Tag: uchumi wa kidijitali

thamani vs gharama, nafuu iko wapi? fahamu siri za kuweza kushawishi wateja katika biashara yako.

THAMANI vs GHARAMA, NAFUU IKO WAPI?

Ubora wa kazi una thamani kubwa sana kuliko gharama za kuifanya kazi hio. Unaweza lipia mradi kwa milioni 5, lakini usikupe matokeo yale ulijipangia mwanzoni. Pia unaweza lipa laki 5 ya mradi na ukapata matokeo mazuri zaidi. Ufanyeje? Je kati ya thamani vs gharama nafuu iko wapi? Fuatilia makala hii mpaka mwisho kufahamu zaidi.

Warren Buffet ambaye ni mbuji kabisa katika buruji la uwekezaji duniani amewahi kunukuliwa akisema “Price is what you pay, value is what you get.” akimaanisha, “Gharama ndio unayolipa, thamani ndio unayopata”. Kifupi ni kwamba thamani ndio msingi wa bidhaa/huduma huku gharama ikiwa ni makubaliano ambayo yanatangulizwa na muuzaji.

Kujua tofauti kati ya Gharama na Thamani ni moja kati ya mbinu bora zaidi za kufanya Uwekezaji. Zaidi kuhusu uwekezaji tayari tumeshakufahamisha SIRI ZA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA Ukishazifahamu hapo tuendelee..

Je kati ya thamani vs gharama, nafuu iko wapi?

umuhimu wa tehama

jinsi ya kufanikiwa katika biashara za mtandaoni

Unaposhindwa kutofautisha kati ya Gharama na Thamani kama mfanyabishara unajiweka kwenye mtego wa kukosa wateja, kutoaminika kwa Wawekezaji wakubwa, Kupoteza points dhidi ya washindani wako kibiashara na mwisho kuiweka biashara yako katika majanga ya kudhoofika na hatimaye kufa.

Unawezaje kupata bidhaa zinazouzwa kwa gharama za chini kuliko thamani yake halisi?

Jibu ni kufanya tathmini kwa kutumia viwango vya bei ambazo ni tofauti kabisa na gharama zinazotangazwa sasa. Hapa unaweza kuangalia bei, miaka 3 iliyopita ilikuaje na miaka 3 ijayo itakuwaje.

Bwana Phil Town, ameweka zoezi la kufanya Tathmini makini kwa kupitia hatua nne alizoziita “Four M’s“. Tuzione chap chap:

1. MEANING: Hatua ya kwanza kabla hujawekeza katika bidhaa/huduma fulani lazima ujiridhishe kuwa bidhaa/huduma hio ina maana sana kwako. Ikiwa na maana utapata fursa ya kuichunguza na kuielewa vyema, na kujituma ipasavyo katika kufanya biashara hio.

2. MOAT: (Upekee ambao hauwezi kuigwa na wengine): Unapochagua bishara ya kuwekeza ama bidhaa/huduma, unatakiwa uifanye iwe katika mtindo ambao washindani wako hawawezi kukuiga. Mfano: Duniani kuna makampuni mengi tu ya vinywaji laini (soft drinks) lakini Coca cola ni moja na itaendelea kubaki hivyo.

Hivyo hebu tuambie hapa biashara yako ina utofauti gani ambao washindani wako hawawezi kuiga kamwe?

3. MANAGEMENT: Je wajua kuwa Chanzo kikubwa kwa biashara kufa ni watu wanaoiendesha? Hivyo unapofikiria kuwekeza kwenye biashara lazima eneo ya utawala na uendeshaji wa shughuli linasimamiwa na watu wenye Weledi, Waaminifu na wanaojali maisha ya biashara hio.

4. MARGIN OF SAFETY: Kama umeshajiridhisha na hizo hatua 3 zilizopita, sasa hebu tizama pia namna unaweza kuweka mtaji ama kununua hisa bila kupoteza pesa na uhakika wa pesa yako kurudi.

Kila biashara inahitaji kitu fulani ambacho kitaitofautisha na washindani wake wengine sokoni. Sasa mchakato wa kutafuta tofauti hizo inaitwa “Positioning”. Hii mbinu inaziwezesha biashara kukazia sehemu fulani ya soko/wateja ili kujiimarisha zaidi kwenye sehemu hio. Unafanyaje?

MBINU ZA KUFANYA POSITIONING:

1. KUPUNGUZA GHARAMA: Ukifanya uchunguzi vizuri sokoni hasa kwenye mitaa ambayo wanafanya biashara ya aina moja mf: Kariakoo kila mtaa una shughuli yake maarufu zaidi kama mtaa wa livingstone ni maarufu kwa vyombo vya ndani.

So ukijigundua kuwa upo kwenye aina hii ya biashara, mbinu bora hapo ni kupunguza gharama za bidhaa zako kwa kiwango kidogo kuliko washindani wako. Lengo ni kuhakikisha unakuwa na mzunguko wa haraka wa mauzo ya bidhaa/huduma zako kwa faida ndogo ili mzigo wako uishe mapema.

Jinsi ya kuongeza mbinu za kulifikia soko la Mtandaoni

Je kati ya thamani vs gharama, nafuu iko wapi?

2. UBORA: Kama unataka kujitofautisha na washindani wako, basi mbinu bora na ya kuaminika ni kuhakikisha bidhaa/huduma zako ni za Ubora wa hali ya juu. Unapozingatia Ubora unajiweka kwenye nafasi ya kupata wateja wa kuaminika, wateja wa kudumu na wateja wa uhakika katika biashara.

3. MAKUNDI YA KIJAMII (DEMORGRAPHIC): Baadhi ya biashara huamua kujihusisha na makundi fulani tu ya kijamii ili kujiletea faida zaidi. Mfano: kwenye TV na redio vinatengenezwa vipindi mahsusi kwa Vijana, watu wa makamu na watu wa dini fulani kwa siku zao. Umeshawahi fanya hii?

Mbinu hii inafaa sana pale unapoyapata makundi hayo karibu na eneo lako la biashara au watu wanaokufuatilia zaidi mtandaoni wakawa ni wanamna hio. Vinginevyo unajiweka kwenye hatari ya kukosa soko kubwa nje ya hao uliolenga kuwahudumia.

4. HUDUMA BORA: Huwa inatokea kwa baadhi ya biashara ushindani unakuwa mkubwa sana kiasi kwamba mbinu 3 tulizoziona awali haziwezi kufanya kazi. Yani watu wanashikana kooni haswa. Hapa ndipo mbinu ya kutoa Huduma Bora kwa wateja inapokuja kuleta tofauti.

Zoezi la kutoa Huduma Bora ni pana na linahitaji ubunifu mwingi. Na hii inatoa fursa kwa biashara kubuni namna nzuri ya kuhudumia wateja wake ili kuhakikisha wateja wanafurahia bidhaa/huduma na kuzidisha mauzo. Mfano: unaweza kuanzisha dawati la wateja kutoa maoni live ili waweze kuona mawazo yao yakifanyiwa kazi. Unaweza kuanzisha kurasa za mitandao ya kijamii ili kukusanya kero za wateja na kuzifanyia kazi vizuri. Pia unaweza kutengeneza mzunguko kwa wateja wako kushiriki kama mabalozi wa kuitangaza biashara yako kwa watu wengine. Unaionaje hii?

UNAWEZA VIPI KUDADAVUA NA KUWASILISHA THAMANI YA BIASHARA YAKO KWA MTEJA WAKO?

Tafiti zinaonyesha kuwa watu hawapendi kabisa kutangaziwa ama kulazimishwa kununua kitu hasa huku mtandaoni. Mfano: Tizama unavyopata kero pale unapoangalia vidio YouTube mara katikat linakuja Tangazo Ama pale unataka kufungua ukurasa fulani mara unafunguka ukurasa wa tangazo kwanza kabla hujafika pale ulitaka kwenda. Hio kero ndio inatakiwa ikufanye uitazame biashara yako katika jicho la Kitaalamu kwa kutatua changamoto na si la Kibiashara kwa kuuza Bidhaa/huduma yako.

Unapotoa Elimu katika namna ya Utaalam wa kutatua changamoto fulani, unamfanya mteja atake kuondokana na kero zinazomsumbua kwa kutumia Bidhaa/Huduma zako. Hii ni tofauti kabisa pale unapotaka kuuza bidhaa. Ukifanya hivyo hutatui changamoto bali unakuwa kero kwa mteja.

Uongozi vs Utawala katika miradi/biashara, kipi kinafaa zaidi?

gharama vs thamani, kipi kinafaa zaidi?

Thamani ya Biashara yako inaonekana katika kutatua changamoto za mteja wako na Urahisi wa kutumia bidhaa/huduma yako. Hivyo lazima uhakikishe kuwa unachokitangaza ni Ile Namna na hisia ya Bidhaa zako zinaweza kutatua changamoto fulani ya mteja kwa urahisi.

Pia lazima uhakikishe suluhu yako inakwenda sambamba na hisia za mteja wako. Kwa kuwa kitaalam watu hununua bidhaa/huduma kutokana na hisia walizo nazo muda huo. Mfano kuna watu watakwambia kuwa wakiwa na hasira ama furaha sana kwao huo ndo muda wanafanya shopping kubwa zaidi.

Mzazi anapotaka kununua keki ya birthday ya mwanae hanunui tu keki tamu, lazima pia ahakikishe keki hio inakwenda kum-suprise mtoto kwa muonekano wake wa kuvutia. Ni mbinu ya kihisia hapo inatumika. Hivyo unapotaka kuongeza Thamani ya biashara yako unatakiwa kuzingatia hilo pia.

Umejifunza nini kwenye makala hii kuhusu thamani vs gharama, nafuu iko wapi? Tafadhali weka maoni au mtazamo wako katika sehemu ya comments hapo chini..

Vyanzo: https://www.forbes.com/sites/forbesfinancecouncil/2018/01/04/the-important-differences-between-price-and-value/?sh=133fd5c94237

https://www.weebly.com/inspiration/difference-between-value-and-cost/

https://yourbusiness.azcentral.com/different-types-strategies-business-1348.html

Biashara yako inaweza vipi kuwa taasisi imara

BIASHARA YAKO INAWEZA VIPI KUWA TAASISI IMARA

Biashara nyingi zimekuwa zikiendeshwa katika mtindo wa “Kujiajiri” ambapo wajasiriamali wengi huteseka wakifanya kazi kwa bidii usiku na mchana lakini hujikuta siku moja tu wasipofanya kazi basi biashara inashindwa kuzalisha. Yaani mfanyabiashara unajikuta unakuwa mtumwa kwenye biashara yako mwenyewe? Hio dhana ya kujiajiri inakuwa na maana gani sasa? Leo sasa tuangalie Biashara yako inaweza vipi kuwa taasisi imara inayojitegemea? Makinika mpaka mwisho wa makala hii.

Septemba 21 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Amani. Sasa katika Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (UN), Lengo Na. 16 limekazia katika kudumisha Amani, Haki na Taasisi Imara. Amani ni mbolea muhimu katika ukuaji wa uchumi mahali popote. Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa uliokaa mwaka 2001 ulithibitisha kuweka Siku maalum ya kutafakari na kudumisha Amani, Haki na Taasisi Imara duniani, ambapo siku hio ni September 21 kila mwaka.

Hii ni kutokana na vitendo vya uvunjifu wa amani, taasisi dhaifu na kukosekana haki si za kidemokrasia katika utendaji, serikali hizi ambazo mara nyingi huwa ni za kidikteta au za kifalme, mara nyingi huendeshwa kwa sheria zinazokandamiza upande mmoja na kuimarisha kikundi kidogo cha watu kwa maslahi yao binafsi.

Jambo hili hutokea pale viongozi (watu wanaopewa dhamana) kushindwa kuwajibika kwa wanachi na hivyo kujiundia sheria ambazo zinawapa mamlaka ya kutumia rasimali za nchi huku zikiwaacha wanachi katika hali ya upofu wasiwe na nguvu ya kuuliza na kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali zao. Hili ni jambo baya na linalopaswa kuagamizwa mahali popote kwanzia ngazi ya familia, biashara, kampuni, shirika mpaka serikalini.

Mwandishi mahiri Robert Kiyosaki katika kitabu chake cha CASH FLOW QUADRANT amefafanua kwanini Matajiri huendelea kuwa matajiri huku Watu wa Uchumi wa kati wakiendelea kukimbia mbio za panya na masikini wakizidi kuwa masikini. Kwa haraka haraka, katika Njia 4 za kuingiza mapato ambazo zimeonyeshwa kwa herufi za E, S, B na I, zimetajwa kuwa ndio chanzo kikuu cha mapato ya watu duniani.

SEHEMU ZA KUIFANYA BIASHARA YAKO KUWA TAASISI IMARA?

Waswahili wanakwambia “Kila mbuzi atakula kwa urefu wa kamba yake” lakini katika uwanda wa kiuchumi na biashara duniani, kila mtu anao uwezo wa kubadilika na kufanya uchaguzi ulio bora zaidi kwa maisha yake ya kiuchumi na kijamii. Na hii ni kwa kujifunza na kufanya kazi tu.

E = EMPLOYEE (MWAJIRIWA): Kitu cha kwanza ambacho kipo kichwani kwa mwajiriwa yeyote ni uhakika wa kibarua chake (job security). Mwajiriwa hufanya kazi kwa bidii ili apate mkate wa kila siku na zaidi awe na hakika kuwa ataendelea kupokea mshahara kila mwisho wa mwezi kwa miaka mpaka atakapostaafu au kumaliza mkataba wake. Dhana ya kuwa majiriwa huathiri ubunifu wa mtu katika kutaka kujaribu shughuli nyingine itakayoimarisha uchumi wake zaidi ya ajira.

Mwajiriwa anapohitaji kukua kiuchumi hutafuta ajira itayomlipa zaidi na si fursa za biashara mpya.

udalali wa mtandaoni ongea na watu uvae viatu

Biashara yako inaweza vipi kuwa taasisi imara

S= SELF-EMPLOYED (KUJIAJIRI): Hii ni njia ya mateso makubwa, japokuwa vijana wengi eti ndio hupenda kufanya shughuli za kujiajiri wakihisi kuwa huko kuna uhuru mkubwa na pesa nyingi. #VijanaWenzangu acheni kujidanganya. Unapojiajiri fahamu kuwa utajinyima uhuru wako binafsi ili biashara yako iweze kuwa hai. Wewe ndio unakua CEO, sales manager, mhasibu wewe, mtu wa masoko wewe, yaani wewe ndio unakuwa kila kitu. Hata hivyo kwa biashara inayoanza si vibaya kupitia katika hatua hii japo hutakiwi kukaa muda mrefu hapa, lazima biashara ivuke hiki kiunzi.

B=BUSINESS OWNER (MMILIKI WA BIASHARA): Tofauti na walio katika Chumba “S” Mtu anayemiliki biashara sio lazima awe anafanya kazi katika biashara hio. Yeye anamiliki mfumo wa utendaji au bidhaa ambayo ndio huzalisha pesa muda wote hata asipokuwepo. Mfano, mtu anayemiliki kiwanda cha kutengeneza nguo. Sio lazima awe ndio mtendaji mkuu wa kutengeneza nguo, hata hivyo yeye anaweza kuajiri watu wa kiwandani na kuwalipa ili waendelee kuzalisha bidhaa zitazoendelea kuingiza pesa.

I=INVESTOR (MUWEKEZAJI): Huyu ndiye mtu mwenye uelewa mkubwa zaidi kati ya wote ambao tumewajadili hapo juu. Mtu huyu hutafuta Mali (Assets) zaidi kuliko madeni (Liabilities). Mara nyingine hutumia pesa za watu wengine (mkopo) ili kuhakikisha anapata Mali itakayozalisha (asset). Ukitaka kufahamu kwa undani kuhusu Uwiano unaofaa wa Mali na Madeni katika biashara gusa link hii Uwiano wa Mali (assets) na Madeni (Liabilities) kwenye biashara.

Mtu huyu hutumia faida anayopata kutoka kwenye assets zake kununua assets nyingine nyingi zaidi, na hujikuta akifurahia maisha ya kuingiza kipato kutoka kwenye assets kuliko vyanzo vya matumizi (liabilities). Kama ulikua hufahamu basi Matajiri unaowajua duniani wote ni Wawekezaji huku wakitumia kanuni ya 70% kwa 30% katika shughuli zote za kifedha. Kiufupi kanuni hio hutumika katika kupanga matumizi ya mapato ambayo hugawanywa katika mafungu matatu ya:

i. 70% Matumizi ya kawaida (Normal Expenses including taxes, rents, food, accomodations etc)

ii. 30% (20% Servings + 10% Charity) Mwekezaji anapohitaji pesa hutafuta assets zaidi kuliko kufanya matumizi yanayofyonza pesa za biashara.

Sasa basi, hayo yote niliyoyaeleza, hayatakuwa na maana kama hayatafanyika katika muundo wa Taasisi Imara.

BIASHARA KAMA TAASISI IMARA INA SIFA ZIPI?

Taasisi Imara ni ile jumuiya ya kiuchumi/Kijamii ambayo inaendeshwa kwa mujibu wa katiba katika utendaji wake wa kila siku. Jumuiya hio inaweza kuwa ni Serikali, Shirika, Kampuni, Chama, Biashara au Familia. Familia (Ndoa) ndio Taasisi ya kwanza kabisa kuwahi kuanzishwa na binadamu duniani. Ndio maana wahenga wanakwambia “Maendeleo yanaanzia nyumbani.

Maendeleo ya taasisi hutegemea uwepo wa sheria zitakazokuwa muongozo wa kila kinachofanyika kila siku ndani ya taasisi hio. Hata hivyo ili iwe taasisi imara inapaswa kuwa na sifa hizi:

1. SHERIA MBELE, MTU NYUMA: Taasisi imara hutambua na kutekeleza matakwa ya kisheria na kamwe si matakwa ya mtu binafsi. Sheria hizi huandikwa katika mfumo wa Katiba (constitution/memorandum/articles of assosciation, Taratibu (regulations) na sheria ndogondogo (by-laws). Taasisi zinazoongozwa vema kwa mujibu wa sheria bila kumuogopa mtu huwa imara sana kiutendaji na hufikia malengo yake kiurahisi zaidi.

2. UTAMADUNI: Katika utendaji bora, Utamaduni huzingatiwa kama silaha bora zaidi katika uzalishaji/utoaji huduma wenye viwango vya juu vinavyitakiwa. Wahenga walishasema “Culture eats strategy for breakfast” yani, hakuna mbinu ambayo itaweza kufanya kazi kwa mafanikio isipofanywa kama sehemu ya utamaduni. Hivyo Taasisi imara hufanya shughuli zake katika Utamaduni uliotengenezwa kwa muda mrefu katika kufikia malengo yaliyowekwa. Mfano, utamaduni wa kupongeza mtendaji bora, utamaduni wa kumhudumia mteja kwa njia ya mtandao na utamaduni wa kuzingatia viwango.

3. UWAJIBIKAJI: Ili iwe Taasisi imara lazima watendaji wawajibike katika majukumu ya kila siku. Watendaji wanapaswa kuwajibika kwa Kupongezwa, Kujiuzulu au Kuongeza kiwango cha uzalishaji/utoaji huduma kwa wateja wao. Taasisi imara haipaswi kufumbia macho swala la uwajibikaji.

Biashara yako inaweza vipi kuwa taasisi imara

4. KWELI NA HAKIKA: Hakuna Taaasisi Imara ambayo haijiendeshi katika namna ya Ukweli na Uhakika kwa wateja wake. Hata hivyo, hakuna mifumo ya Taasisi inayofanya kazi kwa ubora wa 100%, ni vema kuhakikisha jambo hili linazingatiwa.

Tulizoziona leo ni baadhi ya sifa zinazotengeneza Taasisi Imara. Kwa mujibu wa malengo Endelevu ya kimataifa ya UN, imepangwa kutimiza lengo la kuwa na Taasisi Imara ifikapo mwaka 2030 (#Agenda2030). Tujadili kupitia Replies, Retweets na Share ili watu wengi zaidi wanufaike.

Tuungane kwa pamoja kuhakikisha Biashara yako inaweza vipi kuwa taasisi imara. Endelea kupata makala muhimu kuhusu Biashara, Uchumi na Teknolojia kupitia links hizi hapa:

  1. WEBSITE INASAIDIA VIPI KUIMARISHA BIASHARA YAKO?
  2. KWANINI UITANGAZE BIASHARA YAKO?
  3. UMUHIMU WA TAKWIMU KATIKA UTOAJI WA HUDUMA BORA KWA WATEJA
  4. TEKNOLOJIA KATIKA KUKUZA BIASHARA KUPITIA SEKTA YA UTALII

UFAHAMU MFUMO WA KODI NA MAPATO YA SERIKALI ZA MITAA

Serikali za mitaa zikiwa ndani ya Halmashauri za miji/Majiji na Wilaya zina mamlaka ya kukusanya mapato na ushuru kutoka vyanzo mbalimbali vya kodi. Pia zina mamlaka ya kutumia mapato hayo kwa mujibu wa sheria.

Kulingana na mipaka ya kisheria inayowekwa na Serikali Kuu, hizi Serikali za mitaa zina uwezo wa kutengeneza sera zake za mapato ili kuleta maendeleo katika shughuli zinazogusa kwa ukaribu maendeleo jamii nzima kama mashule, hospitali, mazingira ya mitaa na ulinzi shirikishi.

Mapato haya yanayokusanywa yanapata Mamlaka kutoka katika Sheria ya Mapato ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1983 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Sasa leo ukimaliza kusoma makala haya, utakuwa umezijua kodi/tozo zote zinazokusanywa pamoja na matumizi yake kwa ujumla.

Idadi ya kodi na ushuru unaokusanywa chini ya Mamlaka ya serikali za mitaa hutofautiana kutoka Halmashauri moja na Halmashauri nyingine. Mambo yanayoleta utofauti huu ni maendeleo katika sekta za Biashara, makazi, Uwepo wa maliasili na shughuli za kiuchumi.

Kuna baadhi ya tozo hukusanywa kwa siku, zingine mlipakodi hutozwa kwa mwaka, na zingine humpa nafasi mlipakodi kuchagua wakati wa kulipa (kwa mwezi, wiki, miezi mitatu/sita au kwa mwaka). Mfano; ushuru wa masoko, huu kawaida hukusanywa kwa siku. Hata hivyo Halmashauri zingine hutoa nafasi kwa mlipakodi kulipia ushuru huu kwa mwezi, miezi 3/6 au kwa mwaka mzima. Mwisho wa mwaka wa fedha kila Halmashauri inatakiwa kuandaa akaunti za kifedha ikiwa na wadau wafuatao:

i. Halmashauri Nzima

ii. Muwakilishi wa wizara (TAMISEMI)

iii. Ofisi ya Waziri Mkuu

iv. Ofisi ya Mdibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG)

v. Umma

Serikali za Mitaa hupata mapato yake kutoka katika vyanzo vikuu vitatu :

1. Mapato yake yenyewe

2. Ruzuku kutoka Serikali Kuu

3. Misaada kutoka mifuko ya Maendeleo ya ndani na nje ya nchi.

MAPATO/KODI ZINAZOTOZWA NI ZIPI?

1. USHURU WA BIDHAA (PRODUCE CESS)

Ushuru huu hutozwa na halmashauri kutoka katika mauzo ya mazao kama mahindi, mchele, kahawa, chai, pamba korosho pamoja na mifugo. Ushuru huu hutozwa kutokana na uzito/ujazo wa bidhaa yenyewe. Hii hufanya thamani ya bidhaa kutokua thabiti ikitegemea uzito/ujazo wa bidhaa (the source to be inelastic unless adjustments become frequent enough to catch up with inflation), hapa watu wa uchumi mtakuwa mmenipata vizuri sana. Viwango vya ushuru huu hubadilika kutegemeana na Halmashauri kutokana na Jiografia ya eneo, misimu ya hali ya hewa pamoja na hadhi ya kiuchumi ya Halmashauri husika.

2. LESENI ZA BIASHARA

Kodi hizi hutozwa kutokana na ukubwa na aina ya biashara, yaani maduka mawili ya rejareja yatatozwa kodi ya leseni sawasawa bila kujali ukubwa wa mitaji yao au hesabu zao wanazowasilisha kwenye mamlaka za mapato (turnovers).

3. ADA YA MASOKO

Aina hii ya Ushuru kwa kawaida hutozwa kwa siku kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao katika maeneo ya sokoni. Viwango vya tozo hii hubadilika kulingana na bidhaa zainazouzwa.

4. KODI YA ARDHI/MAJENGO

Kisheria, Serikali kuu inatakiwa kukusanya kodi kutoka kwenye mali zote zinazohamishika, wakati Serkali za Mitaa zitakusanya kodi katika mali zote zisizohamishika. Hata Hivyo, kodi ya ardhi na majengo haijaweza kutumika ipasavyo katika mambo ya kisiasa na uongozi katika nchi zinazoendelea. Katika kitabu chake kuhusu kodi ya ardhi, Richard Bird (1974:223) anasema, “The administrative constraint on effective land on effective land tax administration is so severe in most developing countries today that virtually all the more refined fiscal devises beloved by theorists can and should be discarded for this reason alone. Not only will they not be well administered, they will in all likelihood be so poorly administered as to produce neither equity, efficiency, nor revenue.” Nadhani hoja yake imeeleweka.

5. USHURU WA HOTELI/NYUMBA ZA WAGENI

Kodi hii kisheria hutegemea na tathmini binafsi kuhusu hesabu za hoteli/nyumba za wageni. Viwango vikubwa vya kodi huhamasisha ukwepaji wa kodi hasa kwa kurekodi hesabu mara mbilimbili. Katika utekelezaji, hasa kwa biashara ndogo ambazo hazitoi risiti, turnover zao hukadiriwa tu na hivyo kupunguza mapato kwenye serikali za mitaa. Hata hivyo, biashara kubwa ambazo pia hazitoi risiti huwekewa utaratibu wa kufanya maridhiano kati ya wakusanya kodi na walipa kodi. Utaratibu huu unaongeza gharama za uendeshaji na kuongeza mianya ya rushwa. Hata hivyo, kutokana na makusanyo haya kuzingatia asilimia za mapato ya biashara, makusanyo yanategemewa kubadilika kadhalika.

6. KODI YA MABANGO/MATANGAZO

Hii kodi wafanyabiashara wengi huilalamikia, wengine wasijui kwanini wanatozwa wakiweka tu mabango katika biashara zao. Viwango vya kodi hii hutegemea ukubwa wa bango, kama linawaka taa usiku na muda bango hilo litakavyokuwa wazi. Mapato ya mabango yanaendelea kukua kutokana na kuongezeka kwa biashara ambazo pia zinahitaji matangazo kujiimarisha.

7. USHURU WA MCHANGA

Unashangaa? Hadi mchanga wa kujengea unalipiwa kodi ndio katika baadhi ya halmashauri. Gharama ndogo za mchanga pamoja na kuongezeka kwa kasi ya watu kujenga kumechochea mmomonyoko wa udongo kwenye machimbo jambo lilifanya serikali kupiga marufuku Uchimbaji holela wa mchanga na kuanzisha utaratibu mpya wa kuchimba mchanga katika maeneo maalum na hivyo kudhibiti mapato yatokanayo na mchanga.

8. USHURU WA MACHINJIO/MAEGESHO

Halmashauri nyingi ambazo zina machinjio ya wanyama na maengesho ya magari hutoza kodi hio vizuri. Mapato yatokanayo na kodi hii yamekuwa yakiongezeka hasa maeneo ya mijini ambapo kumekuwa na uhitaji mkubwa wa maegesho ya magari na pikipiki pamoja na kuongezeka kwa wanyama wanaonmchinjwa katika maeneo maalum. Hii ni kwa kuwa serikali imefanikiwa kudhibiti machinjio zote za mitaani na kulazimisha wanyama wote kuchinjwa maeneo maalum ya machinjio ambayo yana udhibiti wa kiserikali na kuzingatia viwango vya nyama kwa manufaa ya walaji. Wale wanaopajua vingunguti watakuwa wamenipata sawasawa hapa.

9. KODI ZINGINE

Serikali za Mitaa hukusanya kodi nyingine nyingi sana. Unaweza kuzipata kwa ufupi katika tovuti rasmi ya Wizara ya Fedha kupitia link hii https://mof.go.tz/mofdocs/revenue/revlocal.htm…

Serikali za mitaa hazitozi kodi ambazo zipo nje ya zilizopo kwenye listi iliyo kwenye link hio.

Vile vile unaweza kupata maelezo kuhusu Kodi na wajibu wake katika matumizi ya mwaka 2018/2019 kupitia link hii hapa chini

https://rednet.co.tz/download/taxes-and-duties-at-a-glance-2018-2019…

HIZO KODI ZINATUMIKA VIPI?

Kodi zinazokusanywa na Halmashauri za Wilaya/Miji/Majiji hutumi kodi hizo kuimarisha mambo yafuatayo:

i. Ulinzi shirikishi

ii. Barabara za mitaani pamoja na miundombinu yake

iii. Zimamoto na uokoaji

iv. kuimarisha shughuli za kiuchumi (masoko, biashara) nk

Mfumo wa kodi wa serikali za mitaa kwa muda mrefu umekuwa tata sana na usio na uwazi katika makusanyo ya mapato yake mpaka matumizi. Lakini tangu kuzinduliwa kwa mfumo maalum wa makusanyo ya kodi kwa njia ya kielektroniki wa Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS) mnamo mwaka 2014, mfumo huo umekuwa mkombozi katika kurekodi makusanyo sahihi na kudhibiti matumizi katika Halmashauri. Mfumo huo wa kisasa umekuwa bora zaidi katika kukusanya Mapato ambapo unatoa urahisi wa kutumia njia mbalimbali za kulipia kodi kama MPESA, TIGOPESA, AIRTEL MONEY, Njia ya Benki na kadhalika.

Kuna makala hizi hapa chini tumekuwekea kwenye links. Zitakusaidia kufahamu zaidi kuhusu mifumo ya kodi na mapato hasa nchini Tanzania. Gusa link kisha makinika:

  1. https://rednet.co.tz/ufahamu-mfumo-wa-kodi-nchini-tanzania/ yenye kichwa “UFAHAMU MFUMO WA KODI NCHINI TANZANIA”
  2. https://rednet.co.tz/lipa-kodi-kwa-faida-ya-biashara-yako/ yenye kichwa “LIPA KODI KWA FAIDA YA BIASHARA YAKO”
  3. https://rednet.co.tz/unaweza-vipi-kukabiliana-na-hasara-katika-biashara-yako-mwaka-huu-2021/ yenye kichwa “UNAWEZA VIPI KUKABILIANA NA HASARA KATIKA BIASHARA YAKO MWAKA HUU 2021”

UNAFAHAMU NINI KUHUSU BIASHARA ZA KIELEKTRONIKI (e-commerce BUSINESSES)?

Japokuwa imechelewa, lakini kwa sasa Africa ndio inaongoza mbio katika kufanya mapinduzi ya kidijitali kuliko sehemu yoyote duniani. Namna ya kufanya biashara inazidi kubadilika ikionyesha nia ya dhati kufanya maendeleo ya kiuchumi, miundombinu na maswala ya kijamii. Mwaka 2018 nchi wanachama wa Umoja wa Africa walipiga hatua kubwa katika mfumo wa kufanya biashara na muingiliano wa kiuchumi baada ya kuanzisha Eneo Huru la Kufanyia Biashara barani (Continental Free Trade Area AfCFTA). Eneo hili lililoanzishwa linashirikisha nchi 22 zilizoweka sahihi tayari na utekelezwaji wake ulipangwa kuanza mwaka 2019 (tayari umeshaanza).

Hata hivyo mazungumzo bado yanaendelea kuweza kuzishirikisha nchi ambazo bado si wanachama wa eneo hili jipya, inatarajiwa eneo hili kufikia soko la watu takribani bilioni 1.2 barani wakiwa na jumla ya pato la ndani la taifa (GDP) la dola za kimarekani trilioni 2.5 kwa pamoja, kwa mwaka. Hii inatarajiwa kuwa ni mapinduzi makubwa zaidi kuwahi kutokea kwenye nyanja ya uchumi wa Afrika.

Sasa, swali linakuja; Afrika(wafanyabiashara, makampuni/mashirika na Serikali) imejiandaa vipi na mapinduzi haya ya uchumi wa kidijitali? Na zaidi, watunga sera/sheria wataangalia vipi biashara za kielektroniki (e-commerce) kama mada muhimu katika eneo hilo jipya la kufanya biashara huru barani?

Tume ya kudhibiti uchumi wa Africa ya Umoja wa Mataifa (ECA) ikishirikiana na Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) pamoja na Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo ya kibiashara (UNCTAD) mwaka huu 2019 imechapisha ripoti yake ikiangazia maendeleo ya Afrika kiujumla katika nyanja za kiuchumi, siasa na kijamii.

URAHISI: Imeonekana kwamba e-commerce inaweza kufanya biashara ya bidhaa na huduma kwa urahisi zaidi ambapo itarahisisha mwenendo mzuri wa biashara kati ya wazalishaji, wafanyabiashra na walaji pamoja na kumbukumbu zao na miamala ya kifedha.

MITANDAO YA KIJAMII: Pia imeonekana kwamba e-commerce inapatikana na kufanyika kirahisi katika mitandao ya kijamii kama facebook na Instagram ambapo ndipo mahali kuna watumiaji wengi zaidi wa Intaneti duniani (zaidi ya watu bilioni 2 kati ya watumiaji bilioni 4 wa intaneti).

KUTOKUWA NA MIPAKA: Mfumo wa uchumi wa Kidijitali kiasili umetengenezwa kuepuka mipaka ya kijiografia katika kufanya biashara na kubadilishana fedha ambapo mabadiliko haya ya kiteknolojia yataongeza umakini zaidi katika mwenendo wa masoko na gharama. Lakini bado wimbi kubwa la watu watakaoshiriki kwenye soko barani wanaonekana wataachwa nyuma kutokana na kutokuingiliana kwa lugha na vita/ghasia za mara kwa mara katika baadhi ya jamii/nchi.

BIASHARA: Kwa mujibu wa UNCTAD mwaka 2016 kwa dunia nzima e-commerce iliweza kupitisha mauzoya takribani dola trilioni 26 ambapo 90% ilikuwa ni Biashara kwa Biashara (B2B e-commerce) na 10% ilikuwa ni Biashara kwa Mlaji (B2C e-commerce). Hata hivyo kupima mwenendo wa e-commerce katika baadhi ya nchi zinazoendelea imekuwa ni changamoto kupata data na takwimu, haswa katika nchi za Afrika.

IMPORTATION: Takwimu za Shirika la Fedha Duniani (IMF) zinaonyesha kwamba Biashara kati ya nchi na nchi imekua kwa kiasi kikubwa Afrika ambapo zimechagizwa na vituo vichache vya kiteknolojia (Hubs) ambavyo vimerahisisha mno mwenendo wa biashara. Biashara kati y nchi na nchi (Intraregional import) imekuwa zaidi ya mara 3 katika miongo miwili iliyopita kufikia 12%- 14% sawa na dola bilioni 100 ikichagizwa na uwepo wa jumuiya za kiuchumi barani (Subregional Economic Communities REC‘s).

UZOEFU: Hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na umri wa Jumuiya hizi za Kimaendeleo barani Afrika ambapo uzoefu huo hutumika kuongeza jitihada katika kuboresha namna ya ufanyaji biashara kuelekea uchumi wa kidijitali kiteknolojia. Uzoefu huo pia hutumika kuunganisha jumuiya moja na nyingine (mf, SADC na COMESAna EAC) ambapo zitazalishwa nafasi nyingi zaidi za kufanya biashara kati ya nchi wanachama na ripoti zinaonyesha 75% ya biashara hizi ndani ya jumuiya barani Afrika zimefanyika mwaka 2017 peke yake na nusu ya biashara hizo zilifanyika katika jumuiya ya SADC.

Chini ya mwavuli wa AfCFTA nchi wanachama zinatarajia kufuta tozo/ushuru kwa 90% ya bidhaa zote zitakazopitishwa na kufanyiwa biashara katika eneo hilo. Hii itaruhusu uwezekano wa kupunguza mlolongo wa kodi au kuongeza idadi na thamani ya bidhaa na huduma zitakazohusishwa. Matokeo yoyote katika punguzo hilo linalotarajiwa katika muktadha wa biashara kidijitali yataleta picha tofauti. Kupunguza mlolongo wa tozo za mipakani baina ya nchi na nchi kutapungua kwa 15% pekee ikitegemea thamani ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi husika. Hii ni kwa mujibu wa Tume inayoshughulikia Uchumi wa Afrika kutoka Umoja wa Mataifa (UNECA) mwaka 2018.

Sasa mwaka 2018 Jumuiya ya COMESA ilibuni mfumo wa kudhibiti eneo huru la kibiashara kidijitali (Digital Free Trade Area DFTA). Mfumo huu umeundwa na mambo yafuatayo;

•E-trade: Hili ni jukwaa mahsusi kwa ajili ya kufanya biashara za kimtandao na kuwezesha malipo ya kielektroniki, mobile apps kwa ajili ya wafanyabiashara walioko katika Jumuiya hio.

•E-logistics: hili ni jukwaa maalum kwa ajili ya kuwezesha biashara ya usafirishaji wa mizigo baina ya nchi wanachama wa jumuiya.

•E-legislation: huu ni mfumo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara rasmi ambao unawawezesha kufanya miamala na malipo kielektoniki.

Mfumo huu uliobuniwa na Jumuiya ya COMESA umelenga kutangaza biashara za wanajumuiya katika nchi wanachama ikijumuisha kupitia majukwaa ya e-commerce. Mfumo huu ulikuwa ni mfanano wa mfumo uliotengenezwa na kuzinduliw na nchi ya Malaysia mwaka 2017 katika muktadha wa kufanya biashara huru ndani ya eneo maalum.

Makala haya ya leo yamelenga wafanyabiasha kujidhatiti kidijitali kwa kutumia teknolojia za kisasa katika biashara zao za kila siku ili kuweza kunufaika vyema na masoko pamoja na fursa kede ndani na nje ya nchi.

Makala hizi hapa zinarandana na somo ulilolipata leo. Zitakusaidia sana, shuka nazo:

  1. https://rednet.co.tz/fahamu-kuhusu-biashara-ya-fedha-za-kidijitali-cryptocurrency-business/ yenye kichwa “FAHAMU KUHUSU BIASHARA YA FEDHA ZA KIDIJITALI (CRYPTOCURRENCY BUSINESS)”
  2. https://rednet.co.tz/teknolojia-ya-huduma-za-fedha-kwa-njia-ya-kielektroniki-fintech/ yenye kichwa “TEKNOLOJIA YA HUDUMA ZA FEDHA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI (FINTECH)”
  3. https://rednet.co.tz/fahamu-siri-ya-kufanikiwa-katika-kuwekeza/ yenye kichwa “FAHAMU SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA”

Ukiwa na lolole, tafadhali unaweza kuwasiliana nasi kupitia;

e-mail: info@rednet.co.tz

tovuti: https://rednet.co.tz

Simu:+255765834754