Tag: RIP Magufuli

MAWAZO YANGU

Bado nawaza kuhusu mambo mengi sana. Sijui itakuaje. Hizi sheria ambazo zinalenga kuhamasisha makusanyo ya kodi na mapato kwa serikali (which is not bad) zinanitafakarisha sana. Hata hivyo kodi na makusanyo haya yanapokuwa makubwa kuliko wastani wa uwezo wa walipaji hugeuka kuwa Unyonyaji kiuhalisia, hata kama zina-backup ya sheria halali. Serikali kama Baba/Mlezi na Msimamizi mkuu wa rasilimali za nchi inapaswa kuhakikisha watu inayowaongoza hawabanwi wala kubinywa haki zao za kikatiba. Nafikiri ni muhimu kuhakikisha zile sheria ambazo zilipitishwa lakini zinaonekana kunyonya na kukandamiza uhuru wa watu kutumia ubunifu wao katika kukuza uchumi kihalali, zifanyiwe marekebisho ama zifutwe kabisa. Mathalani Sheria ya vyombo vya habari, Sheria ya makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 pamoja na sheria ya Uchaguzi. Sheria hizi zinapaswa zitazamwe upya kabisa.

Yani sijui tufanyaje, lakini natamani sheria hizo zitungwe kwa kufuata maoni ya wadau wa nyanja husika pamoja na kuwahusisha katika mchakato mzima. Isitokee kama ilivyokuwa katika tume ya Warioba (watu wakatoa maoni yao wee, mwisho wa siku rasimu ikapigwa chini). Hizi sheria ndio muongozo wa wananchi katika shughuli zao za kila siku, sasa kwanini ziwazibie fursa ya kufika pale wanapopataka kimaendeleo kwa wepesi?

Ukiwa kiongozi wa umma, maana yake ni kwamba unawajibu kwa umma kupitia katiba kuhakikisha unalinda maslahi ya umma kwanza (sio chama wala kikundi fulani cha watu). Ndio maana viongozi wote hula kiapo cha Utumishi wa Umma kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao kisheria. Kile kiapo kina maana kubwa sana. Nawaasa viongozi wetu tuteteeni sisi tulio UMMA wa Watanzania. “Sauti ya Umma ni Sauti ya MUNGU” wamesema wahenga. Lakini kwa kuwa kuna Serikali, basi shida/malalamiko/changamoto zetu nyinyi viongozi mnapaswa kuzipaza katika baraza letu rasmi la wananchi (BUNGENI) na kuhakikisha zinafanyiwa kazi. Wawakilishi wetu huko Bungeni, mnatakiwa mfahamu kuwa ni wajibu wenu kutetea maslahi ya Wananchi KWANZA kabla ya Chama au kikundi fulani cha watu. Kuwa kiongozi wa umma ni wito na ni mzigo mzito.

Huwa nashangaa sana kusikia baadhi ya watu wanatumia nguvu kubwa na rushwa ili kupata uongozi wa umma. Watu hao hawatufai kabisa. Kuna muda natamani hata ikiwezekana mishahara na posho za Wabunge na viongozi wanaochaguliwa na wananchi iwe ni ile ya kiwango cha serikali. Yaani kila kiongozi aliyeapa kile Kiapo cha Utumishi wa Umma, alipwe kutokana na elimu yake na uzoefu wa kitaaluma. Mfano; Kiongozi huyu ana shahada, basi alipwe mshahara unaostahili kulipwa mtu mwenye shahada, kadhalika mwenye stashahada, cheti na kadhalika. Yasiwepo yale mambo ya kwa kuwa huyu ni Mbunge basi makusanyo yake kwa mwezi yawe ni milioni 12 au vitu kama hivyo. Kwa kuwa Sisi kama wananchi tuna vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Tafadhali vyombo vyetu mtusaidie kuwabaini watu hao na kuwazuia wasitulaghai na kupora chombo chetu kikuu cha maamuzi (Serikali). Tunawashukuru kwa kazi kubwa mnayoifanya usiku na mchana. Lakini tunawaomba mjiepushe na wanasiasa. Nyinyi ni watu muhimu sana kwetu sisi Umma wa Watanzania. Nyinyi ndio Taa yetu gizani na viatu vyetu kwenye miiba. Tunawategemea sana.

Mwisho, Kuondokewa na Rais wetu Mh. Dr. John Pombe Magufuli ni pigo kubwa kwa Taifa zima. Tumeumia sana kwa kuwa Rais wetu bado alikua na mipango na miradi mingi ambayo alitamani kuisimamia na kuiona ikiisha kwa mafanikio. Tumeumia sana. RIP Rais wetu Magufuli.

Lakini kwa kuwa sisi Tanzania ni Taifa imara, Mungu atatupitisha salama katika kipindi hiki na kwa uimara wetu tutayaendeleza mema yote ambayo Rais wetu ametuachia. His Legacy will live among us forever. Tuchape kazi. Tuirekebishe na kuilinda mifumo yetu. Tujivunie Utanzania wetu. Sisi ni Wamoja Daima.