UFAHAMU MFUMO WA KODI NA MAPATO YA SERIKALI ZA MITAA

Aug 30, 2020 Economic Updates

Serikali za mitaa zikiwa ndani ya Halmashauri za miji/Majiji na Wilaya zina mamlaka ya kukusanya mapato na ushuru kutoka vyanzo mbalimbali vya kodi. Pia zina mamlaka ya kutumia mapato hayo kwa mujibu wa sheria.

Kulingana na mipaka ya kisheria inayowekwa na Serikali Kuu, hizi Serikali za mitaa zina uwezo wa kutengeneza sera zake za mapato ili kuleta maendeleo katika shughuli zinazogusa kwa ukaribu maendeleo jamii nzima kama mashule, hospitali, mazingira ya mitaa na ulinzi shirikishi.

Mapato haya yanayokusanywa yanapata Mamlaka kutoka katika Sheria ya Mapato ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1983 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Sasa leo ukimaliza kusoma makala haya, utakuwa umezijua kodi/tozo zote zinazokusanywa pamoja na matumizi yake kwa ujumla.

Idadi ya kodi na ushuru unaokusanywa chini ya Mamlaka ya serikali za mitaa hutofautiana kutoka Halmashauri moja na Halmashauri nyingine. Mambo yanayoleta utofauti huu ni maendeleo katika sekta za Biashara, makazi, Uwepo wa maliasili na shughuli za kiuchumi.

Kuna baadhi ya tozo hukusanywa kwa siku, zingine mlipakodi hutozwa kwa mwaka, na zingine humpa nafasi mlipakodi kuchagua wakati wa kulipa (kwa mwezi, wiki, miezi mitatu/sita au kwa mwaka). Mfano; ushuru wa masoko, huu kawaida hukusanywa kwa siku. Hata hivyo Halmashauri zingine hutoa nafasi kwa mlipakodi kulipia ushuru huu kwa mwezi, miezi 3/6 au kwa mwaka mzima. Mwisho wa mwaka wa fedha kila Halmashauri inatakiwa kuandaa akaunti za kifedha ikiwa na wadau wafuatao:

i. Halmashauri Nzima

ii. Muwakilishi wa wizara (TAMISEMI)

iii. Ofisi ya Waziri Mkuu

iv. Ofisi ya Mdibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG)

v. Umma

Serikali za Mitaa hupata mapato yake kutoka katika vyanzo vikuu vitatu :

1. Mapato yake yenyewe

2. Ruzuku kutoka Serikali Kuu

3. Misaada kutoka mifuko ya Maendeleo ya ndani na nje ya nchi.

MAPATO/KODI ZINAZOTOZWA NI ZIPI?

1. USHURU WA BIDHAA (PRODUCE CESS)

Ushuru huu hutozwa na halmashauri kutoka katika mauzo ya mazao kama mahindi, mchele, kahawa, chai, pamba korosho pamoja na mifugo. Ushuru huu hutozwa kutokana na uzito/ujazo wa bidhaa yenyewe. Hii hufanya thamani ya bidhaa kutokua thabiti ikitegemea uzito/ujazo wa bidhaa (the source to be inelastic unless adjustments become frequent enough to catch up with inflation), hapa watu wa uchumi mtakuwa mmenipata vizuri sana. Viwango vya ushuru huu hubadilika kutegemeana na Halmashauri kutokana na Jiografia ya eneo, misimu ya hali ya hewa pamoja na hadhi ya kiuchumi ya Halmashauri husika.

2. LESENI ZA BIASHARA

Kodi hizi hutozwa kutokana na ukubwa na aina ya biashara, yaani maduka mawili ya rejareja yatatozwa kodi ya leseni sawasawa bila kujali ukubwa wa mitaji yao au hesabu zao wanazowasilisha kwenye mamlaka za mapato (turnovers).

3. ADA YA MASOKO

Aina hii ya Ushuru kwa kawaida hutozwa kwa siku kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao katika maeneo ya sokoni. Viwango vya tozo hii hubadilika kulingana na bidhaa zainazouzwa.

4. KODI YA ARDHI/MAJENGO

Kisheria, Serikali kuu inatakiwa kukusanya kodi kutoka kwenye mali zote zinazohamishika, wakati Serkali za Mitaa zitakusanya kodi katika mali zote zisizohamishika. Hata Hivyo, kodi ya ardhi na majengo haijaweza kutumika ipasavyo katika mambo ya kisiasa na uongozi katika nchi zinazoendelea. Katika kitabu chake kuhusu kodi ya ardhi, Richard Bird (1974:223) anasema, “The administrative constraint on effective land on effective land tax administration is so severe in most developing countries today that virtually all the more refined fiscal devises beloved by theorists can and should be discarded for this reason alone. Not only will they not be well administered, they will in all likelihood be so poorly administered as to produce neither equity, efficiency, nor revenue.” Nadhani hoja yake imeeleweka.

5. USHURU WA HOTELI/NYUMBA ZA WAGENI

Kodi hii kisheria hutegemea na tathmini binafsi kuhusu hesabu za hoteli/nyumba za wageni. Viwango vikubwa vya kodi huhamasisha ukwepaji wa kodi hasa kwa kurekodi hesabu mara mbilimbili. Katika utekelezaji, hasa kwa biashara ndogo ambazo hazitoi risiti, turnover zao hukadiriwa tu na hivyo kupunguza mapato kwenye serikali za mitaa. Hata hivyo, biashara kubwa ambazo pia hazitoi risiti huwekewa utaratibu wa kufanya maridhiano kati ya wakusanya kodi na walipa kodi. Utaratibu huu unaongeza gharama za uendeshaji na kuongeza mianya ya rushwa. Hata hivyo, kutokana na makusanyo haya kuzingatia asilimia za mapato ya biashara, makusanyo yanategemewa kubadilika kadhalika.

6. KODI YA MABANGO/MATANGAZO

Hii kodi wafanyabiashara wengi huilalamikia, wengine wasijui kwanini wanatozwa wakiweka tu mabango katika biashara zao. Viwango vya kodi hii hutegemea ukubwa wa bango, kama linawaka taa usiku na muda bango hilo litakavyokuwa wazi. Mapato ya mabango yanaendelea kukua kutokana na kuongezeka kwa biashara ambazo pia zinahitaji matangazo kujiimarisha.

7. USHURU WA MCHANGA

Unashangaa? Hadi mchanga wa kujengea unalipiwa kodi ndio katika baadhi ya halmashauri. Gharama ndogo za mchanga pamoja na kuongezeka kwa kasi ya watu kujenga kumechochea mmomonyoko wa udongo kwenye machimbo jambo lilifanya serikali kupiga marufuku Uchimbaji holela wa mchanga na kuanzisha utaratibu mpya wa kuchimba mchanga katika maeneo maalum na hivyo kudhibiti mapato yatokanayo na mchanga.

8. USHURU WA MACHINJIO/MAEGESHO

Halmashauri nyingi ambazo zina machinjio ya wanyama na maengesho ya magari hutoza kodi hio vizuri. Mapato yatokanayo na kodi hii yamekuwa yakiongezeka hasa maeneo ya mijini ambapo kumekuwa na uhitaji mkubwa wa maegesho ya magari na pikipiki pamoja na kuongezeka kwa wanyama wanaonmchinjwa katika maeneo maalum. Hii ni kwa kuwa serikali imefanikiwa kudhibiti machinjio zote za mitaani na kulazimisha wanyama wote kuchinjwa maeneo maalum ya machinjio ambayo yana udhibiti wa kiserikali na kuzingatia viwango vya nyama kwa manufaa ya walaji. Wale wanaopajua vingunguti watakuwa wamenipata sawasawa hapa.

9. KODI ZINGINE

Serikali za Mitaa hukusanya kodi nyingine nyingi sana. Unaweza kuzipata kwa ufupi katika tovuti rasmi ya Wizara ya Fedha kupitia link hii https://mof.go.tz/mofdocs/revenue/revlocal.htm…

Serikali za mitaa hazitozi kodi ambazo zipo nje ya zilizopo kwenye listi iliyo kwenye link hio.

Vile vile unaweza kupata maelezo kuhusu Kodi na wajibu wake katika matumizi ya mwaka 2018/2019 kupitia link hii hapa chini

https://rednet.co.tz/download/taxes-and-duties-at-a-glance-2018-2019…

HIZO KODI ZINATUMIKA VIPI?

Kodi zinazokusanywa na Halmashauri za Wilaya/Miji/Majiji hutumi kodi hizo kuimarisha mambo yafuatayo:

i. Ulinzi shirikishi

ii. Barabara za mitaani pamoja na miundombinu yake

iii. Zimamoto na uokoaji

iv. kuimarisha shughuli za kiuchumi (masoko, biashara) nk

Mfumo wa kodi wa serikali za mitaa kwa muda mrefu umekuwa tata sana na usio na uwazi katika makusanyo ya mapato yake mpaka matumizi. Lakini tangu kuzinduliwa kwa mfumo maalum wa makusanyo ya kodi kwa njia ya kielektroniki wa Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS) mnamo mwaka 2014, mfumo huo umekuwa mkombozi katika kurekodi makusanyo sahihi na kudhibiti matumizi katika Halmashauri. Mfumo huo wa kisasa umekuwa bora zaidi katika kukusanya Mapato ambapo unatoa urahisi wa kutumia njia mbalimbali za kulipia kodi kama MPESA, TIGOPESA, AIRTEL MONEY, Njia ya Benki na kadhalika.

Kuna makala hizi hapa chini tumekuwekea kwenye links. Zitakusaidia kufahamu zaidi kuhusu mifumo ya kodi na mapato hasa nchini Tanzania. Gusa link kisha makinika:

  1. https://rednet.co.tz/ufahamu-mfumo-wa-kodi-nchini-tanzania/ yenye kichwa “UFAHAMU MFUMO WA KODI NCHINI TANZANIA”
  2. https://rednet.co.tz/lipa-kodi-kwa-faida-ya-biashara-yako/ yenye kichwa “LIPA KODI KWA FAIDA YA BIASHARA YAKO”
  3. https://rednet.co.tz/unaweza-vipi-kukabiliana-na-hasara-katika-biashara-yako-mwaka-huu-2021/ yenye kichwa “UNAWEZA VIPI KUKABILIANA NA HASARA KATIKA BIASHARA YAKO MWAKA HUU 2021”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *