Tag: mpaka wa taveta

MFUMO WA KUWEZESHA MALIPO BARANI AFRIKA (PAPSS)

Umeshawahi kuwaza kufanya biashara na wafanyabiashara wenzako na wateja kutoka nchi yoyote barani Afrika ambapo utaweza kutuma na kupokea fedha bila ya ulazima wa kubadili ziwe za kigeni kwanza? Sasa mfumo wa Kuwezesha malipo barani Afrika(PAPPS) unakwenda kukurahisishia mjasiriamali uwezo wa kutuma na kupokea fedha katika bidhaa/huduma unazotoa kila siku kirahisi zaidi. Leo nakupa fursa ya kufahamu namna mambo yamekuwa mazuri kibiashara barani Afrika. Fuatana nami mpaka mwisho wa makala hii..

Kwetu Moshi bwana ikifika mwezi February mpaka June kila mwaka huwa ni msimu wa parachichi na ndizi ambapo watu huuza sana parachichi ndani na nje ya nchi. Najua umeshawahi kuonja parachichi za Rombo, Marangu, Mwika, Machame nk, right?

Sasa bwana hizo parachichi unazokula ni 20% tu ya parachichi zote zinazovunwa kwenye miteremko ya mlima Kilimanjaro. Zaidi ya 80% ya parachichi hizo huuzwa nchini Kenya na kisha kusafirishwa kwenye barani Ulaya na Asia kupitia bandari ya Mombasa.

Bahati mbaya zaidi pale mpakani Holili kuna madalali wengi sana ambao hununua parachichi kutoka kwa wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali na kuziingiza nchini Kenya. Hawa jamaa bwana wajanja sana. Wao tayari wana vibali vya kuingia na kufanya biashara kati ya Tanzania na Kenya na zaidi wanafanya pia biashara ya kubadilisha fedha hapo mpakani (japo sina uhakika kama wanafanya hivyo kihalali). Kwa kufanya hivyo hawa Madalali wamekuwa wakijipatia faida kubwa sana hapo mpakani japo kuwa wao hawana mashamba wala parachichi zenyewe. Wao wanaconnect dots tu.

Na bahati mbaya zaidi wafanyabiashara wengi wadogo hawawezi kuvuka mpaka wakakutana na wateja wenyewe huko Kenya na kuuza bidhaa zao direct. So unaweza kuona namna hawa ndugu zangu wanapata tabu kufanikiwa kwenye biashara yao japokuwa wao ndo wanamzigo wote wa parachichi.

Huu ni mfano mdogo tu unaowakuta wafanyabiashara ambao wanauza bidhaa/huduma zao nje ya nchi. Hali hio pia inawakumba wale wa Tunduma, Rusumo, Taveta na maeneo mengine ya mpakani ambapo madalali (watu wa kati) wamekuwa wakitumia fursa hio kujinufaisha zaidi kuliko wakulima.

Kupitia changamoto kama hizo ndio maana nchi wanachama wa AU wakaanzisha Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) ili kuhakikisha biashara baina ya nchi wanachama zinafanyika kirahisi, tena bila vikwazo kama kodi na ushuru wa mipakani ambayo imekuwa ikiwaumiza wafanyabiashara.

Kuhusu AfCFTA ni nini na inafanya kazi vipi? tayari nimekuandalia makala murua kabisa kupitia link hii hapa chini:

Ukimalizana na makala hio sasa, tuendelee..

Pia nchi za kusini mwa Afrika kufikia July 2020 zikakubaliana kurasinisha biashara zao ili kuwezesha mazingira ya biashara baina ya nchi wanachama wa SADC kufanya biashara bila mrundikano wa kodi na ushuru. Hapa Prof. Kabudi (waziri wa mambo ya nje) na timu yake walicheza sana.

Kuhusu URASINISHAJI huo wa Kibiashara, ni nini na unafanyika vipi, tayari kuna makala yako kupitia link hii hapa:

Kuna mengi sana ya kujifunza hapo kwenye hio makala hapo.

Lakini licha ya yote hayo, mtaani mambo bado ni magumu kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo, kwanini? Kwa sababu taarifa za miamala bado zimetekwa na madalali. Wao ndo wanazuia bidhaa zote pale mpaka na kuzivusha na kufanya biashara nje ya nchi.

Hali hio bado inawatengenezea faida kubwa sana madalali hao na kuwaacha kwenye mataa wakulima na wafanyabiashara wadogo ambao kimsingi ndo wenye mali halisi.

SASA NINI KIFANYIKE ILI KUWEZESHA MALIPO KWA URAHISI?

Wakiwa wanajiuliza serikali, jumuiya za kimataifa na mashirika ya ndani na nje ya nchi, Shirika la African Export-Import Bank (Afreximbank) wakaja na suluhu ambayo inakwenda kumtingisha bwana Dalali na kumtengenezea mazingira mazuri ya kufaidika ndugu Mkulima na mfanyabiashara mdogo. Suluhu hio ni Mfumo wa Kuwezesha Malipo barani Afrika waliouita PAPPS.

Mfumo huu wa PAPSS (Pan-African Payment and Settlement System) ulizinduliwa rasmi tarehe 13 January 2022 katika hafla iliyofanyika nchini Ghana. Kabla ya hapo, mfumo huo ulikua kwenye majaribio tangu mwaka jana 2021 huku ukiwa unatumika ndani ya nchi 6 za Afrika Magharibi. Mtandao wa ICLG unatujuza kwamba mfumo huu unakwenda kuokoa dola bilioni 5 kwa mwaka ambazo hupotea kama makato mbalimbali katika malipo ya kibiashara baina ya wafanyabiashara wa nchi moja na nyingine.

Pia imefahamika kwamba zaidi ya 80% ya miamala inayofanyika maeneo ya mipakani ambayo ilihitaji mifumo ya kimataifa ya kulipa na kubadili fedha, sasa inakwenda kuokolewa na mfumo huu. Imagine wakulima na wafanyabiashara tunavokwenda kunufaika hapa.

UNAJIUNGA VIPI NA MFUMO HUO WA KUWEZESHA MALIPO?

Mfanyabiashara, mteja, mshiriki na mamlaka za serikali ambaye anahitaji kunufaika na mfumo huu kwa sasa anahitajika kujisajili kupitia link hii http://papps.com/connect/ kisha fuata maelekezo.

Changamoto iliyopo ni kwamba mfumo huu bado haujasambaa vya kutosha kiasi cha kuzama katika matumizi ya kila siku ya kibiashara. Hali hio inawalazimu waandaaji kupambana katika kushirikiana na Taasisi za Fedha na Serikali za Mataifa ya Afrika ili kujenga msingi imara wa matumizi.

Mbeleni wafanyabiashara tutaweza kutuma na kupokea fedha ndani ya Jumuiya zetu za kikanda na bara zima kupitia Miundombinu hii ambayo inazidi kuboreshwa katika kutafuta fursa za biashara na maendeleo ya kiuchumi.

Kwa fursa za biashara zinavyofunguka kupitia #AfCFTA pamoja #Urasinishaji unaofanyika katika Jumuiya za Maendeleo (SADC, EAC, COMESA etc) ni wazi mfumo huu wa PAPPS unakwenda kuwezesha malipo yaweze kufanyika kwa haraka na ufanisi wa hali ya juu sana. Hapa hutakiwi kubaki nyuma kabisa ndugu yangu.

NITAIFAIDI VIPI SASA HIO PAPSS NIKIWA MJINI?

Kwanza fahamu mfumo huu ni wa Kimtandao, hivyo, ukiwa popote unaweza kufanya biashara na mteja hasa kupitia ecommerce website yako au Digital Tools zingine kama Instagram, Twita na Whatsapp.

Kufahamu zaidi gusa tweet yetu hii hapa chini

Uzuri wa kuwa na e-commerce website unakuja hapa. Mteja akiwa nchi X anaiona bidhaa kwenye website yako, alipia, kisha wewe mjasiriamali unafanya delivery kupitia Gari, Ndege au Meli na bidhaa inamfikia vema.

Kuna OFA hapa kwa ajili yako. Wasiliana nasi mara moja kuipata:

Umeshawahi kufanya biashara na wateja/wadau walio nje ya nchi yako lakini ndani ya Afrika? Ulipata changamoto gani? Na umejifunza nini? Tushirikishe uzoefu wako kwenye comments Kwa sababu kuna mdau angependa kufahamu kinachoendelea huko nje ya nchi kibiashara, right?

Mfumo huu wa PAPSS unakuja kuleta ushindani katika Kampuni na Mashirika yanayofanya biashara ya fedha kiteknolojia (Fintech) barani Afrika.

Ukiwa kama Mjasiriamali na mdau wa Tech, umejipangaje na ujio wa mfumo huu? Weka majibu na mawazo yako kwenye comments hapo chini.

Je umependezwa na makala yetu hii ya leo?Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER)5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.

MPESA LIPA NAMBA YETU