Japokuwa imechelewa, lakini kwa sasa Africa ndio inaongoza mbio katika kufanya mapinduzi ya kidijitali kuliko sehemu yoyote duniani. Namna ya kufanya biashara inazidi kubadilika ikionyesha nia ya dhati kufanya maendeleo ya kiuchumi, miundombinu na maswala ya kijamii. Mwaka 2018 nchi wanachama wa Umoja wa Africa walipiga hatua kubwa katika mfumo wa kufanya biashara na muingiliano wa kiuchumi baada ya kuanzisha Eneo Huru la Kufanyia Biashara barani (Continental Free Trade Area AfCFTA). Eneo hili lililoanzishwa linashirikisha nchi 22 zilizoweka sahihi tayari na utekelezwaji wake ulipangwa kuanza mwaka 2019 (tayari umeshaanza).
Hata hivyo mazungumzo bado yanaendelea kuweza kuzishirikisha nchi ambazo bado si wanachama wa eneo hili jipya, inatarajiwa eneo hili kufikia soko la watu takribani bilioni 1.2 barani wakiwa na jumla ya pato la ndani la taifa (GDP) la dola za kimarekani trilioni 2.5 kwa pamoja, kwa mwaka. Hii inatarajiwa kuwa ni mapinduzi makubwa zaidi kuwahi kutokea kwenye nyanja ya uchumi wa Afrika.
Sasa, swali linakuja; Afrika(wafanyabiashara, makampuni/mashirika na Serikali) imejiandaa vipi na mapinduzi haya ya uchumi wa kidijitali? Na zaidi, watunga sera/sheria wataangalia vipi biashara za kielektroniki (e-commerce) kama mada muhimu katika eneo hilo jipya la kufanya biashara huru barani?
Tume ya kudhibiti uchumi wa Africa ya Umoja wa Mataifa (ECA) ikishirikiana na Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) pamoja na Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo ya kibiashara (UNCTAD) mwaka huu 2019 imechapisha ripoti yake ikiangazia maendeleo ya Afrika kiujumla katika nyanja za kiuchumi, siasa na kijamii.
URAHISI: Imeonekana kwamba e-commerce inaweza kufanya biashara ya bidhaa na huduma kwa urahisi zaidi ambapo itarahisisha mwenendo mzuri wa biashara kati ya wazalishaji, wafanyabiashra na walaji pamoja na kumbukumbu zao na miamala ya kifedha.
MITANDAO YA KIJAMII: Pia imeonekana kwamba e-commerce inapatikana na kufanyika kirahisi katika mitandao ya kijamii kama facebook na Instagram ambapo ndipo mahali kuna watumiaji wengi zaidi wa Intaneti duniani (zaidi ya watu bilioni 2 kati ya watumiaji bilioni 4 wa intaneti).
KUTOKUWA NA MIPAKA: Mfumo wa uchumi wa Kidijitali kiasili umetengenezwa kuepuka mipaka ya kijiografia katika kufanya biashara na kubadilishana fedha ambapo mabadiliko haya ya kiteknolojia yataongeza umakini zaidi katika mwenendo wa masoko na gharama. Lakini bado wimbi kubwa la watu watakaoshiriki kwenye soko barani wanaonekana wataachwa nyuma kutokana na kutokuingiliana kwa lugha na vita/ghasia za mara kwa mara katika baadhi ya jamii/nchi.
BIASHARA: Kwa mujibu wa UNCTAD mwaka 2016 kwa dunia nzima e-commerce iliweza kupitisha mauzoya takribani dola trilioni 26 ambapo 90% ilikuwa ni Biashara kwa Biashara (B2B e-commerce) na 10% ilikuwa ni Biashara kwa Mlaji (B2C e-commerce). Hata hivyo kupima mwenendo wa e-commerce katika baadhi ya nchi zinazoendelea imekuwa ni changamoto kupata data na takwimu, haswa katika nchi za Afrika.
IMPORTATION: Takwimu za Shirika la Fedha Duniani (IMF) zinaonyesha kwamba Biashara kati ya nchi na nchi imekua kwa kiasi kikubwa Afrika ambapo zimechagizwa na vituo vichache vya kiteknolojia (Hubs) ambavyo vimerahisisha mno mwenendo wa biashara. Biashara kati y nchi na nchi (Intraregional import) imekuwa zaidi ya mara 3 katika miongo miwili iliyopita kufikia 12%- 14% sawa na dola bilioni 100 ikichagizwa na uwepo wa jumuiya za kiuchumi barani (Subregional Economic Communities REC‘s).
UZOEFU: Hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na umri wa Jumuiya hizi za Kimaendeleo barani Afrika ambapo uzoefu huo hutumika kuongeza jitihada katika kuboresha namna ya ufanyaji biashara kuelekea uchumi wa kidijitali kiteknolojia. Uzoefu huo pia hutumika kuunganisha jumuiya moja na nyingine (mf, SADC na COMESAna EAC) ambapo zitazalishwa nafasi nyingi zaidi za kufanya biashara kati ya nchi wanachama na ripoti zinaonyesha 75% ya biashara hizi ndani ya jumuiya barani Afrika zimefanyika mwaka 2017 peke yake na nusu ya biashara hizo zilifanyika katika jumuiya ya SADC.
Chini ya mwavuli wa AfCFTA nchi wanachama zinatarajia kufuta tozo/ushuru kwa 90% ya bidhaa zote zitakazopitishwa na kufanyiwa biashara katika eneo hilo. Hii itaruhusu uwezekano wa kupunguza mlolongo wa kodi au kuongeza idadi na thamani ya bidhaa na huduma zitakazohusishwa. Matokeo yoyote katika punguzo hilo linalotarajiwa katika muktadha wa biashara kidijitali yataleta picha tofauti. Kupunguza mlolongo wa tozo za mipakani baina ya nchi na nchi kutapungua kwa 15% pekee ikitegemea thamani ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi husika. Hii ni kwa mujibu wa Tume inayoshughulikia Uchumi wa Afrika kutoka Umoja wa Mataifa (UNECA) mwaka 2018.
Sasa mwaka 2018 Jumuiya ya COMESA ilibuni mfumo wa kudhibiti eneo huru la kibiashara kidijitali (Digital Free Trade Area DFTA). Mfumo huu umeundwa na mambo yafuatayo;
•E-trade: Hili ni jukwaa mahsusi kwa ajili ya kufanya biashara za kimtandao na kuwezesha malipo ya kielektroniki, mobile apps kwa ajili ya wafanyabiashara walioko katika Jumuiya hio.
•E-logistics: hili ni jukwaa maalum kwa ajili ya kuwezesha biashara ya usafirishaji wa mizigo baina ya nchi wanachama wa jumuiya.
•E-legislation: huu ni mfumo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara rasmi ambao unawawezesha kufanya miamala na malipo kielektoniki.
Mfumo huu uliobuniwa na Jumuiya ya COMESA umelenga kutangaza biashara za wanajumuiya katika nchi wanachama ikijumuisha kupitia majukwaa ya e-commerce. Mfumo huu ulikuwa ni mfanano wa mfumo uliotengenezwa na kuzinduliw na nchi ya Malaysia mwaka 2017 katika muktadha wa kufanya biashara huru ndani ya eneo maalum.
Makala haya ya leo yamelenga wafanyabiasha kujidhatiti kidijitali kwa kutumia teknolojia za kisasa katika biashara zao za kila siku ili kuweza kunufaika vyema na masoko pamoja na fursa kede ndani na nje ya nchi.
Makala hizi hapa zinarandana na somo ulilolipata leo. Zitakusaidia sana, shuka nazo:
- https://rednet.co.tz/fahamu-kuhusu-biashara-ya-fedha-za-kidijitali-cryptocurrency-business/ yenye kichwa “FAHAMU KUHUSU BIASHARA YA FEDHA ZA KIDIJITALI (CRYPTOCURRENCY BUSINESS)”
- https://rednet.co.tz/teknolojia-ya-huduma-za-fedha-kwa-njia-ya-kielektroniki-fintech/ yenye kichwa “TEKNOLOJIA YA HUDUMA ZA FEDHA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI (FINTECH)”
- https://rednet.co.tz/fahamu-siri-ya-kufanikiwa-katika-kuwekeza/ yenye kichwa “FAHAMU SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA”
Ukiwa na lolole, tafadhali unaweza kuwasiliana nasi kupitia;
e-mail: info@rednet.co.tz
tovuti: https://rednet.co.tz
Simu:+255765834754