika kazi, kuongea na wateja ili kuboresha huduma. Kiongozi anaelewa vyema watu wote anaofanya nao kazi na wateja anaowahudumia, muda wote yupo updated. Njia bora zaidi ya kuwasiliana na kujua tabia na mwenendo wa watendaji katika timu pamoja na mwenendo wa wateja ni kupitia mitandao ya kijamii. Sasa mitandao ina mchango gani, tafadhali pitia makala yako hii IJUE NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO.

ii. KIONGOZI BORA NI MNYENYEKEVU: Hakuna mtu anapenda kufanya kazi na mtu mwenye kiburi, majivuno au mjuaji sana. Hata hivyo inafaa sana kwa Kiongozi kutambua pale anapokosea na kujisahihisha mara moja, vile vile Kiongozi huruhusu timu yake kutambua makosa yao na kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali kwa kadiri zinavyotokea. Unyenyekevu (Being Humble) husaidia kuimarisha morali ya ufanyaji kazi katika miradi/biashara kuliko kiburi na majivuno.

 Uongozi vs Utawala katika miradi/biashara, kipi kinafaa zaidi?

iii. MAWASILIANO WAZI: Katika vitu muhimu vya kufanya katika kufanya biashara/mradi kwa mafanikio ni namna timu inawasiliana kwa uwazi. Kila mtu anayefanya kazi katika timu hujihisi ana umuhimu pale anapokuwa na taarifa kamili kuhusu mambo yote yanayoendelea ndani ya timu yake na pale anapoweza kuwasiliana na yeyote ndani ya timu na kujuzwa mambo kwa uwazi. Unapokuwa na jukumu la kuhudumu ndani ya timu ni muhimu kuwa straight-forward kwa kuwa biashara/kampuni yako ni taswira yako mwenyewe kama Kiongozi. Hivyo, unapokuwa muwazi katika mawasiliano pamoja na kuzingatia maadili ya kiweledi (ethical behaviors) katika utendaji wa shughuli za kila siku, timu nzima unayoiongoza itafuata taswira hio.

iv. KUWA MSIKIVU: Kama Kiongozi ni jukumu lako kusikikiza kwa umakini mara zote mwingine anapozungumza iwe katika timu ama mteja. Usikivu humpa mzungumzaji nafasi ya kusema kile anadhani kinafaa katika kuboresha shughuli za kibiashara/kimradi ambazo ni muhimu sana katika ukuaji wa kampuni/biashara. Usikivu humfanya mzungumzaji kuungana moja kwa moja na wewe kama kiongozi katika kuimarisha mradi/biashara.

Uongozi vs Utawala katika miradi/biashara, kipi kinafaa zaidi?

Usikivu pia huimarisha Mvuto (impression) wako katika macho na akili za watu ulionao katika mazungumzo. Tafiti zinaonyesha mzungumzaji husema kile kilichopo moyoni mwake kuhusu vile anataka kuhudumiwa au kutoa wazo la kuimarisha biashara pale anaposikilizwa kwa umakini.

v. KUWA NA MTAZAMO CHANYA: Katika kufanya shughuli za kila siku za mradi/biashara, changamoto hazikosekani. Iwe ni changamoto ndogo au kubwa, kama Kiongozi jinsi unavyoshughulika na mazingira hasi katika mradi/biashara yako hutafsiri mengi kuhusu maarifa ya kiuongozi uliyonayo. Robert Mann (mwandishi ya kitabu The Measure of a Leader) ananukuliwa “Look at three positive things about a problem before you identify what makes it dissatisfying. The more you look at the positives in a problem, the more positive people react with one another.”

Katika utafiti wake bwana Mann aligundua kuwa baada ya watu kuona mambo mazuri katika mazingira yenye changamoto, hufikiria namna ya kukabiliana na changamoto hio ili kufikia lile jambo lenye faida. Sawa sawa na vile jinsi Kiongozi anavyotaka kuimarisha mbinu za kiutendaji.

vi. FAHAMU BIASHARA/MRADI WAKO: Njia bora ya kufahamu kitu unachokifanya ni kwa kutumia uchambuzi wa SWOT ambao unakusaidia kufahamu Strength (nguvu/faida ya biashara), Weaknesses(Udhaifu wa mradi/biashara), Opportunities (fursa zinazokuja na biashara hio) pamoja na Threats(matishio yanayoikabili biashara). Kwenye kufanya uchambuzi huu zingatia haya;

STRENGTH (Nguvu/Faida ya biashara/mradi wako): Unaweza kuboresha jambo gani zaidi ya washindani wako? Uongeze malighafi/huduma gani ambazo washindani wako bado hawana? Mteja wako anafuraha?

•WEAKNESSES(Madhaifu ya mradi/biashara): Ni malighafi/huduma gani ambazo washindani wako wanazo ila wewe bado huna? Ni kipi unahitaji kuimarisha katika mradi/biashara yako? Una uzoefu wa kutosha kushindana na wafanyabiashara wengine? Unafanyaje baada ya hapo?

OPPORTUNITIES (Fursa): Unaona fursa gani katika mradi/biashara yako? Sheria za nchi, unaweza vipi kuzitumia vizuri katika kuimarisha mradi/biashara yako? Nje ya biashara/mradi wako kuna jambo/trend gani maarufu linaendelea? Unaweza vipi kulitumia jambo hilo kwa faida yako?

Je, kuna matamasha, matukio ya kijamii katika kalenda yako hivi karibuni? Unaweza vipi kuyatumia matukio hayo kwa faida ya biashara/mradi wako?

•THREATS (Matishio yanayoweza kuikumba biashara/mradi wako): Una changamoto za kifedha? Biashara/mradi wako utajiendesha vipi? Je vyanzo vyako vya kifedha ni vya kuaminika na kutegemeka (reliability)? Biashara/mradi wako unaweza kuhimili maendeleo ya kiteknolojia yanayozidi kushika kasi duniani? Kuna mambo gani binafsi yanayoweza kuathiri biashara/mradi wako? Katika timu yako, kuna mtu anapitia wakati mgumu katika kukabiliana na mambo binafsi kama msiba, ugonjwa au harusi?

Hayo ni baadhi ya maswali ambayo unaweza kujiuliza wewe kama kiongozi pamoja na timu yako ili uweze kuifahamu biashara yako na mazingira inayopitia ili kutengeneza njia nzuri zaidi ya kufanikiwa.

MTAWALA ANAATHIRI VIPI BIASHARA/MRADI?

Mazingira ya biashara/mradi ni sehemu inayohitaji mahusiano mazuri zaidi ili kuhakikisha biashara inakuwa na kudumu kwa miaka mingi zaidi. Lakini unapoingiza Utawala unaingiza ile hali ya kuhitaji zaidi na kuweka mbele matakwa binafsi.

•Mtawala anatoa amri na maagizo pasi na kuangalia hali ya utendaji ya timu yake.

•Si mara zote mtawala anakuwa muwazi kwa timu yake. Jambo linalohatarisha utendaji bora wa timu.

•Kiburi na majivuno humfanya kiongozi bora kuwa mtawala dhalimu ambaye hahitajiki katika biashara.

Hizo ni baadhi ya athari za Uongozi na Utawala katika maendeleo ya Biashara/Miradi. Je unadhani kati ya Uongozi vs Utawala katika miradi/biashara, kipi kinafaa zaidi? Makala zifuatazo katika link ni muendelezo mzuri wa somo ulilolipata katika makala hii ya leo. TUJADILI..

  1. FANYA MAAMUZI SAHIHI KATIKA MUDA SAHIHI
  2. UKWELI KUHUSU PROPAGANDA
  3. KWANINI UITANGAZE BIASHARA YAKO?
3 thoughts on “UONGOZI vs UTAWALA KATIKA MIRADI/BIASHARA, KIPI KINAFAA ZAIDI?”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *