Tag: Uchumi wa Afrika

mageuzi ya Intaneti (iot) katika biashara na maisha. Jihudumie leo kutoka Rednet Technologies.

IFAHAMU AINA MPYA YA UDALALI WA MTANDAONI (DROPSHIPPING)

Dunia inakwenda kasi sana na Teknolojia inazidi kusambaa na kuteka sekta za kiuchumi. Mwandishi mmoja alinukuliwa akisema “In this modern world, prepare to change your career.” Umeshafikiria kuwa Dalali smart? Leo sasa ifahamu aina mpya ya udalali wa mtandaoni (Dropshipping) kwa undani. Ni nini na inafanya kazi vipi? Makinika mpaka mwisho wa makala hii..

Kwa Afrika yenye watumiaji wa huduma za internet wanaokadiriwa kuzidi milioni 400, tafiti zinaonyesha fursa za kuongezeka kwa biashara za mtandaoni (e-commerce) sasa ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote. Shirika la Statista linakadiria sekta ya e-commerce kufikia thamani ya US 29$ milioni kufikia mwaka 2022.

DROPSHIPPING NI NINI?

Hii ni aina ya Udalali wa kimtandao ambapo Mtu wa kati (Dalali) huchukua Oda kutoka kwa Mteja kisha huituma Oda hio kwa Mwenye Mali (Muuzaji) ambaye hukamilisha mauzo kwa Mteja na kumwachia Dalali Kamisheni yake stahili.

Lakini wakati mwingine hasa barani Afrika huyu Mtu wa Kati huchukua Oda kutoka kwa mteja kisha huenda kwa Mwenye mali na kuchukua Bidhaa na kisha kwenda kuiuza yeye moja kwa moja kwa Mteja. Hii ndio kitu inafanyika sana Afrika kama ulikua hujui.

Hata hivyo msingi Mkuu wa Dropshipping ni kuwa namna hii ya Biashara hufanywa na Mtu wa kati ambaye hana stock kabisa (haihitaji uwe na mtaji wa fedha au bidhaa ili kufanya dropshipping). Kwa hiyo Dropshipping ndiyo kinara katika aina za biashara za mtandaoni (e-commerce).

Hii Dropshipping ni biashara moja ambayo mtu yeyote hasa kijana anaweza kabisa kuifanya kwa kuwa haihitaji uwe na mtaji wa kifedha ama bidhaa (stock). Hata hivyo, kama zilivyo biashara zingine, sio biashara rahisi wala sio biashara ambayo inaweza kukutajirisha mara moja.

Unahitajika kuwa mbunifu, mwenye juhudi na mvumilivu ili uweze kufanikiwa kwenye aina hii ya biashara kwa kuwa:

1. KIWANGO CHA FAIDA NI KIDOGO: Kiwango cha faida hutegemea kamisheni au “cha juu” ambacho mara nyingi hakiwi kiwango kikubwa. Hivyo ili uweze kupata Faida kubwa inakubidi pia uhakikishe bidhaa/huduma nyingi zimemfikia mteja kupitia wewe.

KUMBUKA: Kila mauzo unayoyafanya hapa, kiwango kikubwa cha pesa humwendea Mwenye Mali, kile “Cha juu” ndio hubaki kuwa halali yako.

udalali wa mtandaoniongea na watu uvae viatu

ZINGATIA: Waswahili wanasema, “Ongea na watu uvae viatu” Ukitafsiri vizuri hii nafasi ya kufanikiwa ni kubwa kwa sababu kadiri unavyokuwa na watu wengi zaidi katika mtandao wako basi nafasi yako ya kutengeneza faida inazidi kuwa kubwa.

2. USHINDANI NI MKUBWA: Hii ni aina ya bishara ambayo ushindani wake ni mkubwa kweli kweli. Fikiria haihitaji mtaji wa Kifedha wala bidhaa(stock) ili kuanza kuifanya, watu wangapi wanaweza kuifanya? wangapi tayari wanaifanya sasa hivi? Hivyo ili ufanikiwe, lazima ukomae kweli.

3. UHALALI/UBORA WA BIDHAA: Mara nyingi hii sio kesi kubwa lakini huwa inatokea. Ni mara ngapi imetokea mteja ameona bidhaa fulani kupitia ukurasa wako(mtu kati) wa mtandaoni, halafu vile umeenda kwa Mwenye Mali ukakuta ile bidhaa iliyoonekana kwenye picha mtandaoni sio ile halisi uliyoikuta kwa Mwenye Mali. Hili jambo ni baya na linaumiza sana watu wa kati na wakati mwingine hushusha heshima na uaminifu ambao wameutengeneza kwa wateja wao kwa muda mrefu sana.

Wakati mwingine hutokea hata mwenye mali si halali kisheria au/na wewe (dalali) hufahamu hata bidhaa unazozichukua ili kupeleka kwa mteja zinatoka wapi. Swala la bidhaa feki linaathiri sana kipengele hiki ambapo hutokea bidhaa iliyoonekana mtandaoni kuwa na logo fulani inayoaminika, lakini ile iliyo kwa ground inakuwa logo ya kughushi/feki. Hivyo lazima uwe mwangalifu.

4. UGUMU WA KUTENGENEZA BRAND: Ukiwa mfanyabiashara wa aina ya Dropshipping, fahamu kuwa sifa ya ubora wa bidhaa mara zote itakwenda kwa Mwenye Mali tu. Kitachokufanya uendelee kubaki kwenye game ni namna yako nzuri ya kuhudumia wateja wako wote bila ubaguzi na kwa ubora wa juu.

Kutengeneza Brand ni muhimu sana. Brand haijengwi kwa siku moja hata hivyo, ni mchakato wa muda mrefu. Sasa kuelewa zaidi kuhusu Brand (ni nini na inafanyika vipi) gusa link hii hapa Branding vs Marketing, kipi ni kipi?

Kumbuka: sio Logo yako iliyo kwenye bidhaa. Hivyo tengeneza SUMAKU yako kwa kutumia aina ya maneno yanayoweza kuuza bidhaa (copywriting), matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii pamoja na website bora na ambayo imeunganishwa na huduma za S.E.O.

Hizo ni baadhi ya Changamoto ambazo unategemea kukutana nazo katika aina hii ya biashara mtandaoni. Hata hivyo, kuna namna ambayo unatakiwa ujipange ili kuhakikisha Biashara yako inakuwa na mafanikio zaidi na uwezo wa kupambana na changamoto.

Kipi cha kufanya ili ufanikiwe katika Udalali huu wa Mtandaoni (Dropshipping)?:

1. CHAGUA HADHIRA YAKO: Haya ni mazingira na aina ya watu ambao unajihusanisha nao kila siku mtandaoni. Fahamu kuwa aina ya watu unaojihusanisha nao ni muhimu katika kutengeneza Aina ya soko linalofaa kwa bidhaa zako. Pia aina ya watu inaweza kukuambia ni aina gani ya bidhaa itawafaa kulingana na changamoto unaziziona zikiwatatiza kutoka kwao. Hapa lazima uwe na jicho zuri la kuona kile watu wengi hasa wafanyabiashara wenzako hawakioni. Kuwa Mchunguzi kidogo, hala hala usije kuwa mbea tu. Kwa vyovyote unapokua dalali hasa wa mtandaoni lazima ujitangaze, Kwanini ujitangaze sasa fuatana na makala hii hapa kufahamu zaidi..

2. TAFUTA MFANYABIASHARA (MWENYE MALI) WA KUAMINIKA: Hiki ni kipengele muhimu katika kuhakikisha bidhaa zako zinaweza kupatikana kwa wakati bila longolongo wala ujanjaujanja. Mteja mara nyingi hununua kwa uhitaji ambao husukumwa na hisia. Hivyo hisia hizo zinaposhindwa kufikiwa ndani ya muda fulani, basi mteja anaweza kugairi au kununua kwa mtu mwingine.

Hapa ukiwa kama mfanyabiashara lazima ujue namna ya kutengeneza hali ya dharura kwa mteja ili anunue bidhaa yako kwa upesi, lakini zaidi lazima utimize haja ya mteja wako ndani ya muda na kwa uhakika.

3. CHAGUA BIDHAA YA KUUZA: Kabla hujaanza kufanya aina hii ya biashara lazima ujue hizo bidhaa zinazohusika “utamuuzia nani?”. Katika kuchagua unatakiwa uangalie Umri, Elimu, Makundi ya kijamii (wanafunzi, wasomi wa vyuo, wafanyakazi, wazazi, watu wa dini nk). Hivyo lazima ujue ni bidhaa zipi zinawafaa wateja na hadhira yako Kiujumla.

Njia nzuri ya kuchagua bidhaa zinazouzika sana ni kupitia majukwaa kama YouTube kupitia matafuto kama “top 10 products to sell” utajifunza mengi humo.

•Pia unaweza kutumia Majukwaa ya Amazon na AlliExpress kupata bidhaa zinazofaa kufanyia biashara unayotaka kuifanya.

•Chunguza matangazo (sponsored ads) kupitia mitandao kama facebook, instagram na twitter. Kwenye kuchagua aina ya bidhaa jitahidi kuepuka:

•Bidhaa za chakula ambazo zinahitaji uthibitisho wa mamlaka, huna muda wa kupeleka bidhaa ikathibitishwe TMDA/TBS kabla haijamfikia mteja.

•Bidhaa ambazo ni silaha. Hizi mara nyingi soko lake ni la shaka kwa wateja wengi, hivyo kizifanya kutokuwa reliable.

•Mambo ya Fashion: Najua hii ndio watu wengi wanapenda kufanya, lakini jitafakari kuhusu ushindani wake sokoni, Nadhani unawajua wanaouza nguo na viatu katika mitandao ya kijamii.

4. WEKA BIDHAA ZAKO MTANDAONI: Baada yakufanya yote hapo juu, hakikisha bidhaa zako zinaonekana mtandaoni. Njia nzuri zaidi ya kuweka bidhaa mtandaoni ni kupitia Website na Instagram kwa sababu bidhaa inatakiwa kuonekana kwa picha ili kumvutia mteja. Mitandao mingi ya kijamii haikupi nafasi nzuri ya kuonyesha bidhaa zako kwa wateja katika unadhifu unaotakiwa. Hata hivyo ni muhimu pia kutumia mitandao mingine ya kijamii katika kunadi bidhaa zako mara kwa mara kupitia ujuzi wa “Copywriting” vizuri.

Sasa nimekuwekea makala kupitia links hizi hapa chini ili kuhakikisha somo la leo unalielewa vizuri. Zitakusaidia sana ukizimaliza zote.

  1. UKIRITIMBA KATIKA BIASHARA, NI ASALI AU SHUBIRI?
  2. KWANINI NI MUHIMU KUWA NA WEBSITE RASMI YA BIASHARA YAKO?
  3. IJUE NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO

Nadhani leo ume ifahamu aina mpya ya udalali wa mtandaoni (Dropshipping) katika kiwango chake. Unalo lolote la kushare nasi? Tafadhali tujadili kupitia comment hapo chini.

Je umependezwa na makala yetu hii ya leo?

Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?

Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.

Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.

Ifahamu aina mpya ya udalali wa mtandaoni.

UFAHAMU MFUMO WA KODI NA MAPATO YA SERIKALI ZA MITAA

Serikali za mitaa zikiwa ndani ya Halmashauri za miji/Majiji na Wilaya zina mamlaka ya kukusanya mapato na ushuru kutoka vyanzo mbalimbali vya kodi. Pia zina mamlaka ya kutumia mapato hayo kwa mujibu wa sheria.

Kulingana na mipaka ya kisheria inayowekwa na Serikali Kuu, hizi Serikali za mitaa zina uwezo wa kutengeneza sera zake za mapato ili kuleta maendeleo katika shughuli zinazogusa kwa ukaribu maendeleo jamii nzima kama mashule, hospitali, mazingira ya mitaa na ulinzi shirikishi.

Mapato haya yanayokusanywa yanapata Mamlaka kutoka katika Sheria ya Mapato ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1983 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Sasa leo ukimaliza kusoma makala haya, utakuwa umezijua kodi/tozo zote zinazokusanywa pamoja na matumizi yake kwa ujumla.

Idadi ya kodi na ushuru unaokusanywa chini ya Mamlaka ya serikali za mitaa hutofautiana kutoka Halmashauri moja na Halmashauri nyingine. Mambo yanayoleta utofauti huu ni maendeleo katika sekta za Biashara, makazi, Uwepo wa maliasili na shughuli za kiuchumi.

Kuna baadhi ya tozo hukusanywa kwa siku, zingine mlipakodi hutozwa kwa mwaka, na zingine humpa nafasi mlipakodi kuchagua wakati wa kulipa (kwa mwezi, wiki, miezi mitatu/sita au kwa mwaka). Mfano; ushuru wa masoko, huu kawaida hukusanywa kwa siku. Hata hivyo Halmashauri zingine hutoa nafasi kwa mlipakodi kulipia ushuru huu kwa mwezi, miezi 3/6 au kwa mwaka mzima. Mwisho wa mwaka wa fedha kila Halmashauri inatakiwa kuandaa akaunti za kifedha ikiwa na wadau wafuatao:

i. Halmashauri Nzima

ii. Muwakilishi wa wizara (TAMISEMI)

iii. Ofisi ya Waziri Mkuu

iv. Ofisi ya Mdibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG)

v. Umma

Serikali za Mitaa hupata mapato yake kutoka katika vyanzo vikuu vitatu :

1. Mapato yake yenyewe

2. Ruzuku kutoka Serikali Kuu

3. Misaada kutoka mifuko ya Maendeleo ya ndani na nje ya nchi.

MAPATO/KODI ZINAZOTOZWA NI ZIPI?

1. USHURU WA BIDHAA (PRODUCE CESS)

Ushuru huu hutozwa na halmashauri kutoka katika mauzo ya mazao kama mahindi, mchele, kahawa, chai, pamba korosho pamoja na mifugo. Ushuru huu hutozwa kutokana na uzito/ujazo wa bidhaa yenyewe. Hii hufanya thamani ya bidhaa kutokua thabiti ikitegemea uzito/ujazo wa bidhaa (the source to be inelastic unless adjustments become frequent enough to catch up with inflation), hapa watu wa uchumi mtakuwa mmenipata vizuri sana. Viwango vya ushuru huu hubadilika kutegemeana na Halmashauri kutokana na Jiografia ya eneo, misimu ya hali ya hewa pamoja na hadhi ya kiuchumi ya Halmashauri husika.

2. LESENI ZA BIASHARA

Kodi hizi hutozwa kutokana na ukubwa na aina ya biashara, yaani maduka mawili ya rejareja yatatozwa kodi ya leseni sawasawa bila kujali ukubwa wa mitaji yao au hesabu zao wanazowasilisha kwenye mamlaka za mapato (turnovers).

3. ADA YA MASOKO

Aina hii ya Ushuru kwa kawaida hutozwa kwa siku kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao katika maeneo ya sokoni. Viwango vya tozo hii hubadilika kulingana na bidhaa zainazouzwa.

4. KODI YA ARDHI/MAJENGO

Kisheria, Serikali kuu inatakiwa kukusanya kodi kutoka kwenye mali zote zinazohamishika, wakati Serkali za Mitaa zitakusanya kodi katika mali zote zisizohamishika. Hata Hivyo, kodi ya ardhi na majengo haijaweza kutumika ipasavyo katika mambo ya kisiasa na uongozi katika nchi zinazoendelea. Katika kitabu chake kuhusu kodi ya ardhi, Richard Bird (1974:223) anasema, “The administrative constraint on effective land on effective land tax administration is so severe in most developing countries today that virtually all the more refined fiscal devises beloved by theorists can and should be discarded for this reason alone. Not only will they not be well administered, they will in all likelihood be so poorly administered as to produce neither equity, efficiency, nor revenue.” Nadhani hoja yake imeeleweka.

5. USHURU WA HOTELI/NYUMBA ZA WAGENI

Kodi hii kisheria hutegemea na tathmini binafsi kuhusu hesabu za hoteli/nyumba za wageni. Viwango vikubwa vya kodi huhamasisha ukwepaji wa kodi hasa kwa kurekodi hesabu mara mbilimbili. Katika utekelezaji, hasa kwa biashara ndogo ambazo hazitoi risiti, turnover zao hukadiriwa tu na hivyo kupunguza mapato kwenye serikali za mitaa. Hata hivyo, biashara kubwa ambazo pia hazitoi risiti huwekewa utaratibu wa kufanya maridhiano kati ya wakusanya kodi na walipa kodi. Utaratibu huu unaongeza gharama za uendeshaji na kuongeza mianya ya rushwa. Hata hivyo, kutokana na makusanyo haya kuzingatia asilimia za mapato ya biashara, makusanyo yanategemewa kubadilika kadhalika.

6. KODI YA MABANGO/MATANGAZO

Hii kodi wafanyabiashara wengi huilalamikia, wengine wasijui kwanini wanatozwa wakiweka tu mabango katika biashara zao. Viwango vya kodi hii hutegemea ukubwa wa bango, kama linawaka taa usiku na muda bango hilo litakavyokuwa wazi. Mapato ya mabango yanaendelea kukua kutokana na kuongezeka kwa biashara ambazo pia zinahitaji matangazo kujiimarisha.

7. USHURU WA MCHANGA

Unashangaa? Hadi mchanga wa kujengea unalipiwa kodi ndio katika baadhi ya halmashauri. Gharama ndogo za mchanga pamoja na kuongezeka kwa kasi ya watu kujenga kumechochea mmomonyoko wa udongo kwenye machimbo jambo lilifanya serikali kupiga marufuku Uchimbaji holela wa mchanga na kuanzisha utaratibu mpya wa kuchimba mchanga katika maeneo maalum na hivyo kudhibiti mapato yatokanayo na mchanga.

8. USHURU WA MACHINJIO/MAEGESHO

Halmashauri nyingi ambazo zina machinjio ya wanyama na maengesho ya magari hutoza kodi hio vizuri. Mapato yatokanayo na kodi hii yamekuwa yakiongezeka hasa maeneo ya mijini ambapo kumekuwa na uhitaji mkubwa wa maegesho ya magari na pikipiki pamoja na kuongezeka kwa wanyama wanaonmchinjwa katika maeneo maalum. Hii ni kwa kuwa serikali imefanikiwa kudhibiti machinjio zote za mitaani na kulazimisha wanyama wote kuchinjwa maeneo maalum ya machinjio ambayo yana udhibiti wa kiserikali na kuzingatia viwango vya nyama kwa manufaa ya walaji. Wale wanaopajua vingunguti watakuwa wamenipata sawasawa hapa.

9. KODI ZINGINE

Serikali za Mitaa hukusanya kodi nyingine nyingi sana. Unaweza kuzipata kwa ufupi katika tovuti rasmi ya Wizara ya Fedha kupitia link hii https://mof.go.tz/mofdocs/revenue/revlocal.htm…

Serikali za mitaa hazitozi kodi ambazo zipo nje ya zilizopo kwenye listi iliyo kwenye link hio.

Vile vile unaweza kupata maelezo kuhusu Kodi na wajibu wake katika matumizi ya mwaka 2018/2019 kupitia link hii hapa chini

https://rednet.co.tz/download/taxes-and-duties-at-a-glance-2018-2019…

HIZO KODI ZINATUMIKA VIPI?

Kodi zinazokusanywa na Halmashauri za Wilaya/Miji/Majiji hutumi kodi hizo kuimarisha mambo yafuatayo:

i. Ulinzi shirikishi

ii. Barabara za mitaani pamoja na miundombinu yake

iii. Zimamoto na uokoaji

iv. kuimarisha shughuli za kiuchumi (masoko, biashara) nk

Mfumo wa kodi wa serikali za mitaa kwa muda mrefu umekuwa tata sana na usio na uwazi katika makusanyo ya mapato yake mpaka matumizi. Lakini tangu kuzinduliwa kwa mfumo maalum wa makusanyo ya kodi kwa njia ya kielektroniki wa Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS) mnamo mwaka 2014, mfumo huo umekuwa mkombozi katika kurekodi makusanyo sahihi na kudhibiti matumizi katika Halmashauri. Mfumo huo wa kisasa umekuwa bora zaidi katika kukusanya Mapato ambapo unatoa urahisi wa kutumia njia mbalimbali za kulipia kodi kama MPESA, TIGOPESA, AIRTEL MONEY, Njia ya Benki na kadhalika.

Kuna makala hizi hapa chini tumekuwekea kwenye links. Zitakusaidia kufahamu zaidi kuhusu mifumo ya kodi na mapato hasa nchini Tanzania. Gusa link kisha makinika:

  1. https://rednet.co.tz/ufahamu-mfumo-wa-kodi-nchini-tanzania/ yenye kichwa “UFAHAMU MFUMO WA KODI NCHINI TANZANIA”
  2. https://rednet.co.tz/lipa-kodi-kwa-faida-ya-biashara-yako/ yenye kichwa “LIPA KODI KWA FAIDA YA BIASHARA YAKO”
  3. https://rednet.co.tz/unaweza-vipi-kukabiliana-na-hasara-katika-biashara-yako-mwaka-huu-2021/ yenye kichwa “UNAWEZA VIPI KUKABILIANA NA HASARA KATIKA BIASHARA YAKO MWAKA HUU 2021”

FAHAMU MCHANGO WA ICT KATIKA MAENDELEO YA SEKTA BINAFSI BARANI AFRICA

Kwa mara ya kwanza katika Historia ya mwanadamu, zaidi ya nusu ya watu wote duniani wanatumia huduma za internet. Na katika maeneo yote, imeonekana huduma hizo zinakua kwa kasi zaidi barani Africa. Idadi ya watu wanaotumia internet imeongezeka sana barani Afrika kutoka 2.1% mwaka 2005 mpaka 24.4% mwaka 2018. Sasa leo nataka u fahamu mchango wa ICT katika maendeleo ya sekta binafsi barani Africa. Twende sambamba.

Huduma hizi za internet zimekuja kurahisisha shughuli za kiuchumi kama kurahisisha njia za malipo (bank, MPESA, tigopesa nk), matumizi ya drones katika matibabu kama inavyofanyika nchini Rwanda, matumizi ya smartphones katika kuongeza maarifa ya kitaaluma na kiufundi stadi na kuongezeka kwa biashara za mtandaoni (e-commerce businesses, network marketing and online businesses). Bill Gates amewahi kuandika katika moja ya tweets zake “If your business is not on the Internet yet, Your are out of the Business.” Mwenye macho haambiwi ona.

SEKTA BINAFSI, INJINI YA UCHUMI AFRIKA

Kama ulikua hufahamu, basi sekta binafsi ndio imetawala Uchumi wa Afrika kwa kuwa zaidi ya 80% ya uzalishaji mali mzima hufanyika katika sekta hio. Zaidi, theluthi mbili (⅔) ya uwekezaji mzima barani na robo tatu (¾) ya jumla ya mitaji katika uchumi kati ya mwaka 1996-2008 imeonekana kutokea katika sekta hio binafsi. Vile vile sekta hio inatoa 90% ya ajira zote kwa vijana walio katika umri wa kufanya kazi. Mchango wa biashara za ndani katika sekta binafsi katika GDP ilikua 59% katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ukilinganisha na 30% ya nchi za Latin America na Caribbean, 32% Asia Kusini na 42% katika Mashariki ya Kati. Hii inaonyesha kiasi gani Afrika sekta binafsi inalipa maradufu. Umeiona nafasi yako hapa ndugu yangu mfanyabiashara.!?

Kujiimarisha katika Sekta binafsi, huna budi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kila mara unapohitajika kufanya hivyo. Unawezaje kufanya maamuzi sahihi katika changamoto zinazokukabili? Tafadhali fuatana nasi katika makala hii hapa FANYA MAAMUZI SAHIHI KATIKA MUDA SAHIHI.

Katika nchi za Uchumi wa kati, kampuni binafsi hufanya kazi katika mfumo wa sekta rasmi, ambapo makampuni makubwa na yale madogo (SME’s) huzalisha hisa za thamani katika uwekezaji na zaidi, ajira kwa vijana ambao ndio kundi kubwa zaidi katika nguvu kazi barani Afrika. Lakini zaidi, sekta binafsi katika nchi hizi hufanya ⅔ ya uzalishaji mzima.

Uchumi huwa na ushindani pale kunapokuwa na ushindani mkali wa kibiashara. Na biashara huwa na ushindani pale:

•Sheria zinapokua sawa na haki.

•Wafanyakazi wana maarifa stahiki.

•Gharama za uendeshaji (umeme, maji, mafuta, usafiri) zinakuwa nafuu.

•Wateja wanafikika kila kona.

ICT INAINGIA VIPI HAPO?

Uchumi wa kidijitali umekuwa dhima kuu ya kidunia na Afrika haijabaki nyuma katika hili. Matumizi ya teknolojia yanazidi kushika kasi barani yakichagizwa na kasi ya ueneaji wa huduma za internet ambapo biashara nyingi zinazidi kuhamia mtandaoni kirahisi. Mpaka kufikia mwaka 2015 tu tayari watu 557 barani walikua wanatumia simu ya mkononi ambayo ni 12% ya watumiaji wote wa simu duniani huku idadi hio ikikusanya 6% ya mapato yote yaliyofanyika duniani wakati huo.

Sasa leo wacha tuone maeneo muhimu ya ICT yanayokuza uchumi zaidi;

1. TELECOMUNICATIONS

Eneo hili linajumuisha makampuni makubwa ya mawasiliano. Kwa kiasi kikubwa hufanya shughuli zake katika utaratibu wa sekta rasmi, hivyo kuwafikia watu wengi na kufanya kazi karibu zaidi na mamlaka za serikali. Makampuni kama Vocacom, MTN, Tigo, Airtel na TTCL yapo hapa. Kutokana na kuwa na watumiaji wengi, makampuni haya huchangia kiasi kikubwa katika mapato ya kiserikali kama kodi na gawio huku yakichangia sehemu kubwa katika kukuza uchumi wa watumiaji wake kutokana na fursa zinazopatikana katika huduma wanazozitoa kama uwakala wa huduma, huduma za kifedha nakadhalika.

2. SOFTWARE AND IT CONSULTING

Hapa ndo utatukuta sisi sasa ambao tunakuhudumia wewe muda huu. Zaidi ya kukupatia taarifa hizi ghafi, pia eneo hili la ICT hutoa huduma za kutengeneza mifumo ya computer, Apps za simu, Ushauri na Uchambuzi wa kiteknolojia katika Biashara na Uchumi. Japokuwa sio maarufu sana lakini sehemu hii inachangia uchumi wa mabiashara mbalimbali, makapuni madogo na yale yanayokuwa (SME’s) pamoja na sekta zingine za uma na binafsi kwa kutoa huduma za matengenezo ya tovuti, mifumo mbalimbali ya kibiashara, huduma za afya, elimu, uhifadhi wa data pamoja na uchambuzi na ushauri wa biashara mbalimbali kiteknolojia zaidi.

3. DIGITAL SERVICES

Hapa utawakuta watu wanaotoa huduma za kidijitali ambao wengi wao hufanya kazi kwa ukaribu na makampuni ya mawasiliano. Watoa huduma hawa pia wanahusika kutengeneza mifumo ya makampuni ya mawasiliano pamoja na kutengeneza/kuendesha mitandao ya kijamii zaidi. Watoa huduma hawa wamekuwa wakitengeneza michezo ya video pamoja na kutoa huduma za WebHosting na Cloud services kwa makampuni ya Kiafrika. Kampuni kama Dudumizi Technologies(Tanzania), ISB North Africa (Morocco), Web4Africa (Ghana) na Domains Africa Technologies (Kenya) zipo hapa.

4. INFORMATION SERVICES

Hapa sasa ndio utazikuta redio na televisheni zote unazozifahamu. Hawa kwa jina lingine wanaitwa Watoaji wa Maudhui, ambapo hutafuta habari na maudhui wanayodhani yanafaa kwa wateja wao na hivyo kukusanya jamii ili ipate maudhui hayo huku yenyewe yakijipatia faida yake katika matangazo mbalimbali ya kibiashara yanayoruka sambamba na maudhui yao. Hapa unaweza kunitajia Redio/TV ambayo ina maudhui unayoyapenda yakienda sambamba na matangazo ya wadhamini wa vipindi vyao. Usishangae ukiona hivyo. Kwenye matangazo ndo wanapopatia pesa wenzio, usione unapata bure maudhui hayo.

Kwa uchache haya ndio mambo ya fahamu mchango wa ICT katika maendeleo ya sekta binafsi barani Africa yanayochangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa Uchumi wa Kidijitali na kuboresha biashara nyingi zaidi kila kukicha barani Afrika. Jiulize, unayatumia vipi maeneo haya katika kukuza biashara yako wewe kama mjasiriamali?

Makala hizi hapa chini zitakusaidia kufahamu kwa undani namna sekta binafsi zinachangia uchumi na maendeleo ya wafanyabiashara hasa vijana wa Afrika Mashariki. Gusa links kisha makinika:

  1. KWANINI NI MUHIMU KUWA NA WEBSITE (TOVUTI) RASMI YA BIASHARA YAKO?
  2. UKIRITIMBA KATIKA BIASHARA, NI ASALI AU SHUBIRI?
  3. UNAFAHAMU NINI KUHUSU URASINISHAJI (HARMONIZATION) KATIKA BIASHARA

Usisahau kutoa maoni yako kuhusu ukichojifunza katika makala hii ya leo na unaweza kusambaza ili kuhakikisha ulichijifunza kinawafikia wengine. Pia unaweza kutembelea tovuti yetu maridhawa ya https://rednet.co.tz kuhakikisha unaendelea kupata taarifa sahihi kuhusu uchumi na biashara yako kiteknolojia. Asante.

Makala hii ni Kwa Heshima ya Hayati B.W. Mkapa aliyekuwa Rais awamu ya 3 nchini Tanzania. Mzee Mkapa aliongoza Taifa kuelekea zama hizi za maendeleo ya Sekta Binafsi kupitia Sera yake ya Ubinafsishaji wa mali za umma zilizokua mzigo kwa serikali, hivyo kuchochea ukuaji wa sekta binafsi kwa kiasi kikubwa mpaka kufikia hivi ilivyo leo. Mzee aliona mbali sana. #RIPMkapa