IFAHAMU AINA MPYA YA UDALALI WA MTANDAONI (DROPSHIPPING)
Dunia inakwenda kasi sana na Teknolojia inazidi kusambaa na kuteka sekta za kiuchumi. Mwandishi mmoja alinukuliwa akisema “In this modern world, prepare to change your career.” Umeshafikiria kuwa Dalali smart? Leo sasa ifahamu aina mpya ya udalali wa mtandaoni (Dropshipping) kwa undani. Ni nini na inafanya kazi vipi? Makinika mpaka mwisho wa makala hii..
Kwa Afrika yenye watumiaji wa huduma za internet wanaokadiriwa kuzidi milioni 400, tafiti zinaonyesha fursa za kuongezeka kwa biashara za mtandaoni (e-commerce) sasa ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote. Shirika la Statista linakadiria sekta ya e-commerce kufikia thamani ya US 29$ milioni kufikia mwaka 2022.
DROPSHIPPING NI NINI?
Hii ni aina ya Udalali wa kimtandao ambapo Mtu wa kati (Dalali) huchukua Oda kutoka kwa Mteja kisha huituma Oda hio kwa Mwenye Mali (Muuzaji) ambaye hukamilisha mauzo kwa Mteja na kumwachia Dalali Kamisheni yake stahili.
Lakini wakati mwingine hasa barani Afrika huyu Mtu wa Kati huchukua Oda kutoka kwa mteja kisha huenda kwa Mwenye mali na kuchukua Bidhaa na kisha kwenda kuiuza yeye moja kwa moja kwa Mteja. Hii ndio kitu inafanyika sana Afrika kama ulikua hujui.
Hata hivyo msingi Mkuu wa Dropshipping ni kuwa namna hii ya Biashara hufanywa na Mtu wa kati ambaye hana stock kabisa (haihitaji uwe na mtaji wa fedha au bidhaa ili kufanya dropshipping). Kwa hiyo Dropshipping ndiyo kinara katika aina za biashara za mtandaoni (e-commerce).
Hii Dropshipping ni biashara moja ambayo mtu yeyote hasa kijana anaweza kabisa kuifanya kwa kuwa haihitaji uwe na mtaji wa kifedha ama bidhaa (stock). Hata hivyo, kama zilivyo biashara zingine, sio biashara rahisi wala sio biashara ambayo inaweza kukutajirisha mara moja.
Unahitajika kuwa mbunifu, mwenye juhudi na mvumilivu ili uweze kufanikiwa kwenye aina hii ya biashara kwa kuwa:
1. KIWANGO CHA FAIDA NI KIDOGO: Kiwango cha faida hutegemea kamisheni au “cha juu” ambacho mara nyingi hakiwi kiwango kikubwa. Hivyo ili uweze kupata Faida kubwa inakubidi pia uhakikishe bidhaa/huduma nyingi zimemfikia mteja kupitia wewe.
KUMBUKA: Kila mauzo unayoyafanya hapa, kiwango kikubwa cha pesa humwendea Mwenye Mali, kile “Cha juu” ndio hubaki kuwa halali yako.

ZINGATIA: Waswahili wanasema, “Ongea na watu uvae viatu” Ukitafsiri vizuri hii nafasi ya kufanikiwa ni kubwa kwa sababu kadiri unavyokuwa na watu wengi zaidi katika mtandao wako basi nafasi yako ya kutengeneza faida inazidi kuwa kubwa.
2. USHINDANI NI MKUBWA: Hii ni aina ya bishara ambayo ushindani wake ni mkubwa kweli kweli. Fikiria haihitaji mtaji wa Kifedha wala bidhaa(stock) ili kuanza kuifanya, watu wangapi wanaweza kuifanya? wangapi tayari wanaifanya sasa hivi? Hivyo ili ufanikiwe, lazima ukomae kweli.
3. UHALALI/UBORA WA BIDHAA: Mara nyingi hii sio kesi kubwa lakini huwa inatokea. Ni mara ngapi imetokea mteja ameona bidhaa fulani kupitia ukurasa wako(mtu kati) wa mtandaoni, halafu vile umeenda kwa Mwenye Mali ukakuta ile bidhaa iliyoonekana kwenye picha mtandaoni sio ile halisi uliyoikuta kwa Mwenye Mali. Hili jambo ni baya na linaumiza sana watu wa kati na wakati mwingine hushusha heshima na uaminifu ambao wameutengeneza kwa wateja wao kwa muda mrefu sana.
Wakati mwingine hutokea hata mwenye mali si halali kisheria au/na wewe (dalali) hufahamu hata bidhaa unazozichukua ili kupeleka kwa mteja zinatoka wapi. Swala la bidhaa feki linaathiri sana kipengele hiki ambapo hutokea bidhaa iliyoonekana mtandaoni kuwa na logo fulani inayoaminika, lakini ile iliyo kwa ground inakuwa logo ya kughushi/feki. Hivyo lazima uwe mwangalifu.
4. UGUMU WA KUTENGENEZA BRAND: Ukiwa mfanyabiashara wa aina ya Dropshipping, fahamu kuwa sifa ya ubora wa bidhaa mara zote itakwenda kwa Mwenye Mali tu. Kitachokufanya uendelee kubaki kwenye game ni namna yako nzuri ya kuhudumia wateja wako wote bila ubaguzi na kwa ubora wa juu.
Kutengeneza Brand ni muhimu sana. Brand haijengwi kwa siku moja hata hivyo, ni mchakato wa muda mrefu. Sasa kuelewa zaidi kuhusu Brand (ni nini na inafanyika vipi) gusa link hii hapa Branding vs Marketing, kipi ni kipi?
Kumbuka: sio Logo yako iliyo kwenye bidhaa. Hivyo tengeneza SUMAKU yako kwa kutumia aina ya maneno yanayoweza kuuza bidhaa (copywriting), matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii pamoja na website bora na ambayo imeunganishwa na huduma za S.E.O.
Hizo ni baadhi ya Changamoto ambazo unategemea kukutana nazo katika aina hii ya biashara mtandaoni. Hata hivyo, kuna namna ambayo unatakiwa ujipange ili kuhakikisha Biashara yako inakuwa na mafanikio zaidi na uwezo wa kupambana na changamoto.
Kipi cha kufanya ili ufanikiwe katika Udalali huu wa Mtandaoni (Dropshipping)?:
1. CHAGUA HADHIRA YAKO: Haya ni mazingira na aina ya watu ambao unajihusanisha nao kila siku mtandaoni. Fahamu kuwa aina ya watu unaojihusanisha nao ni muhimu katika kutengeneza Aina ya soko linalofaa kwa bidhaa zako. Pia aina ya watu inaweza kukuambia ni aina gani ya bidhaa itawafaa kulingana na changamoto unaziziona zikiwatatiza kutoka kwao. Hapa lazima uwe na jicho zuri la kuona kile watu wengi hasa wafanyabiashara wenzako hawakioni. Kuwa Mchunguzi kidogo, hala hala usije kuwa mbea tu. Kwa vyovyote unapokua dalali hasa wa mtandaoni lazima ujitangaze, Kwanini ujitangaze sasa fuatana na makala hii hapa kufahamu zaidi..
2. TAFUTA MFANYABIASHARA (MWENYE MALI) WA KUAMINIKA: Hiki ni kipengele muhimu katika kuhakikisha bidhaa zako zinaweza kupatikana kwa wakati bila longolongo wala ujanjaujanja. Mteja mara nyingi hununua kwa uhitaji ambao husukumwa na hisia. Hivyo hisia hizo zinaposhindwa kufikiwa ndani ya muda fulani, basi mteja anaweza kugairi au kununua kwa mtu mwingine.
Hapa ukiwa kama mfanyabiashara lazima ujue namna ya kutengeneza hali ya dharura kwa mteja ili anunue bidhaa yako kwa upesi, lakini zaidi lazima utimize haja ya mteja wako ndani ya muda na kwa uhakika.
3. CHAGUA BIDHAA YA KUUZA: Kabla hujaanza kufanya aina hii ya biashara lazima ujue hizo bidhaa zinazohusika “utamuuzia nani?”. Katika kuchagua unatakiwa uangalie Umri, Elimu, Makundi ya kijamii (wanafunzi, wasomi wa vyuo, wafanyakazi, wazazi, watu wa dini nk). Hivyo lazima ujue ni bidhaa zipi zinawafaa wateja na hadhira yako Kiujumla.
Njia nzuri ya kuchagua bidhaa zinazouzika sana ni kupitia majukwaa kama YouTube kupitia matafuto kama “top 10 products to sell” utajifunza mengi humo.
•Pia unaweza kutumia Majukwaa ya Amazon na AlliExpress kupata bidhaa zinazofaa kufanyia biashara unayotaka kuifanya.
•Chunguza matangazo (sponsored ads) kupitia mitandao kama facebook, instagram na twitter. Kwenye kuchagua aina ya bidhaa jitahidi kuepuka:
•Bidhaa za chakula ambazo zinahitaji uthibitisho wa mamlaka, huna muda wa kupeleka bidhaa ikathibitishwe TMDA/TBS kabla haijamfikia mteja.
•Bidhaa ambazo ni silaha. Hizi mara nyingi soko lake ni la shaka kwa wateja wengi, hivyo kizifanya kutokuwa reliable.
•Mambo ya Fashion: Najua hii ndio watu wengi wanapenda kufanya, lakini jitafakari kuhusu ushindani wake sokoni, Nadhani unawajua wanaouza nguo na viatu katika mitandao ya kijamii.
4. WEKA BIDHAA ZAKO MTANDAONI: Baada yakufanya yote hapo juu, hakikisha bidhaa zako zinaonekana mtandaoni. Njia nzuri zaidi ya kuweka bidhaa mtandaoni ni kupitia Website na Instagram kwa sababu bidhaa inatakiwa kuonekana kwa picha ili kumvutia mteja. Mitandao mingi ya kijamii haikupi nafasi nzuri ya kuonyesha bidhaa zako kwa wateja katika unadhifu unaotakiwa. Hata hivyo ni muhimu pia kutumia mitandao mingine ya kijamii katika kunadi bidhaa zako mara kwa mara kupitia ujuzi wa “Copywriting” vizuri.
Sasa nimekuwekea makala kupitia links hizi hapa chini ili kuhakikisha somo la leo unalielewa vizuri. Zitakusaidia sana ukizimaliza zote.
- UKIRITIMBA KATIKA BIASHARA, NI ASALI AU SHUBIRI?
- KWANINI NI MUHIMU KUWA NA WEBSITE RASMI YA BIASHARA YAKO?
- IJUE NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO
Nadhani leo ume ifahamu aina mpya ya udalali wa mtandaoni (Dropshipping) katika kiwango chake. Unalo lolote la kushare nasi? Tafadhali tujadili kupitia comment hapo chini.
Je umependezwa na makala yetu hii ya leo?
Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?
Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.
Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.
