Tag: microsoft

KWANINI UHAMIE WINDOWS 10?

Inawezekana unaipenda sana windows7. Inawezekana pia computer yako ina taarifu nyingi ambazo usingependa uzipoteze. Lakini mifumo ya uendeshaji (OS) kutoka kampuni ya Microsoft hukamilisha muda wa huduma zake kila baada ya miaka 10. Sasa leo nataka nikujuze, kwanini uhamie windows 10?

Sasa kufikia January 14 mwaka 2020, kampuni ya Microsoft iliacha kutoa matoleo (updates) mbalimbali kuhusu windows7. Hivyo, matoleo ya kiusalama, speed n.k yalikomea hapo na kufanya kama unatumia Windows7 baada ya tarehe hio, basi computer yako ipo hatarini kushambuliwa kimtandao kwa kuwa hakuna uimara wa kiusalama tena katika mifumo ya uendeshaji (OS) ya computer yako.

JE, COMPUTER ITAZIMA BAADA YA UKOMO HUO?

Hapana, computer yako yenye windows7 itaendelea kufanya kazi kama kawaida isipokuwa, Microsoft hawatakupa updates za kuisalama wala marekebisho yoyote ya kiautomatiki yaliyokua yakitolewa hapo kabla. Hii itaifanya computer yako kuwa katila hatari kubwa ya kuvamiwa na virusi au mashambulio ya kimtandao yatakayoelekezwa kwako muda wowote upenyo ukipatikana.

KWANI LAZIMA KUWEKA WINDOWS 10?

Sio lazima, wala hakuna mtu atakulazimisha kuanza kutumia windows10. Lakini ni jambo muhimu na la busara zaidi kuimarisha mifumo tendaji (OS) ya computer yako kwa kuwa windows10 imetengenezwa kwa uimara zaidi katika matoleo ya kiusalama, antivirus iliyojishikiza (built-in antivirus) na Windows defender ambazo hukulinda zaidi dhidi ya shambulio lolote la kimtandao.

KWANINI MICROSOFT WAMEIACHA WINDOWS 7?

Microsoft wana utaratibu wao wa kisera (Fixed Lifestyle Policy) ambao unazipa muda wa kuhudumu bidhaa zao mbalimbali. Mfano, Windows 7 ilitoka kwa mara ya kwanza October 2009, hivyo miaka yake 10 ya kuhudumu imehitimishwa January 14 mwaka huu (japo imechelewa kidogo kufikia ukomo wake). Hii windows 10 inayopigiwa chapuo ilizinduliwa mwaka 2015 na inatarajiwa kuhudumu kwa miaka 10 mpaka 2025. Sasa windows 10 ilikua ni bure kabisa kuinstall mpaka kufikia majira ya kiangazi cha mwaka 2016. Lakini, ofa hio iliishia hapo ambapo kwa sasa itakulazimu kulipia gharama za kufanya installation kama unatumia matoleo ya zamani ya mifumo tendaji. Windows10 ya kawaida (Home edition) hugharimu dola za kimarekani $ 139.99 na ile ya kiuweledi (Pro edition) itakugharimu dola za kimarekani $ 199.99 kuipata katika majukwaa ya kimtandao ya Microsoft.

Sasa Leo tukiacha yote hayo, nataka nikupe faida 10 za kutumia windows10 kama mfumo tendaji katika computer yako:

1. USALAMA

Windows10 imerithi mifumo ya kiusalama kutokea kwenye toleo la nyuma yake la windows8, hivyo kuifanya windows10 kuwa salama zaidi. Hii ni kwa kuwa code yoyote ambayo huanza kufanya kazi pale computer inapowaka, basi code hio ni lazima ipewe kibali na Microsoft au watengenezaji wa Hardware (Dell, hp n.k). Lakini zaidi ya windows8, windows10 imetengenezwa kuhakikisha codes zake haziwezi kuvukwa (kuwa bypassed). Kuboresha huduma, hivi karibuni Microsoft wameongeza features katika usalama zaidi za Ransomware Protection na Threat Protection. Zaidi katika kuzingatia usalama wako uwapo mtandaoni hakikisha unapitia makala katika link hii KWANINI USALAMA WA KIMTANDAO NI MUHIMU KWAKO? huu ni ukweli muhimu sana kuufahamu unapojiuliza kwanini uhamie windows 10?

2. SPEED

Kuanzia pale unapowasha computer yako, Windows10 hufunguka kwa spidi zaidi pengine kuliko computer zenye MacOS japokuwa mifumo tendaji ys Mac imeonekana muda mrefu kuwa ipo fasta zaidi. Safari hii imekula kwao. Injini ya 3D iitwayo DirectX 12, ambayo watengenezaji wa michezo ya video (video games) huitumia kurahisisha matengenezo na viwango vya michezo hio, hufanya kazi vizuri zaidi katika windows10 kuliko katika matoleo mengine.

3. CORTANA

Ebwana eeh, nna uhakika hata wewe huwa unafurahi sana pale unapoweza kuzungumza/kukiamuru kifaa chako kufanya jambo unalolitaka kwa sauti tu. Hapa watumiaji wa iPhone na yule “Siri” wao watakuwa wananipata vizuri sana. Sasa kwenye Windows10 kuna feature inaitwa “Cortana” ambayo ni teknolojia ya Sauti ambayo unaweza kuiamuru ifanye shughuli mbalimbali zilizopo kwenye computer yako kama “Hey Cortana, Cheza muvi ya Ray Kigosi, Imba wimbo wa Ray C, Onyesha picha ya Mr. Blue, zima computer.” nakadhalika. Hivyo vyote vinaweza kufanyika kwa sauti yako tu kupitia Kipengele hicho ndani ya computer yako yenye Windows10. Kumbe mambo ni murua bwana.

4. START MENU

Kama ulikua hufahamu basi Windows95 ambayo ilitoka mwaka 1995 ilikua na kipengele cha menu ambayo inafanana na menu ya windows8. Lakini watu waliilalamikia sana kuwa menu ile ilikua na mambo mengi hivyo kulazimisha Microsoft kuiondoa katika matoleo yake yaliyofuata. Lakini ajabu ni kwamba baada ya kubuni start menu ambayo ilitumika kwenye matoleo ya windows98 mpaka windows7 bado watu wengi walikua wakilalamika kuwa menu haijakaa vizuri mpaka ilipotoka windows8 na start screen yake. Hivyo toleo la Windows10 limeboreshwa zaidi na kuipa muonekano bora Start Menu yake na kuifanya yenye kuvutia na rahisi kutumia. Mudhui yake yameifanya iwe bora zaidi kwa kufanya Apps muhimu zaidi ziweze kuongezeka ukubwa na zile zenye umuhimu kidogo zinaweza kufanywa ndogo ili iwe rahisi hata kuchagua kwa kutumia kipanya (mouse).

kwanini uhamie windows 10?

5. TOUCH

Kama kila kifaa unachotumia kimetengenezwa kuruhusu teknolojia ya “Touch screen” kuanzia simu janja, redio za gari, tablet mpaka mifumo ya ramani elekezi (navigation systems). Sasa kwanini isiwezekane katika computer yako pia? Kuna watu watasema “oh kioo cha Pc ukiwa unakigusa gusa kinachafuka na kuharibika mapema” Sasa hilo linakuaje tatizo kwenye Pc na lisiwe kwenye simu yako ambayo kioo chake ni kidogo zaidi na unaitumia muda mwingi zaidi kwa siku. Basi kama ulikua hujui, computer zilizotengenezwa kupokea teknolojia ya “Touch screen” hufanya kazi kwa ufanisi zaidi pale zinapokuwa na Windows10 kuliko zile zinazokua na mifumo tendaji mingine. Pc kama Lenovo IdeaCenter Yoga A940, The Surface Pro7, Convertible Tablet na Acer T232HL ambazo zimewezeshwa na Touch screen hufanya kazi kwa ufanisi zikiwa na Windows10 kuliko hata Tablet za iOS katika mambo mengi.

6. KIVINJARI BORA

Hakuna tena mambo ya Internet Explorer. Sasa hivi ni mwendo wa Microsoft Edge ambayo ni balaa. Hii Microsoft Edge imefanywa kuwa bora sana katika speed, vipengele (features) kama web page markup na reading mode. Vile vile hii Edge inatajwa kuwa inatumia kiasi kidogo cha umeme (Power use) kuliko kiasi kinachohitajika katika kivinjari cha Google Chrome. Huu ndio ukweli muhimu sana kuufahamu unapojiuliza kwanini uhamie windows 10? Sasa Inategemewa katika maboresho yajayo kutakuwa na matafuto ya mtandaoni kupitia “Cortana” katika hii Microsoft Edge. Watu wamejipanga bwana.

7. KUCHAPA(TYPING) KWA SAUTI

Kirahisi kabisa, bonyeza alama ya Windows na kitufe H (Ili kuiamuru computer yako ianze kukusikiliza). Halafu anza kuongea kila unachotaka kichapishwe kwenye nyaraka yako. Hakuna haja ya kutatanisha mambo hapa. Wale wavivu wa kuchapa hapa ndo kwenyewe.

8. VIUNGANISHI VYA SIMU (SMARTPHONE TIE-INS)

Windows 10 bwana imeundwa kitaalamu sana. Yaani sasa unaweza kuunganisha smarphone yako na computer yako ili kuhakikisha shughuli zako unazofanya baina ya vifaa vyako zinakuwa zikishirikiana na kuungana (synchronized). Kuna App imeundwa katika Windows10 inaitwa “Continue on PC App“, Hii sasa hutuma kurasa za tovuti ulizopitia au nyaraka ulizozihifadhi katika computer yako moja kwa moja zinafika kwa simu yako na hivyo unapata wepesi wa kufanya shughuli zako kirahisi hivyo yani. Unaweza kutumia kivinjari cha Microsoft Edge kuunganisha shughuli zako za mtandaoni na kipengele cha Cortana kuunganisha kumbukizi (reminders) baina ya vifaa vyako. Watumiaji wa Android hapa ndo wanafaidi zaidi, nyie wengine wa iOS ebu tulieni kwanza. Kwa kutumia kipengele cha “Your Phone App” sasa unaweza kuona picha zako na video mara tu unapopiga kutokea katika camera ya simu yako. Hivi karibuni kutakuwa na toleo la Voice calling hata katika computer yako yenye Windows10. Mambo ni mazito.

9. DARK AND LIGHT MODES

Sikuizi bwana kila kitu ni Dark mode. Sio Whatsapp, Telegram, Instagram, kote kote yani ni mwendo wa Dark mode. Sasa Windows10 nayo haiko nyuma, toleo la mwezi May, 2019, kampuni ya Microsoft walisambaza upendo kwa “wapenda giza” pia ambapo sasa unaweza Kwenda kwenye Settings>Personalization>Colors. Halafu hapo unachagua rangi uipendayo halafu mambo yanakuwa safi kabisa. Kuna baadhi ya vivinjari (browsers) huheshimu aina ya rangi unayotumia katika windows10 yako mfano Microsoft Edge. Hii ndio raha ya kuufahamu utamu unapojiuliza kwanini uhamie windows 10?

10. GAMING BAR

Yes, kwa kubofya kitufe cha Windows kikifuatiwa na kitufe G (kama haiko active nenda kwa Settings>Gaming>Game Bar). Hapo sasa unaweza kupiga screenshot, kurekodi video, audio na mambo kibao kuhusu game unayocheza hapo. Ikiwa tu computer yako ina RAM ya kutosha pamoja na Processor nzuri. Basi hiki kipengele kinakuhusu vilivyo.

BONUS: Kuna watu wanahisi Windows10 ni nzito, ngumu kutumia na ina mambo mengi ambayo sio muhimu. FYI, kampuni ya Microsoft imefanya marekebisho ili kuhakikisha mtumiaji anafanya kazi zake kirahisi bila shida yoyote ya kiufundi. Na zaidi, wa wataalam (coders and gamers) wameongezewa vipengele ili kuhakikisha kazi zao zinapatiwa msaada stahiki kupitia matoleo ya Windows10.

Zaidi, hakikisha unapotumia Windows10 unapata huduma ya Internet (wi-fi) ili kuhakikisha matoleo muhimu ya kiusalama (security updates) unayapata kwa wakati. Tumia wifi nzuri ili usije ukapata gharama za ziada unapotumia bando lako la simu (ambalo kwa watu wengi hupigiwa bajeti kali).

Sasa tumekuwekea makala zingine kwa ajili ya kukupa maarifa na taarifa zaidi kuhusu namna nzuri ya kutumia teknolojia hizi kwa manufaa yako binafsi na manufaa ya uchumi wa biashara yako binafsi. Gusa link kisha makinika:

  1. WEBSITE INASAIDIA VIPI KUIMARISHA BIASHARA YAKO?
  2. UTAJUAJE KAMA KIFAA CHAKO KIMEDUKULIWA
  3. YAFAHAMU MASHAMBULIZI YA KIMTANDAO (CYBER ATTACK) NA ATAHARI ZAKE KATIKA BIASHARA YAKO

Kiufupi hii ndo Windows10 na umuhimu wake. Kama hujawahi kutumia OS zingine, hii inakufaa. Ukiwa na maoni yoyote ama ushauri kuhusu kufanya installation ya Windows10 katika computer yako, tafadhali wasiliana nasi kupitia namba yetu ya simu ya 0765834754 au barua pepe info@rednet.co.tz. Karibu sana.