Tag: viwanda

IFAHAMU TEKNOLOJIA YA QR-CODE KATIKA BIASHARA YAKO

Kwa kasi ya maendeleo ya kiteknolojia inavyozidi kuchanja mbuga, watu wanatumia sana simu janja kwa matumizi mengi zaidi ukiacha kupiga simu na kutuma ujumbe. Uwezo wa kununua bidhaa na kupata huduma haraka umewezeshwa zaidi kupitia ujio wa QR-Codes. Sasa leo ifahamu teknolojia ya QR-Code katika biashara yako. Makinika.

Hizi QR (Quick Response) codes zinaweza kusomwa na kudadavuliwa vyema kwa kutumia Simu janja na vifaa maalum vya kielektroniki (QR-scanners) na hivyo kujenga wepesi kwa watu wa masoko kuingiza maelezo kuhusu majukwaa yao kupitia hizi QR Codes. Yani maisha ya kibiashara yamekuwa mepesi kweli.

QR-codes hizi huweza kuwekwa katika mabango, magazeti, kurasa za tovuti na vyombo vingine vya kimasoko ili kurahisisha usambazaji wa bidhaa na huduma kwa haraka na wepesi zaidi. Matumizi ya QR-Codes yamekuwa yakizidi kutanuka kila uchwao ambapo katika kipindi cha mwaka 2018/19 peke yake, matumizi ya QR Codes duniani yaliongezeka kwa 28% huku ongezeko la muingiliano katika kipindi hicho likikuwa kwa 26% (chanzo: akaunti ya Blue Bite, mtandao wa medium).

QR CODES ZINA TOFAUTI GANI NA BARCODES?

Japokuwa Barcodes zilianzishwa miongo mingi kabla, QR Codes zimekuja na mapinduzi makubwa ndani ya muda mfupi.

1. Kama ulishawahi kununua bidhaa ya kiwandani hasa zile zinazouzwa katika supermarkets, utagundua bidhaa hizo zina alama fulani za vimistari pamoja na namba. Alama hizo ndio huitwa BARCODES. Sasa hizo Barcodes hutumika kuhifadhi maelezo muhimu kuhusu bidhaa husika kama jina la bidhaa, mtengenezaji, bei, kiwango cha ubora n.k. QR Codes kwa upande wake hufanya kazi sawa sawa na hizo Barcodes, isipokuwa tu katika QR Codes, zina uwezo wa kuhifadhiwa data nyingi kwa mamia zaidi katika nafasi ndogo.

2. MUONEKANO: Hii ndio tofauti kubwa katika ya hizi teknolojia mbili. Kwa kutizama tu unaweza kujua ipi ni QR Code na Ipi ni Barcode. Hebu tizama mifano hii hapa chini.

ifahamu teknolojia ya QR-Code katika biashara yako. Makinika.

3. UWEZO WA KUJISAHIHISHA: Kwa utofauti huu, QR Code inakuwa bora zaidi kuliko Barcode na kujitofautisha katika viwango vya matumizi. Muonekano wa QR Code unaifanya iweze kutoa taarifa kuhusu bidhaa/huduma vizuri hata kama ikitokea sehemu za alama hazionekani vizuri au zimechanika tofauti na Barcode ambapo ukifutika mstari mmoja tu Barcode inashindwa kutoa maelezo kamili kuhusu bidhaa/huduma.

QR CODES HUTUMIKA WAPI NA WAPI?

Kimsingi QR Codes hutumika katika kuhamasisha muingiliano katika ya mteja na huduma kupitia alama za kielektroniki kwa uharaka zaidi kwa kutumia simu janja au QR-Code scanners. Hii ni mbinu bora sana ya kimasoko katika kurahisisha utoaji huduma na uwezeshaji wa malipo/miamala ya kifedha. Sasa tuone maeneo ambayo QR Codes zinatumika:

1. KUELEKEZA WATUMIAJI KATIKA KURASA/TOVUTI:

Unaposcan QR Code, inaweza kukuelekeza katika kurasa fulani maalum au tovuti ambayo maelezo yake yamefichwa katika CODE hio. Zoezi hili unaweza kulifanya kwa wepesi kupitia QRCode iliyopo kwenye tangazo hili ambayo itakuelekeza katika fomu maalum ya kujiandikisha kuhudhuria mafunzo yanayojieleza.

2. KUPIGA SIMU NA KUPATA MAWASILIANO:

Katika mikutano ya kibiashara mara nyingi watu hukutana na kubadilishana mawasiliano kwa wingi. Lakini zoezi hilo hufanywa jepesi kwa kutumia QR Code ambapo kitendo cha kuscan tu hukuwezesha kupata mawasiliano yote muhimu kuhusu mtu fulani.

Kinachofanyika ni kujaza taarifa muhimu katika QR Code kisha CODE hio hupachikwa katika Business Card mara nyingi. Hivyo unaposcan unapata mawasiliano yote pasi na kuhangaika kuandika namba moja moja katika simu yako.

simu za michongo Faida za kutumia Google kama Jukwaa la biashara yako.

3. KUPAKUWA APPS MTANDAONI:

Unaposcan QRCode katika masijala za Aplikesheni za mitandaoni, basi unakuwa na uwezo wa kupakuwa App husika kirahisi bila ya kuhangaika kutafuta App hio mitandaoni. Unapoikuta QR Code wewe scan tu, mambo mengine yatajiendeleza yenyewe kirahisi.

4. KUJUA MAHALI BIASHARA ILIPO:

Naam, kupitia ramani za kimtandao kama Google Map, mtumiaji anaweza kuscan QR Code ya biashara na mara hio akaweza kuona mpaka mahali/location biashara hio ilipo. NOTE: Location hio lazima iingizwe kwanza katika QR Code na mfanyabiashara husika.

5. KUFANYA MANUNUZI NA MALIPO:

Pengine hii ndio njia maarufu zaidi ambayo QR Code hutumika. Makampuni ya huduma za mitandao yameingiza na kuboresha sana njia hii katika kufanya manunuzi na malipo. Mara nyingi wafanyabiashara hutumia njia hii katika kutoa punguzo la bei au kufanya matangazo (promo) kwa bidhaa/huduma fulani. Ni mwendo wa kuscan tu na malipo yako unakuwa umekamilika mara hio. Unachotakiwa kufanya kama mfanyabiashara ni kuhakikisha QR Code yako inafanya kazi ile uliyoiamuru (Call-To-Action). Mtumiaji hatakiwi ajiulize afanye nini baada ya kuscan hio code.

HIZI QR CODES ZINAFANYA KAZI VIPI?

Ili uweze kutengeneza au kutumia QR Code ukiiona mahali unatakiwa kuwa na vitu vifuatavyo:

>QR Code Generator: Kuna majukwaa mengi sana mtandaoni ambayo unaweza kuyatumia kutengenza QR Code kwa matumizi yako unavyotaka. Baadhi ya majukwaa hayo Ni pamoja na http://qrcode-monkey.com na http://the-qrcode-generator.com . Katika majukwaa haya unaweza kutengeneza QR Code yako, ukaweza na maelezo kama namba ya simu, tovuti, location nakadhalika. Lakini pia yapo majukwaa ambayo unalazimika kulipia ili uweze kutengeneza QR Code yako.

Majukwaa hayo ni pamoja na KAYWA na ni salama zaidi pale unapotaka kutengeneza QR Code ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kurahisisha malipo yoyote. Vya bure vina madhara sana hasa katika maswala ya kifedha. Kuwa makini hapo.

>QR Code Readers: Hizi ni Apps ambazo unazipata katika simu yako mahsusi kwa ajili ya kutambua QR Code na kukupeleka kule kunapotakiwa kwenda. Kwa watumiaji wa iPhone unaweza kupakuwa App inaitwa i-nigma ambayo inatajwa kama App bora zaidi duniani katika kuscan hizi QR Codes. Kwa watumiaji wa Android unaweza kupakuwa App iitwayo Barcode Scanner (watumiaji wa tekno nao wamo hapa.)

KWANINI UTUMIE QR CODE KATIKA BIASHARA YAKO LEO?

Mwaka 2019 matumizi ya QR Code katika kufanya malipo ya bidhaa na huduma yalipata umaarufu mkubwa sana duniani huku makampuni makubwa kama Mastercard na Paypal yakithibitisha matumizi katika kutambua account za wateja na kuidhinisha malipo.

Tafiti zinaonyesha kuwa wateja wanaolipia kwa kutumia QR Code hufanya manunuzi makubwa zaidi. Sasa leo hizi ndizo sababu zitakufanya ifahamu teknolojia ya QR-Code katika biashara yako. Mwaka 2013 Adobe mobile consumer uliowahusisha wstumiaji wa simu 3,075 ulionesha majibu haya;

•46% ya wateja waliscan ili kupata discount

•42% walitumia QR Code kama tiketi

•67% walishuhudia huduma za QR Code katika maduka ya mtaani.

Mpaka kufikia mwaka 2020 takwimu hizo zinatajwa kuongezeka maradufu zaidi. Lengo kuu hapa ni kuhakikisha QR Codes zinasaidia wateja kufanya shughuli zao kwa wepesi zaidi.

Makala hizi hapa chini zinarandana na somo ulilolipata leo. Zitakusaidia sana ukizipitia zote. Gusa link kisha makinika:

  1. FAHAMU KUHUSU MAPINDUZI YA 4 YA VIWANDA DUNIANI
  2. UMUHIMU WA TAKWIMU KATIKA UTOAJI WA HUDUMA BORA KWA WATEJA
  3. UGUNDUZI WA KITEKNOLOJIA KUELEKEA KATIKA MUSTAKABALI WA SEKTA YA UZALISHAJI MALI

Umejifunza nini kwenye makala ya leo katika ku ifahamu teknolojia ya QR-Code katika biashara yako. Tafadhali toa maoni yako na sambaza hii kwa jirani yako.

FAHAMU MCHANGO WA ICT KATIKA MAENDELEO YA SEKTA BINAFSI BARANI AFRICA

Kwa mara ya kwanza katika Historia ya mwanadamu, zaidi ya nusu ya watu wote duniani wanatumia huduma za internet. Na katika maeneo yote, imeonekana huduma hizo zinakua kwa kasi zaidi barani Africa. Idadi ya watu wanaotumia internet imeongezeka sana barani Afrika kutoka 2.1% mwaka 2005 mpaka 24.4% mwaka 2018. Sasa leo nataka u fahamu mchango wa ICT katika maendeleo ya sekta binafsi barani Africa. Twende sambamba.

Huduma hizi za internet zimekuja kurahisisha shughuli za kiuchumi kama kurahisisha njia za malipo (bank, MPESA, tigopesa nk), matumizi ya drones katika matibabu kama inavyofanyika nchini Rwanda, matumizi ya smartphones katika kuongeza maarifa ya kitaaluma na kiufundi stadi na kuongezeka kwa biashara za mtandaoni (e-commerce businesses, network marketing and online businesses). Bill Gates amewahi kuandika katika moja ya tweets zake “If your business is not on the Internet yet, Your are out of the Business.” Mwenye macho haambiwi ona.

SEKTA BINAFSI, INJINI YA UCHUMI AFRIKA

Kama ulikua hufahamu, basi sekta binafsi ndio imetawala Uchumi wa Afrika kwa kuwa zaidi ya 80% ya uzalishaji mali mzima hufanyika katika sekta hio. Zaidi, theluthi mbili (⅔) ya uwekezaji mzima barani na robo tatu (¾) ya jumla ya mitaji katika uchumi kati ya mwaka 1996-2008 imeonekana kutokea katika sekta hio binafsi. Vile vile sekta hio inatoa 90% ya ajira zote kwa vijana walio katika umri wa kufanya kazi. Mchango wa biashara za ndani katika sekta binafsi katika GDP ilikua 59% katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ukilinganisha na 30% ya nchi za Latin America na Caribbean, 32% Asia Kusini na 42% katika Mashariki ya Kati. Hii inaonyesha kiasi gani Afrika sekta binafsi inalipa maradufu. Umeiona nafasi yako hapa ndugu yangu mfanyabiashara.!?

Kujiimarisha katika Sekta binafsi, huna budi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kila mara unapohitajika kufanya hivyo. Unawezaje kufanya maamuzi sahihi katika changamoto zinazokukabili? Tafadhali fuatana nasi katika makala hii hapa FANYA MAAMUZI SAHIHI KATIKA MUDA SAHIHI.

Katika nchi za Uchumi wa kati, kampuni binafsi hufanya kazi katika mfumo wa sekta rasmi, ambapo makampuni makubwa na yale madogo (SME’s) huzalisha hisa za thamani katika uwekezaji na zaidi, ajira kwa vijana ambao ndio kundi kubwa zaidi katika nguvu kazi barani Afrika. Lakini zaidi, sekta binafsi katika nchi hizi hufanya ⅔ ya uzalishaji mzima.

Uchumi huwa na ushindani pale kunapokuwa na ushindani mkali wa kibiashara. Na biashara huwa na ushindani pale:

•Sheria zinapokua sawa na haki.

•Wafanyakazi wana maarifa stahiki.

•Gharama za uendeshaji (umeme, maji, mafuta, usafiri) zinakuwa nafuu.

•Wateja wanafikika kila kona.

ICT INAINGIA VIPI HAPO?

Uchumi wa kidijitali umekuwa dhima kuu ya kidunia na Afrika haijabaki nyuma katika hili. Matumizi ya teknolojia yanazidi kushika kasi barani yakichagizwa na kasi ya ueneaji wa huduma za internet ambapo biashara nyingi zinazidi kuhamia mtandaoni kirahisi. Mpaka kufikia mwaka 2015 tu tayari watu 557 barani walikua wanatumia simu ya mkononi ambayo ni 12% ya watumiaji wote wa simu duniani huku idadi hio ikikusanya 6% ya mapato yote yaliyofanyika duniani wakati huo.

Sasa leo wacha tuone maeneo muhimu ya ICT yanayokuza uchumi zaidi;

1. TELECOMUNICATIONS

Eneo hili linajumuisha makampuni makubwa ya mawasiliano. Kwa kiasi kikubwa hufanya shughuli zake katika utaratibu wa sekta rasmi, hivyo kuwafikia watu wengi na kufanya kazi karibu zaidi na mamlaka za serikali. Makampuni kama Vocacom, MTN, Tigo, Airtel na TTCL yapo hapa. Kutokana na kuwa na watumiaji wengi, makampuni haya huchangia kiasi kikubwa katika mapato ya kiserikali kama kodi na gawio huku yakichangia sehemu kubwa katika kukuza uchumi wa watumiaji wake kutokana na fursa zinazopatikana katika huduma wanazozitoa kama uwakala wa huduma, huduma za kifedha nakadhalika.

2. SOFTWARE AND IT CONSULTING

Hapa ndo utatukuta sisi sasa ambao tunakuhudumia wewe muda huu. Zaidi ya kukupatia taarifa hizi ghafi, pia eneo hili la ICT hutoa huduma za kutengeneza mifumo ya computer, Apps za simu, Ushauri na Uchambuzi wa kiteknolojia katika Biashara na Uchumi. Japokuwa sio maarufu sana lakini sehemu hii inachangia uchumi wa mabiashara mbalimbali, makapuni madogo na yale yanayokuwa (SME’s) pamoja na sekta zingine za uma na binafsi kwa kutoa huduma za matengenezo ya tovuti, mifumo mbalimbali ya kibiashara, huduma za afya, elimu, uhifadhi wa data pamoja na uchambuzi na ushauri wa biashara mbalimbali kiteknolojia zaidi.

3. DIGITAL SERVICES

Hapa utawakuta watu wanaotoa huduma za kidijitali ambao wengi wao hufanya kazi kwa ukaribu na makampuni ya mawasiliano. Watoa huduma hawa pia wanahusika kutengeneza mifumo ya makampuni ya mawasiliano pamoja na kutengeneza/kuendesha mitandao ya kijamii zaidi. Watoa huduma hawa wamekuwa wakitengeneza michezo ya video pamoja na kutoa huduma za WebHosting na Cloud services kwa makampuni ya Kiafrika. Kampuni kama Dudumizi Technologies(Tanzania), ISB North Africa (Morocco), Web4Africa (Ghana) na Domains Africa Technologies (Kenya) zipo hapa.

4. INFORMATION SERVICES

Hapa sasa ndio utazikuta redio na televisheni zote unazozifahamu. Hawa kwa jina lingine wanaitwa Watoaji wa Maudhui, ambapo hutafuta habari na maudhui wanayodhani yanafaa kwa wateja wao na hivyo kukusanya jamii ili ipate maudhui hayo huku yenyewe yakijipatia faida yake katika matangazo mbalimbali ya kibiashara yanayoruka sambamba na maudhui yao. Hapa unaweza kunitajia Redio/TV ambayo ina maudhui unayoyapenda yakienda sambamba na matangazo ya wadhamini wa vipindi vyao. Usishangae ukiona hivyo. Kwenye matangazo ndo wanapopatia pesa wenzio, usione unapata bure maudhui hayo.

Kwa uchache haya ndio mambo ya fahamu mchango wa ICT katika maendeleo ya sekta binafsi barani Africa yanayochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa Uchumi wa Kidijitali na kuboresha biashara nyingi zaidi kila kukicha barani Afrika. Jiulize, unayatumia vipi maeneo haya katika kukuza biashara yako wewe kama mjasiriamali?

Makala hizi hapa chini zitakusaidia kufahamu kwa undani namna sekta binafsi zinachangia uchumi na maendeleo ya wafanyabiashara hasa vijana wa Afrika Mashariki. Gusa links kisha makinika:

  1. KWANINI NI MUHIMU KUWA NA WEBSITE (TOVUTI) RASMI YA BIASHARA YAKO?
  2. UKIRITIMBA KATIKA BIASHARA, NI ASALI AU SHUBIRI?
  3. UNAFAHAMU NINI KUHUSU URASINISHAJI (HARMONIZATION) KATIKA BIASHARA

Usisahau kutoa maoni yako kuhusu ukichojifunza katika makala hii ya leo na unaweza kusambaza ili kuhakikisha ulichijifunza kinawafikia wengine. Pia unaweza kutembelea tovuti yetu maridhawa ya https://rednet.co.tz kuhakikisha unaendelea kupata taarifa sahihi kuhusu uchumi na biashara yako kiteknolojia. Asante.

Makala hii ni Kwa Heshima ya Hayati B.W. Mkapa aliyekuwa Rais awamu ya 3 nchini Tanzania. Mzee Mkapa aliongoza Taifa kuelekea zama hizi za maendeleo ya Sekta Binafsi kupitia Sera yake ya Ubinafsishaji wa mali za umma zilizokua mzigo kwa serikali, hivyo kuchochea ukuaji wa sekta binafsi kwa kiasi kikubwa mpaka kufikia hivi ilivyo leo. Mzee aliona mbali sana. #RIPMkapa

mapinduzi ya viwanda

FAHAMU KUHUSU MAPINDUZI YA 4 YA VIWANDA KATIKA BIASHARA DUNIANI

Japokua ilipitwa na zama 3 tayari, lakini sasa Afrika imedhihirisha kwamba haitaki kupitwa tena katika Mapinduzi ya 4 ya viwanda Duniani. Hii ni kutokana na kukua na kuimarika katika sekta za Afya, Elimu, Biashara, Teknolojia pamoja na Mahusiano na Muingiliano wa kijamii ikichagizwa na maendeleo katika miundombinu, usafirishaji na mitandao ya kijamii. Leo tuta fahamu kuhusu Mapinduzi ya 4 ya viwanda katika biashara duniani. Ni nini na yanaashiria nini kwenye maendeleo ya biashara zingine? Makninika mpaka mwisho.

Mwezi September, 2019, jijini Cape Town Afrika Kusini ulifanyika mkutano wa kiuchumi wa WEF (World Economic Forum) ambao unazishirikisha nchi mbali mbali duniani, wafanyabiashara pamoja na wadau wa uchumi.

Mwaka huo 2019 viongozi waliokutana kujadili mustakabali wa Afrika walikua na jambo la msingi sana ambalo linatumainiwa kuleta maendeleo katika uchumi barani ambalo ni Utekelezaji wa Kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara Barani (African Continental Free Trade Area AfCFTA). Baada ya miaka mingi ya mazungumzo, makubaliano yamefikiwa ya jinsi ya kuvunja vikwazo vya kibiashara, kukuza uchumi na kuunganisha nchi ambazo katika historia zilikuwa na mahusiano mazuri ya kibiashara na bara Ulaya, Amerika na Asia. Kufahamu zaidi gusa hapa chini:

Changamoto; Afrika (wafanyabiashara, kampuni na mashirika) imejifunza nini katika Kongamano hilo la Kiuchumi (WEF)? Na zaidi, Afrika inajiandaa vipi na Mapinduzi ya 4 ya viwanda yanayoendelea duniani?

Kufikia mwaka 2018 Afrika peke yake iliripotiwa kuwa na vijana takribani milioni 200 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24. Na namba hio inatajwa kuongezeka mara mbili kufikia mwaka 2050.

Sasa “Kuwa na bara lililosheheni vijana ni fursa adhimu sana, lakini vile vile ni tishio kubwa.” alitahadharisha Albert Zeufack, Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia barani Afrika. “Ni tishio kama hatutohakikisha idadi hio ya vijana hawaanzi kufanya kazi inavyotakiwa.” Sasa kufikia Mapinduzi ya 4 ya viwanda, maeneo kadhaa yaliangaziwa na kituo cha mabadiliko ya kiuchumi barani (Africa Center for Economic Transformation, ACET) kwa niaba ya Benki ya maendeleo barani AfDB.

africa na mapinduzi ya viwanda

1. MACHINE LEARNING/ARTIFICIAL INTELLIGENCE/ROBOTICS;

Fikiria kuhusu gari inayojiendesha bila dereva na kufuata sheria na alama za barabarani ipasavyo ikijumuisha foleni. Watu wengi wangesita kupanda katika gari inayojiendesha yenyewe bila dereva, lakini hayo ndio mapinduzi halisi ya viwanda kupitia teknolojia.

Pia eneo hili limeshuhudiwa na ubunifu mwingi ukiwemo; mashine za kisasa za kuvuna na kupembua nafaka na madini, mifumo ya kiautomatiki inayoendesha ndege, meli pamoja na Teknolojia ya kupima udongo. Ni wazi mashine zinaweza kufanya kazi zifanywazo na binadamu katika zama hizi za mapinduzi ya 4 viwanda.

Swali, umejiandaeje kulinda taaluma yako dhidi ya zama hizi za mashine kujifunza (machinelearning) pamoja na teknolojia ya akili isiyo ya asili (ai)?

2. INTERNET OF THINGS (IoT);

Vifaa vingi vya kielektroniki vinavyotumiwa na mwanadamu sasa vinao uwezo wa kuingiliana na vifaa vingine kirahisi katika kurahisisha utendaji. Fikiria pale unarudi nyumbani na kuwasha feni yako kwa kutumia simu yako ya rununu (smartphone). Au kuweza kuendesha jokofu lako kwa kutumia teknolojia ya RFID. Kuunganishwa vifaa vya kielektroniki na huduma za intaneti imerahisisha sana mfumo wa mawasiliano na manunuzi ambao umeinua uchumi japo faida zake bado hazijasambaa sana barani Afrika.

Fikiria vile unaweza nunua bidhaa katika duka bila kumwona hata muuzaji. Hii inawezeshwa na teknolojia za biashara za kielektroniki (ecommerce) ambapo mteja anaweza kulipia kwa kutumia kadi yake ya benki au huduma za kifedha za simu ya mkononi kama MPESA na tigopesa. Katika bara ambalo muingiliano ni mkubwa kama Afrika, hili ni jambo la kutilia maanani sana, haswa wakati huu ambapo unajaribu ku fahamu kuhusu Mapinduzi ya 4 ya viwanda katika biashara duniani. (Ambapo sisi kama Rednet Technologies ni wadau wakubwa kuhakikisha hupitwi na huduma za kisasa kwa kutumia teknolojia).

Kufahamu mapinduzi ya IoT katika biashara na maisha kwa ujumla tayari tumekuwekea makala maalum kupitia link hii hapa MAGEUZI YA INTANETI (IoT) KATIKA BIASHARA NA MAISHA

3. DATA MINING/DATA SCIENCE TECHNOLOGIES;

Kituo cha ACET katika mwaka 2018 kiligundua kwamba “kuvua taarifa nyingi mtandaoni, kwa kutumia kompyuta zenye uwezo mkubwa na kanuni za mifumo ya Akili isiyo ya Asili (AI), huwezeshwa kupatikana kwa ripoti bora ya taarifa sahihi.” Fikiria mifumo ya tiketi za ndege, hoteli, mifumo ya kulipa kodi na taarifa za mteja wa benki.

Sekta ya Takwimu inafurahia sana ujio wa teknolojia ya Kuvua/Kuvuna Taarifa na Sayansi ya Taarifa. Jinsi ya utendaji katika teknolojia hii ni fursa adhimu sana katika kuimarisha biashara kwa kutumia takwimu sahihi zilizovunwa kutokana na taarifa mbalimbali za watu. Mifumo ya tiketi za ndege, Usajili wa vyumba vya Hoteli, taarifa za wateja wa benki na hata mfumo wa Kulipa kodi (Tax returns), hivi ni baadhi ya vyanzo vya ukusanyaji wa taarifa muhimu katika kufanya Uvunaji wa Data na Sayansi ya Data. Serikali za Africa zinamiliki kiwango kikubwa cha taarifa hizi. Je, italeta manufaa kwa Umma au itafanywa kama biashara na wajasiriamali? (Tafiti na ripoti tunazokuwekea kwenye makala zetu hizi zitakupa majibu.😋)

4. 3D PRINTING;

Ama kwa hakika mapinduzi ya viwanda yanakuja na mengi. Hebu buni bidhaa yako kwenye kompyuta halafu ichapishe kama ilivyo. Kutoka ubunifu uliotengenezwa kimchoro mpaka uhalisia katika kuchapisha tu, hii inakwenda kubadili hata namna ya uendeshwaji wa viwanda barani Africa ambapo ugunduzi huu unaleta matumaini katika uwanda wa ubunifu na ujenzi ambao unatazamiwa kuleta maendeleo katika nchi za Afrika. Viwanda vinawezaje kuendana na teknolojia hii ya Uchapishaji? Vimal Shah mkuu wa shirika la viwanda vya BIDCO nchini Kenya mwaka 2017 alinukuliwa akitania, “Tunaweza kuchapisha pizza wakati ujao.”😂

Sasa watunga sera na sheria barani walishaona uhalisia huu kama kuchapisha mfano wa kitu halisi (3D-Printing) katik mipango yao ya muda mrefu?

5. BLOCKCHAIN/TRUST TECHNOLOGIES;

Mwaka 2018 kituo cha ACET kiligundua kwenye uchunguzi wake kwamba teknolojia ya Blockchain inawafanya watu hata wasiaminiana au kujuana, kuweza kushirikiana bila ya kuwa na haja ya kwenda kwenye mamlaka za serikali. Yaani Blockchain ni jalada huru linalosajili miamala ya kifedha kati ya watu wawili au zaidi kwa usahihi na njia bora zaidi. (Tulishaelezea kuhusu Blockchain na cryptocurrencies kwenye makala zetu zilizopita). Sasa itakuaje kwa huduma za kibenki, wanasheria, wakala wa fedha (brokerage firms) na wahusika wa kiserikali katika maswala ya kifedha? Kitawakuta nini, tutajadili kwenye athari ya mapinduzi ya viwanda mbeleni.

mapinduzi ya viwanda

Si ajabu, teknolojia ya Blockchain inaonekana kama mkombozi dhidi ya vitendo vya Rushwa kutokana na undeshwaji wake ulio sahihi na wa haki. Kwa inavyoonekana teknolojia hii ya Blockchain inakwenda kuwa pigo kubwa kwa watu wenye misuli ya kiutawala, madikteta wa waendeshaji wa siasa chafu. Itakapofika siku Teknolojia hii imefikia matumizi yale yaliyonuiwa wakati inaanzishwa, basi wahafidhina na mawakala wa kifedha wa serikali na mashirika binafsi watapoteza nguvu zao. Hakutakuwa na haja ya mihuri, wala sahihi, wala zile nenda urudi kesho tukuhudumie. Blockchain itakwenda kuiweka Afrika huru dhidi ya kero za huduma za kifedha na usalama wake kuwa katika ukuaji mzuri. Haya ndio mapinduzi ya 4 ya viwanda duniani.

5. BIOPHYSICS AND BIOENGINEERING;

Eneo la 5 ambalo kituo cha ACET imeliacha ni kuhusu mtandao wa mifumo ya kibaolojia na kifizikia. Utahitaji mkono wa bandia unaoweza kuendeshwa na ubongo wako kwa usahihi ikitokea mkono wako halisi umekatika? Hebu fikiria hapo. Tunakubali kwamba asili ni bora sana kuliko sisi, hivyo ni bora kujifunza kwayo, kwasababu mapinduzi haya ya viwanda kwa kuchagizwa na ukuaji wa kiteknolojia duniani yatafanya taaluma ziweze kunyumbulika kwa namna nyingi sana hapo baadaye. Je, mifumo ya elimu imejiandaa na hili katika maandalizi ya mitaala yake ya muda mrefu?

Sasa tumeshajua yanayokuja na Mapinduzi ya 4 ya viwanda duniani. Afrika, bara ambalo ajira bado ni tatizo kubwa kwa vijana, wataweza vipi kupambana na athari za mapinduzi haya? Kuna nadharia tatu (3) katika kukabiliana na hali hii;

1. Afrika inaweza kuketi chini na kubaki kutizama dunia nzima ikipambana katika Mapinduzi haya. Hii ilishafanyika katika zama 3 zilizopita za Mapinduzi ya viwanda ambapo Mapinduzi ya Kwanza yaliegemea katika kutengeneza mifumo ya Kimekanika na matumizi ya Injini za mvuke katika kutengeneza bidhaa kama nguo.

Mapinduzi ya pili yakiwa ni kuhamasisha Uzalishaji mkubwa (mass production) wa bidhaa viwandani yakichagizwa na Henry Ford na awamu ya 3 ya mapinduzi ikiwa ni zama za kidijitali katika uzalishaji.

Ukitizama elimu ya msingi ya kuunda Injini ni ile ile iliyokuwepo tangu mwanzo, lakini bado Afrika haijaweza kutengeneza magari yake yenyewe.

2. Afrika inaweza kufanya kile ilichokifanya katika kuingia kwenye zama za Kidijitali, mtindo wa kuruka kama chura (leapfrog). Kwa mfano nchini Kenya watu hawakuwa na huduma za simu za mezani miaka ya 1990’s kurudi nyuma, hali kadhalika ilikuwa hivyo nchini Tanzania pamoja na nchi nyingi za kusini mwa jangwa la Sahara katika ku fahamu kuhusu Mapinduzi ya 4 ya viwanda katika biashara duniani.

Lakini baada ya mwaka 2000 watu wengi katika eneo hilo wameweza kumiliki simu za mkononi hata kama hawakuwahi kumiliki simu za mezani. Simu za mkononi zimekuja na teknolojia kubwa zaidi baada ya kuunganishwa na huduma za kifedha kama MPESA, huduma za internet, GPS na ramani, huduma za kiafya pamoja na biashara za kielektroniki ecommerce.

Mazingira ya Uchumi jumuishi (social economy) yanafanya iwe rahisi kukaribisha zama za Mapinduzi ya 4 ya viwanda. Watu wengi duniani hawapendi kusoma vitabu, hivyo sasa tunaweza kuziachia mashine kufanya kazi mbalimbali badala yetu. Kama Blockchain inatazamwa kwenda kuangamiza kabisa changamoto ya rushwa, Teknolojia ya 3D-Printing itafanya hata nyumba zetu kuwa viwanda vidogo katika kubuni bidhaa mbalimbali.

Taarifa zote zilizo kwenye mashirika ya Serikali na binafsi ikijumusha taasisi za dini zinaweza kuvunwa kwa ajili ya kupata takwimu mbadala katika chunguzi mbalimbali. Hii inatazamwa kuwa njia mbadala kuyafikia mapinduzi ya viwanda ya 4. Unahitaji kuLeapfrog biashara yako (kuepuka gharama kubwa za matangazo)? Tunalo suluhisho, wasiliana nasi mara moja tukupatie.

3. Vile vile, Afrika inaweza kukuza thamani ya uzalishaji na ubunifu wake ili kuwa mshindani halisi duniani katika kutengeneza na kusambaza bidhaa na huduma za kiteknolojia, kama inavyofanyika mahali kwingine duniani.

Japan imeweza kufanya hivyo katika sekta ya magari na India inafanya vizuri katika sekta ya Famasia na Programu za Kompyuta. Sasa kwanini Tanzania isiwe kinara katika Sayansi ya Data(Data Science) duniani. (maana mbongo mpe picha tuu, vingine utaona atakapovipata😂. Natania.) Sekta hizi za teknolojia zinataka matumizi ya akili zaidi, sio kama viwanda vya saruji na chuma ambavyo vinahitaji mtaji mkubwa wa kifedha.

Mfanyabiashara, umejiandaa vipi kuyapokea Mapinduzi haya ya 4 ya Viwanda katika eneo lako la biashara? Pitia makala hizi ili kupata taarifa zaidi:

  1. IFAHAMU NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO
  2. BANDO LAKO NI MTAJI
  3. FAHAMU SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA
  4. KUANZISHWA KWA ENEO HURU LA BIASHARA BARANI AFRIKA, KUNA MANUFAA GANI KWAKO?

Je umependezwa na makala yetu hii ya leo?

Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?

Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.

Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.

mapinduzi ya 4 viwanda katika biashara duniani