Tag: Teknojia

IJUE TEKNOLOJIA NA UMUHIMU WAKE KATIKA SERA YA KULINDA TAARIFA ZA MTEJA

Tarehe 12, August 2019 Benki Kuu ya Tanzania ilitoa rai kwa makampuni yanayotoa huduma za kifedha kwa njia ya kimtandao kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kulinda taarifa za wateja wao kuhusu maswala ya kifedha kwa kutumia teknolojia. Akitoa changamoto hio katika hafla ya kufungua mkutano wa 19 wa Mafunzo ya Kibenki kwa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha, Kaimu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Dr. Benard Kibese amesema ” uaminifu wa mteja ndio thamani halisi kwa mtoa huduma wa masuala ya kifedha. Kama hivyo ni kweli, teknolojia peke yake inaweza vipi kulinda uaminifu huu? Kama ni kweli itaweza vipi? Kama hapana, wabobevu wa huduma za kifedha wanatakiwa kufanya nini ili kujenga uaminifu huu? Haya ni baadhi ya maswali mnatakiwa kujiuliza.” alisema Dr. Kibese. Hii ni kwa mujibu wa gazeti za The Citizen.

Sasa swali, huu utaratibu wa kulinda taarifa za mteja (Consumer Protection regulation) ni nini, na unamchango gani katika kukuza uchumi na biashara?

Kufuatia mtikisiko wa kiuchumi duniani mnamo mwaka 2008, wito wa uanzishwaji wa sheria ya kulinda taarifa za mteja kuhusu masoko ya kifedha umezidi kukuwa mkubwa na kupata ushawishi. Watunga sera na sheria duniani wamekuwa wakipewa changamoto za kutafsiri sheria hizo katika namna rahisi na za kiutaratibu ili kuruhusu utoaji huduma za kifedha. Hata hivyo sheria hizi ziko tofauti katika nchi mbalimbali kulingana na viwango vya maendeleo ya kiuchumi, malengo ya ushirikishwaji wa maswala ya kifedha, uwezo wa mamlaka kusimamia na kudhibiti pamoja na uelewa wa wateja.

Sasa mwaka 2009 katika mkutano wa MFW4A (Making Finance Work for Africa) uliofanyika Accra, Ghana, mambo mbalimbali yalijadiliwa katika kutaka kuazishwa kwa utaratibu wa kulinda taarifa za kifedha za wateja walioko katika nchi zinazoendelea. Majadiliano hayo yalilenga maeneo matatu ya kushughulikia katika kufikia lengo. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyoandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya nchini Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Wizara ya Maendeleo na Ushirikiano wa Kiuchumi nchini Ujerumani.

Mambo hayo matatu ni yapi? Baki nasi hapahapa..

1. UWAZI:

Udhaifu wa mawasiliano na uwazi katika kuhifadhi na kufanyia kazi taarifa za wateja umeonekana kukithiri katika masoko ya nchi zinazoendelea jambo linalohitaji mabadiliko chanya ya haraka. Katika masoko ya fedha, taarifa ndio msingi wa shughuli zote nyeti. Hivyo kutokuwa na msawaziko na ulinzi bora wa taarifa katika mamlaka za uendeshaji kwa kutumia teknolojia za kisasa na mifumo ya ulinzi wa kimtandao (network/internet security mechanisms) hudhoofisha masoko haya ya kifedha. Vile vile ufahamu mdogo wa elimu kuhusu maswala ya kifedha kwa watu wengi katika masoko ya nchi zinazoendelea huwapa faida za taarifa watoaji wa huduma za kifedha. Yaani uwazi wa taarifa hutoa maelekezo na mwangaza kwa taratibu zenye lengo la kupangilia bei za bidhaa/huduma, makubaliano na tahadhari kwa wateja na mamlaka za usimamizi.

2. BIASHARA HURU:

Masoko yaliyo huru huchochea utekelezwaji wa usawa katika utendaji bora wa biashara kwa wateja ambao wanatofautiana viwango vya kiuchumi. Hili ni moja kati ya mambo yanayochagiza ulindwaji wa taarifa za wateja ambao wengi hawana uzoefu na mifumo ya kiteknolojia na taarifa zao zipo hatarini kudukuliwa bila ya wao wenyewe kujua. Usawa huu katika biashara huru hujumuisha sheria za kuzuia matangazo yenye lengo la kupotosha na utapeli, miiko ya kibiashara na wafanyakazi na kuzuia bidhaa zenye sumu au madhara kwa afya ya binadamu.

Hivyo huduma zenye usawa kwa wateja pia zinatakiwa kuzuia unyanyasaji kwa wateja na vizuizi visivyo haki vinavyowekwa na watoaji wa huduma za kifedha.

Eneo lingine ni kuhusu matumizi ya data za wateja ambayo inajumuisha ushikishwaji katika taasisi za mikopo na jinsi data hizo zinaweza kutumika kutengeneza vifurushi fulani vya huduma, tahadhari ya bei pamoja na ufanyaji wa minada.

Sheria hizi zinatakiwa kuwekwa ili kulinda haki ya faragha kwa wateja kwa mapana wakati huo huo zielezee kuhusu namna nzuri ya utoani wa taarifa hizo kwa taasisi zingine katika mazingira maalum kama ripoti za madeni na kadhalika. Haya yote ni hufanyika kwa kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa za kompyuta katika intaneti na mitandao.

3. MAFUNZO STAHIKI NA NIDHAMU YA KAZI:

Mfumo bora wa mafunzo kwa wafanyakazi na elimu kwa wateja kuhusu haki zao za kuhudumiwa hujenga kujiamini katika kutumia huduma za kifedha. Hii hujumuisha utaratibu wa kutoa malalamiko, uzembe na unyanyasaji ambao unafanywa na wafanyakazi au watoani wa huduma, jambo ambalo litamlinda mteja pindi mambo yatakapokwenda kinyume na utaratibu.

Mifumo hii ya kutoa mafunzo kwa wafanyakazi na elimu kwa mteja inajumuisha usimamiaji wa masanduku ya maoni ambayo yanapatikana kwa wingi katika vituo vya watoaji wa huduma za kifedha kama benki na taasisi za mikopo.

Mpaka sasa utaratibu wa kulinda taarifa za mteja tayari unafanyika, unaandaliwa au kupangwa katika nchi nyingi barani Afrika. Nchi zingine zina vielelezo kuhusu kulinda taarifa za wateja katika vifungu vya sheria zao. Nchi 25 barani tayari zimejumuisha utaratibu au mahitaji ya taasisi za kifedha katika sheria zao. Vile vile wakati huo huo zaidi ya nchi 35 tayari zina mawakala mahsusi wa kusimamia ulinzi wa taarifa za wateja. Lakini bado taratibu hizi ni dhaifu na zinajiendesha bila ya kuwa na msaada muhimu wa sheria mama. Kiukweli mawakala wengi wanaoshughulikia usimamiaji wa taarifa za wateja ni mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) na hawajajikita sana kwa wateja wa huduma za kifedha.

Nchini Kenya kupitia ripoti ya shirika la Financial Sector Deepening (FSD) Imegundulika kwamba taasisi mpya zote zinazoanzishwa huweka kiapo kulinda taarifa za wateja wao kwa mujibu wa malengo ya nchi hio katika sera zake kufikia mwaka 2030. Pia 25% ya watu wanaokwenda kuweka fedha benki katika mwaka 2010, uchunguzi wa mashirika ya FSD na CGAD wameonyesha “kushtuka” baada ya kukutana na tozo ambazo hawakujifahamu licha ya mwaka 2007 taasisi ya CBK kugundua aina 53 za tozo katika mabenki tofauti tofauti.

Afrika Mashariki tunajiandaa vipi na Ulinzi na Usimamizi wa Taarifa za Wateja katika masuala ya huduma za kifedha? Tujadili..👇👇