Tag: tracking system

UFAHAMU MFUMO WA KODI NA MAPATO YA SERIKALI ZA MITAA

Serikali za mitaa zikiwa ndani ya Halmashauri za miji/Majiji na Wilaya zina mamlaka ya kukusanya mapato na ushuru kutoka vyanzo mbalimbali vya kodi. Pia zina mamlaka ya kutumia mapato hayo kwa mujibu wa sheria.

Kulingana na mipaka ya kisheria inayowekwa na Serikali Kuu, hizi Serikali za mitaa zina uwezo wa kutengeneza sera zake za mapato ili kuleta maendeleo katika shughuli zinazogusa kwa ukaribu maendeleo jamii nzima kama mashule, hospitali, mazingira ya mitaa na ulinzi shirikishi.

Mapato haya yanayokusanywa yanapata Mamlaka kutoka katika Sheria ya Mapato ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1983 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Sasa leo ukimaliza kusoma makala haya, utakuwa umezijua kodi/tozo zote zinazokusanywa pamoja na matumizi yake kwa ujumla.

Idadi ya kodi na ushuru unaokusanywa chini ya Mamlaka ya serikali za mitaa hutofautiana kutoka Halmashauri moja na Halmashauri nyingine. Mambo yanayoleta utofauti huu ni maendeleo katika sekta za Biashara, makazi, Uwepo wa maliasili na shughuli za kiuchumi.

Kuna baadhi ya tozo hukusanywa kwa siku, zingine mlipakodi hutozwa kwa mwaka, na zingine humpa nafasi mlipakodi kuchagua wakati wa kulipa (kwa mwezi, wiki, miezi mitatu/sita au kwa mwaka). Mfano; ushuru wa masoko, huu kawaida hukusanywa kwa siku. Hata hivyo Halmashauri zingine hutoa nafasi kwa mlipakodi kulipia ushuru huu kwa mwezi, miezi 3/6 au kwa mwaka mzima. Mwisho wa mwaka wa fedha kila Halmashauri inatakiwa kuandaa akaunti za kifedha ikiwa na wadau wafuatao:

i. Halmashauri Nzima

ii. Muwakilishi wa wizara (TAMISEMI)

iii. Ofisi ya Waziri Mkuu

iv. Ofisi ya Mdibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG)

v. Umma

Serikali za Mitaa hupata mapato yake kutoka katika vyanzo vikuu vitatu :

1. Mapato yake yenyewe

2. Ruzuku kutoka Serikali Kuu

3. Misaada kutoka mifuko ya Maendeleo ya ndani na nje ya nchi.

MAPATO/KODI ZINAZOTOZWA NI ZIPI?

1. USHURU WA BIDHAA (PRODUCE CESS)

Ushuru huu hutozwa na halmashauri kutoka katika mauzo ya mazao kama mahindi, mchele, kahawa, chai, pamba korosho pamoja na mifugo. Ushuru huu hutozwa kutokana na uzito/ujazo wa bidhaa yenyewe. Hii hufanya thamani ya bidhaa kutokua thabiti ikitegemea uzito/ujazo wa bidhaa (the source to be inelastic unless adjustments become frequent enough to catch up with inflation), hapa watu wa uchumi mtakuwa mmenipata vizuri sana. Viwango vya ushuru huu hubadilika kutegemeana na Halmashauri kutokana na Jiografia ya eneo, misimu ya hali ya hewa pamoja na hadhi ya kiuchumi ya Halmashauri husika.

2. LESENI ZA BIASHARA

Kodi hizi hutozwa kutokana na ukubwa na aina ya biashara, yaani maduka mawili ya rejareja yatatozwa kodi ya leseni sawasawa bila kujali ukubwa wa mitaji yao au hesabu zao wanazowasilisha kwenye mamlaka za mapato (turnovers).

3. ADA YA MASOKO

Aina hii ya Ushuru kwa kawaida hutozwa kwa siku kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao katika maeneo ya sokoni. Viwango vya tozo hii hubadilika kulingana na bidhaa zainazouzwa.

4. KODI YA ARDHI/MAJENGO

Kisheria, Serikali kuu inatakiwa kukusanya kodi kutoka kwenye mali zote zinazohamishika, wakati Serkali za Mitaa zitakusanya kodi katika mali zote zisizohamishika. Hata Hivyo, kodi ya ardhi na majengo haijaweza kutumika ipasavyo katika mambo ya kisiasa na uongozi katika nchi zinazoendelea. Katika kitabu chake kuhusu kodi ya ardhi, Richard Bird (1974:223) anasema, “The administrative constraint on effective land on effective land tax administration is so severe in most developing countries today that virtually all the more refined fiscal devises beloved by theorists can and should be discarded for this reason alone. Not only will they not be well administered, they will in all likelihood be so poorly administered as to produce neither equity, efficiency, nor revenue.” Nadhani hoja yake imeeleweka.

5. USHURU WA HOTELI/NYUMBA ZA WAGENI

Kodi hii kisheria hutegemea na tathmini binafsi kuhusu hesabu za hoteli/nyumba za wageni. Viwango vikubwa vya kodi huhamasisha ukwepaji wa kodi hasa kwa kurekodi hesabu mara mbilimbili. Katika utekelezaji, hasa kwa biashara ndogo ambazo hazitoi risiti, turnover zao hukadiriwa tu na hivyo kupunguza mapato kwenye serikali za mitaa. Hata hivyo, biashara kubwa ambazo pia hazitoi risiti huwekewa utaratibu wa kufanya maridhiano kati ya wakusanya kodi na walipa kodi. Utaratibu huu unaongeza gharama za uendeshaji na kuongeza mianya ya rushwa. Hata hivyo, kutokana na makusanyo haya kuzingatia asilimia za mapato ya biashara, makusanyo yanategemewa kubadilika kadhalika.

6. KODI YA MABANGO/MATANGAZO

Hii kodi wafanyabiashara wengi huilalamikia, wengine wasijui kwanini wanatozwa wakiweka tu mabango katika biashara zao. Viwango vya kodi hii hutegemea ukubwa wa bango, kama linawaka taa usiku na muda bango hilo litakavyokuwa wazi. Mapato ya mabango yanaendelea kukua kutokana na kuongezeka kwa biashara ambazo pia zinahitaji matangazo kujiimarisha.

7. USHURU WA MCHANGA

Unashangaa? Hadi mchanga wa kujengea unalipiwa kodi ndio katika baadhi ya halmashauri. Gharama ndogo za mchanga pamoja na kuongezeka kwa kasi ya watu kujenga kumechochea mmomonyoko wa udongo kwenye machimbo jambo lilifanya serikali kupiga marufuku Uchimbaji holela wa mchanga na kuanzisha utaratibu mpya wa kuchimba mchanga katika maeneo maalum na hivyo kudhibiti mapato yatokanayo na mchanga.

8. USHURU WA MACHINJIO/MAEGESHO

Halmashauri nyingi ambazo zina machinjio ya wanyama na maengesho ya magari hutoza kodi hio vizuri. Mapato yatokanayo na kodi hii yamekuwa yakiongezeka hasa maeneo ya mijini ambapo kumekuwa na uhitaji mkubwa wa maegesho ya magari na pikipiki pamoja na kuongezeka kwa wanyama wanaonmchinjwa katika maeneo maalum. Hii ni kwa kuwa serikali imefanikiwa kudhibiti machinjio zote za mitaani na kulazimisha wanyama wote kuchinjwa maeneo maalum ya machinjio ambayo yana udhibiti wa kiserikali na kuzingatia viwango vya nyama kwa manufaa ya walaji. Wale wanaopajua vingunguti watakuwa wamenipata sawasawa hapa.

9. KODI ZINGINE

Serikali za Mitaa hukusanya kodi nyingine nyingi sana. Unaweza kuzipata kwa ufupi katika tovuti rasmi ya Wizara ya Fedha kupitia link hii https://mof.go.tz/mofdocs/revenue/revlocal.htm…

Serikali za mitaa hazitozi kodi ambazo zipo nje ya zilizopo kwenye listi iliyo kwenye link hio.

Vile vile unaweza kupata maelezo kuhusu Kodi na wajibu wake katika matumizi ya mwaka 2018/2019 kupitia link hii hapa chini

https://rednet.co.tz/download/taxes-and-duties-at-a-glance-2018-2019…

HIZO KODI ZINATUMIKA VIPI?

Kodi zinazokusanywa na Halmashauri za Wilaya/Miji/Majiji hutumi kodi hizo kuimarisha mambo yafuatayo:

i. Ulinzi shirikishi

ii. Barabara za mitaani pamoja na miundombinu yake

iii. Zimamoto na uokoaji

iv. kuimarisha shughuli za kiuchumi (masoko, biashara) nk

Mfumo wa kodi wa serikali za mitaa kwa muda mrefu umekuwa tata sana na usio na uwazi katika makusanyo ya mapato yake mpaka matumizi. Lakini tangu kuzinduliwa kwa mfumo maalum wa makusanyo ya kodi kwa njia ya kielektroniki wa Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS) mnamo mwaka 2014, mfumo huo umekuwa mkombozi katika kurekodi makusanyo sahihi na kudhibiti matumizi katika Halmashauri. Mfumo huo wa kisasa umekuwa bora zaidi katika kukusanya Mapato ambapo unatoa urahisi wa kutumia njia mbalimbali za kulipia kodi kama MPESA, TIGOPESA, AIRTEL MONEY, Njia ya Benki na kadhalika.

Kuna makala hizi hapa chini tumekuwekea kwenye links. Zitakusaidia kufahamu zaidi kuhusu mifumo ya kodi na mapato hasa nchini Tanzania. Gusa link kisha makinika:

  1. https://rednet.co.tz/ufahamu-mfumo-wa-kodi-nchini-tanzania/ yenye kichwa “UFAHAMU MFUMO WA KODI NCHINI TANZANIA”
  2. https://rednet.co.tz/lipa-kodi-kwa-faida-ya-biashara-yako/ yenye kichwa “LIPA KODI KWA FAIDA YA BIASHARA YAKO”
  3. https://rednet.co.tz/unaweza-vipi-kukabiliana-na-hasara-katika-biashara-yako-mwaka-huu-2021/ yenye kichwa “UNAWEZA VIPI KUKABILIANA NA HASARA KATIKA BIASHARA YAKO MWAKA HUU 2021”
mapinduzi ya kiteknolojia katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi

MAPINDUZI YA KITEKNOLOJIA KATIKA SEKTA YA USAFIRISHAJI NA UCHUKUZI

Ubunifu wa kiteknolojia na zama za Kidijitali huathiri karibu kila mchakato katika utendaji na uendeshaji wa mfumo wa Usafirishaji na Uchukuzi duniani kote. Kuanzia njia na namna ya usafirishaji wa majini/baharini, ardhini na angani, usimamiaji wa mizigo pamoja na shughuli za utawala na ugavi zikiwemo utaratibu/usimamizi wa nyaraka na ufuatiliaji mzuri wa malipo. Leo sasa tuangazie mapinduzi ya kiteknolojia katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi. Kuna nini kinaendelea huko? Makinika..

Idadi wa watu duniani itaongezeka kutoka watu bilioni 7.4 mpaka watu bilioni 10.6 kufikia mwaka 2050, vile vile idadi ya mizigo inayosafirishwa kwa njia ya meli peke yake itaongezeka mpaka mara 4 ambayo inatarajiwa kukua kwa ongezeko la 715% kwa nchi za Africa.

Pia kasi ya ukuaji wa miji itakuwa kwa 56% ya idadi ya watu katika Africa mpaka mwaka huo 2050. Ongezeko hili linatarajiwa kuchagizwa na kasi ya ukuaji wa miji, kukua kwa kipato cha mtu mmoja mmoja, kupenya kwa matumizi ya intaneti pamoja na urahisi wa kupata na kutumia Teknolojia mpya.

Hata hivyo mtindo wa uchukuzi wa mizigo kwa kupitia njia ya meli kwa kutegemea nyaraka peke yake unatarajiwa kupungua kwa kiasi kikubwa kufuatia ujio wa matumizi ya nyaraka za kielektroniki na barua pepe. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la EY.

Kufuatia kasi hio ya ukuaji na mabadiliko, makampuni na biashara zilizopo katika sekta ya Usafiri na Uchukuzi yanahitaji kubadilika ili kumudu kuwepo katika ulimwengu ambao ushindani unakuja kutoka pande zote na teknolojia za kidijitali ndio zitakuwa chachu kuu ya mabadiliko.

Sasa Swali; Teknolojia Inaweza vipi kubadili Kesho ya Sekta hii ya Usafirishaji na Uchukuzi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara?

Leo hii sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi na kijamii hufanyika mtandaoni na haswa haraka zaidi kupitia katika simu janja (smartphones). Ukuaji huu wa kiteknolojia unanufaisha maeneo yote yaliyomo kwenye Sekta hii ya Usafirishaji na Uchukuzi kama; usafiri wa magari ya mizigo (malori), usafiri wa kimataifa (njia ya anga na majini), usimamiaji wa shughuli za ugavi na kuratibu safari za majini, nchi kavu na angani. Yafuatayo ni mapinduzi ya kiteknolojia katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi barani Afrika;

1. MFUMO WA KURATIBU SAFARI/ONLINE TRACKING SYSTEM (Magari ya mizigo, Meli na Anga): Imezoeleka mteja kuhifadhiwa nafasi ya kusafirisha mizigo yake kwa kujaza fomu fulani ya usafirishaji, halafu anaachwa gizani mpaka siku mzigo wake unamfikia asipoamua kufuatilia kwa kupiga simu. Lakini leo, kwa kutumia huduma za intaneti na programu za kompyuta mteja anao uwezo wa kuagiza na kufuatilia kwa ukaribu zaidi mizigo yake muda wowote akihitaji kufanya hivyo.

Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.Mapinduzi ya kiteknolojia katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi

Hii si tu kwamba imerahisisha matumizi ya intaneti kisasa zaidi lakini zaidi teknolojia hii inaokoa muda na gharama za ziada kwa kampuni ya usafirishaji na mtu binafsi.

2. TEKNOLOJIA YA INTERNET OF THINGS (IoT) na RADIO FREQUENCY IDENTIFICATION (RFID): Ulishawahi kufikiria siku fulani una uwezo wa kuwasha feni yako nyumbani kwa kutumia simujanja yako? Sasa leo hii vifaa vingi vya kielektroniki vimeundwa na uwezo wa Wi-Fi na vifaa vya kuhisi mazingira mbalimbali. IoT inafungua nafasi nyingi sana katika kurahisisha shughuli za ugavi kama kupunguza gharama za uendeshaji. Vifaa vya kuhisi mazingira (sensors) pia hufungwa katika magari madogo na makubwa, meli za mizigo, treni na kadhalika. Vifaa hivi hufungwa mfumo wa kengele au mfumo wa GPS ambayo hufuatilia na kuratibu mwenendo wa mzigo kumfikia mteja.

Hali kadhalika teknolojia ya RFID ambayo imeshatumika miaka kadhaa hutumiwa na makampuni ya uchukuzi na usafirishaji kufuatilia mwenendo wa hesabu za bidhaa zao (Inventories). Kwenye teknolojia hii hujumuisha pia matumizi ya barcode za kwenye bidhaa, pamoja na matumizi ya rimoti za televisheni na redio, teknolojia ambayo imetumika kwa miaka mingi zaidi, hivyo kuyafanya makampuni mengi kutumia zaidi RFID’s. Vile vile RFID’s hutumika kusambaza bidhaa katika maghala yao na kuratibu mienendo ya makontena.

3.MAGARI/ MALORI YA KUJIENDESHA NA DRONES: Katika ulimwengu ambao unaendeshwa na matumizi ya kompyuta kutoka mahali fulani kwenda mahali kwingine, utajihisi vipi siku unapokea mzigo kutoka kwenye chombo kinachoruka angali mfano wa helikopta ndogo? Sasa huko ndipo tunapoelekea. Magari ya kujiendesha tayari yanaonekana duniani ambapo kampuni za UBER na EMBARK wametengeneza magari yanayojiendesha japokuwa bado miradi hiyo haijarasimishwa kwa wateja. Ni swala la muda tu kutoka sasa kabla matumizi yake hayajawafikia wateja ulimwenguni kote.

4. MITANDAO YA KIJAMII: Nani ambaye hapitii kwenye mitandao ya kijamii angalau mara moja kwa siku? Nguvu ya mitandao hii ya kijamii inaboresha kwa namna ya kipekee sana sekta hii ya Usafirishaji na Uchukuzi kwa ujumla wake. Mitandao hii inarahisisha sana katika kutangaza huduma za usafirishaji na uchukuzi pamoja na kampuni kuwasiliana na wateja wake kwa ukaribu na urahisi zaidi katika kutoa taarifa muhimu, dharura na mrejesho kutoka kwa wateja.

Kwa mujibu wa Hootsuite, 59% ya Wamarekani ambao ni watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekubali kwamba huduma kwa wateja kupitia mitandao ya kijamii imerahisisha kujibu maswali na huduma husika.

Zaidi ya yote, miundombinu ya uchukuzi katika nchi za Afrika bado ipo nyuma sana kimaendeleo ukilinganisha na sehemu zingine za dunia. Nchi ya Afrika Kusini ndiyo inaongoza barani kwa kuwa na miundombinu ya kisasa zaidi ya kiuchukuzi ambapo kasi ya ukuaji wa miundombinu kwa mwaka ni ndogo kwa 3% katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2017. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Fedha duniani (IMF).

Kwa upande mwingine nchi za Kenya na Nigeria zinaongoza kwa kuwa na ukuaji mkubwa katika miundombinu yake ya kiuchukuzi na usafirishaji kwa 6.2% na 6.8% katika kipindi hicho hicho (2012-2017). Kwa wafanyabiashara na makampuni ya usafirishaji na uchukuzi; Kuwekeza vema Afrika kunahitaji uelewa mzuri wa maeneo muhimu pamoja na uelewa wa masoko ya wenyeji.

Afrika si tu kwamba ni kubwa mno, lakini zaidi Kuna mtawanyiko mkubwa wa jamii za watu na rasilimali. Hata hivyo, zaidi ya 70% ya makampuni makubwa zaidi duniani yanayozalisha bidhaa za watumiaji tayari zinafanya kazi Afrika. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kimataifa la PwC.

Usipitwe na Ofa Yetu katika msimu huu wa Nane Nane. Makala haya ya leo yamelenga wafanyabiasha kujidhatiti kidijitali kwa kutumia teknolojia za kisasa katika biashara zao za kila siku ili kuweza kunufaika vyema na masoko pamoja na fursa kede ndani na nje ya nchi. Umejifunza nini leo kuhusu mapinduzi ya kiteknolojia katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi? Share nasi mawazo yako kwenye comment au tucheki kwa kugusa WhatsApp namba yetu hii hapa 0765834754.

Makala hizi hapa zitakupa mwanga zaidi katika kuwekeza katika Biashara zinahohusiana na sekta ya Usafiri na Chukuzi hasa katika eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara:

  1. FAHAMU SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA
  2. USAFIRISHAJI NA MIUNDOMBINU KATIKA USTAWI WA BIASHARA AFRIKA
  3. FAHAMU KUHUSU TEKNOLOJIA KATIKA SEKTA YA HABARI NA BURUDANI