Tag: masoko

ukiritimba katika biashara, ni asali au shubiri?

UKIRITIMBA KATIKA BIASHARA NI ASALI AU SHUBIRI?

Mara nyingi hutokea biashara ndogo hazina rasilimali nyingi kama washindani wao ambao ni Makampuni makubwa. Ile hali ya Biashara kuwa na ushindani mdogo/kutokuwa na ushindani kabisa ndio inaitwa ukiritimba (business monopoly). Sasa ukiritimba katika biashara, ni asali au shubiri? Leo tutakwenda kufahamu. Makinika mpaka mwisho.

Katika dunia hii ya leo ambayo inatawaliwa na sera za kibepari katika nchi nyingi, kitu kinachozingatiwa zaidi ni kuhakikisha FAIDA inazidi kuingia kila siku bila kuchoka wala kujali washindani wako watakuwa kwenye hali gani. Kibinadamu saa ingine hii inawezekana haijakaa sawa, lakini ndio UBEPARI wenyewe huo katika ubora wake.

Katika mfumo huu wa maisha, biashara huonekana imefanikiwa pale inapofikia hatua inakuwa na Ukiritimba wa kutosha katika masoko ya Bidhaa/Huduma zake. Kimsingi Ukiritimba sio dhambi, wala sio kosa kisheria. Ni ile jinsi bishara inaweza kutawala soko la bidhaa/huduma fulani katika jamii. Kuna ubaya gani hapo? Mfano kundi la WCB Wasafi kinavyotawala muziki nchini Tanzania. Sio kwamba hakuna ushindani kutoka kwa wasanii wengine, bali kundi hilo limeweza kutengeneza Ukiritimba sokoni na kufaidika zaidi kuliko kundi lingine lolote katika muziki nchini humo. Kwa unavyoona hapa ukiritimba katika biashara, ni asali au shubiri?

 ukiritimba katika biashara, ni asali au shubiri?

Kwenye siasa pia kuna Ukiritimba mwingi sana, hasa katika siasa za Afrika ambapo zimekuwa zikitawaliwa katika mifumo ya Kiimla, Utawala wa chama kimoja kwa muda mrefu (mfano CCM nchini Tanzania, kule Rwanda, Mali n.k). Hizi siasa za ukiritimba zimekuwa Asali na Shubiri vilevile katika nchi husika.

Kuhusu Ukiritimba katika siasa za Afrika tutaliona jambo hilo wakati mwingine. Leo twende na Ukiritimba katika Uchumi na Biashara kwanza.

UKIRITIMBA KATIKA BIASHARA UNATENGENEZWA VIPI?

1. SERA ZA KISERIKALI: Mara nyingi serikali hujaribu kuzuia ukiritimba katika biashara mbalimbali. Lakini, wakati mwingine serikali hio hio huhamasisha sera za ukiritimba au kuutengeneza ukiritimba wenyewe katika baadhi ya mashirika. Mfano Shirika la Ugavi wa umeme (Tanesco) limefanywa kuwa mtoa huduma ya umeme pekee nchini na kutotoa mwanya kwa mtoa huduma mwingine aingie sokoni.

Pia hapo kabla ya mwaka 2015 barabara ya morogoro jijini Dar es salaam ilikua na daladala nyingi kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali, jambo lililokuwa likitengeneza ushindani mkali katika sekta ya usafiri. Lakini baada ya kuzinduliwa kwa mradi wa mabasi ya Mwendokasi ushindani wa kibiashara katika sekta ya usafiri kupitia barabara ya morogoro umekuwa mdogo sana kiasi kwamba shirika la UDA(serikali) na lile la DART(binafsi) ndio pekee wameungana kuunda shirika la UDART na hivyo kulishika soko la usafiri katika barabara hio na hivyo kutengeneza Ukiritimba wa aina yake hapo.

Kwingine ni katika sekta ya madini ambapo sasa Mnunuzi pekee wa madini yanayochimbwa nchini na wachimbaji wadogo ni Serikali. Yaani serikali sasa imechukua dhamana ya kununua madini yote yanayochimbwa kabla hayajauzwa kwa wafanyabiashara wengine nje na ndani ya nchi.

Hii ni kwa mujibu wa sheria ya madini iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2018, 2019 (sikumbuki vizuri mwaka). Hapa nadhani wote mlimuona Bwana Laizer akivuta Hundi yake pale BoT baada ya kuuza mawe ya Tanzanite kupitia Wizara ya Madini. Kwa upande huu unauonaje ukiritimba katika biashara, ni asali au shubiri?

2. KUSHUSHA BEI:

Bila shaka utakubaliana nami kuwa kama unataka kuuza bidhaa/huduma zako kwa wingi na kuliteka soko, huna budi kushusha bei. Watoto wa mjini wanakwambia, Biashara nzuri na yenye mafanikio hufanyika Uswahilini. Kule ambapo barafu linauzwa 50/-, ice-cream 100/-, Muhogo 100/-, nguo za mitumba 3000/-. Huko ndiko biashara zinapofanyika haswa. Angalia ice-cream za Ukwaju kutoka kwa Bakhresa zinavyouzika halafu linganisha na zile zinazouzwa kwenye maduka ya mlimani city. Au tizama nguo za mtumba zinavyouzika pale Mwenge na Karume halafu linganisha na nguo zinazouzwa kwenye maduka makubwa pale Kinondoni na Tegeta. Utakuja kugundua kuwa Mlimani City, Kinondoni na Tegeta bidhaa zinauzwa lakini si kwa kasi kama zinavyouzika Mwenge, karume na Manzese. Hii ni kwa kuwa punguzo la bei linatengeneza ukiritimba wake hapo.

3. MATUMIZI YA HATIMILIKI:

Hii hufanyika kwa msaada wa serikali ambayo ina jukumu la kuunda sheria za kulinda na kudhibiti hatimiliki ambayo humpa mwenye nayo uwezo wa kutumia vizuri Mawazo yake, Ubunifu, Wimbo na Mipango. Mfano wa jambo hili unatoka katika uwanda wa teknolojia ambapo shirika la Microsoft (MSFT) ambalo hutumia hatimiliki za mfumo tendaji wake wa Microsoft Windows kutengeneza ukiritimba katika mifumo tendaji ya kompyuta inayotumia duniani kwa sasa.

Hatimiliki hio inawapa Microsoft haki ya kurekebisha na kuimarisha mifumo tendaji yake ili iendane na matakwa ya wateja wao na hivyo kuweza kutawala soko la mifumo tendaji duniani. Niambie, wewe umeshakutana na watu wangapi ambao kompyuta zao hazitumii microsoft windows? Bila shaka ni wachache sana au hakuna kabisa. Ndio ukiritimba wenyewe huo sasa.

4. KUMILIKI RASILIMALI ADIMU:

Moja kati ya njia bora zaidi za kutengeneza Ukiritimba (monopoly) katika masoko ya kibiashara ni hii. Nchini marekani shirika la Standard Oil chini ya uongozi wa John D. Rockefeller ambaye alikua ni kiongozi mwenye maono na bidii, aliweza kumiliki 90% ya njia zote za mafuta (oil pipelines and refeneries) katika nchi nzima ya Marekani. Baada ya kutawala soko la mafuta kwa muda mrefu, serikali ilianza kumpiga vita jamaa na kujaribu kumpokonya sehemu ya umiliki wa soko ambapo ilichukua miaka takribani 20 mpaka ukiritimba wa Kampuni hio ulipopungukiwa nguvu.

Makampuni kama Chevron Corporation (CVX), Exxon Mobil Corp (XOM) na ConocoPhillips Co. (COP) ni kampuni zilizozaliwa baada ya kufa kwa ukiritimba wa Standard Oil ya bwana John D. Rockefeller. (Chanzo mtandao wa Investopedia).

Sasa wewe unamiliki bidhaa/huduma gani ambayo unahisi ni adimu kweli kweli? Ukiijua hio itumie kutengeneza mtandao ukiritimba wa kutosha katika biashara zako.

KWANINI UKIRITIMBA (Monopoly) KATIKA BIASHARA UNATENGENEZWA?

Kama tulivyoeleza hapo mwanzo, mara nyingi serikali hupiga vita swala la ukiritimba lakini serikali hio hio huhamasisha uundwaji wa ukiritimba katika baadhi ya sekta sababu chache zifuatazo:

i. MSAWAZO WA KIUCHUMI: kuhakikisha Uchumi unakuwa katika viwango sawa sawa kutoka sehemu zote (economies of scale) ambapo lengo kuu ni kuwanufaisha wananchi kwa kuhakikisha gharama zinakuwa chini katika huduma za msingi za kijamii kama umeme, maji na usafiri.

Ndio maana unaona mashirika yanayotoa huduma za umeme na Maji (mfano DAWASCO na TANESCO) yanaendelea kuhodhiwa na serikali ili kuhakikisha yanatoa huduma stahiki kwa wanachi. Hebu waza siku kutokee kampuni 10 zinazotoa huduma ya usambazaji wa umeme ambayo kila moja itatakiwa kusambaza nguzo zake na miundombinu yake ya utoaji huduma pamoja na kufanya huduma za marekebisho kila inapohitajika. Huo usumbufu wake utakuaje huko mtaani? Hivyo ndivyo imefanya kuwe na mtoa huduma mmoja tu katika sekta hio ya nishati pamoja na zingine za maji na kadhalika.

ii. KUHAMASISHA UBUNIFU: Hii ni sababu muhimu kwanini ukiritimba unahamasishwa. Sera za Serikali kuhusu Hakimiliki zimeundwa ili kuhakikisha wabunifu na wasanii wanalida kazi zao na kufaidi matunda ya ubunifu wao vile inavyostahili. Kama wabunifu hao wasingekuwa na hakimiliki basi bila shaka juhudi zao, muda wa kujitolea pamoja na sadaka zingine ambazo wamezitoa katika kazi na biashara zao zingekuwa ni kazi bure. Hii ndio maana serikali imeweka sheria kusimamia hatimiliki za wabunifu katika sekta mbalimbali rasmi na zile zisizokuwa rasmi.

Hio ndio Ukiritimba katika Biashara za barani Afrika haswa kusini mwa jangwa la Sahara. Una lolote la kuongezea? Tafadhali tujulishe. Pia hakikisha unapitia makala zetu zingine hizi hapa tumekuwekea ili kuhakikisha unapata muendelezo mzuri wa somo ulilolipata leo. Gusa link kisha makinika:

  1. FAHAMU SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA
  2. KWANINI UITANGAZE BIASHARA YAKO?
  3. IJUE NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO
  4. IFAHAMU AINA MPYA YA UDALALI WA MTANDAONI (DROPSHIPPING)

KWANINI UITANGAZE BIASHARA YAKO?

Iwe ni shirika binafsi, taasisi za uma(serikali), mashirika ya dini au biashara binafsi, matangazo ni muhimu sana katika maisha ya taasisi au biashara binafsi. Kutuma barua pepe, kuanzisha kurasa katika mitandao ya kijamii au kufikisha taarifa za ana kwa ana kwa uma ni bure (haijumuishi gharama za moja kwa moja). Lakini kutangaza biashara ni gharama zaidi, hata hivyo inakulazimu kuitangaza biashara yako. Makampuni na mashirika duniani hutumia gharama kubwa sana katika kujitangaza japokuwa tayari wana majina makubwa na bidhaa/huduma zao zinajulikana duniani kote. Sasa swali la msingi, kwanini uitangaze biashara yako? Makinika hapa leo kupata majawabu.

Coca cola Company kwa mfano, mwaka 2015 walitumia dola bilioni 3.96, 2016-dola bilioni 4, 2017-dola bilioni 3.96. Kwa upande mwingine Pepsi ambao ni mpinzani wa kibiashara wa Coca cola duniani wao mwaka 2015 walitumia dola bilioni 2.4 kufanya matangazo yao, mwaka 2016- dola bilioni 2.5, mwaka 2017 dola bilioni 2.4. Hii ni kwa mujibu wa tovuti ya Investopedia (http://www.investopedia.com). Sasa, jiulize Kwanini ni muhimu uitangaze biashara yako.!?

1. MASOKO: Katika muktadha wa ulimwengu wa kibiashara, masoko ndiyo moyo wa biashara haswa. Yaani ili biashara yoyote iweze kuendelea kufanya vizuri, haina budi kuwa na soko la kutosha la kuhudumia. Jiulize, bidhaa unazosambaza/unazouza au huduma unayotoa, kuna kampuni au biashara ngapi ambazo zinafanya kitu hicho hicho unachokifanya.!? Kama hauko peke yako, basi hauna budi kutafuta masoko kwa hali na mali ili biashara yako ipate hadhira ya kuhudumia.

2. KUTAMBULISHA BIDHAA/HUDUMA MPYA: Ukuaji wa biashara/kampuni au taasisi yako hujumuisha kwa kiasi kikubwa ubunifu kila siku. Sehemu ya ubunifu huo pia huchagiza utambulisho wa huduma/bidhaa mpya kwa wateja wako. Ili uweze kuwafikishia taarifa wateja wako kuhusu huduma/bidhaa mpya unayoongeza katika biashara/kampuni au taasisi yako, unalazimika kuitangaza huduma/bidhaa hio mpya ili ifike kwa urahisi na usahihi kwa wateja wako.

3. ELIMU KUHUSU BIDHAA/HUDUMA ZITOLEWAZO NA TAASISI:Taasisi yako inapotoa huduma/bidhaa zake kwa mlaji wa mwisho au mteja wako hujumuisha zaidi sana elimu ya jinsi ya kutumia bidhaa/huduma hio. Sio watu wote watajua jinsi au njia za kuipata na kutumia kwa usahihi bidhaa/huduma zinazotolewa na taasisi yako. Vile vile ili elimu hio kuhusu bidhaa/huduma zako ipate kufika kwa mlaji wa mwisho au mteja wako huna budi kufanya tangazo. Hivyo matangazo ya namna hii yenye lengo la kutoa elimu ni muhimu sana katika kuhakikisha huduma/bidhaa zako zinafika kwa wateja lakini zaidi zinatumika kwa usahihi ule unaohitajika.

4.KUTENGENEZA MVUTO WA KIBIASHARA:

Matangazo ni njia bora zaidi kutengeneza mvuto wa kibiashara. Hapa kuna namna nyingi sana katika kutengeneza mvuto huu wa kibiashara kwa kutumia teknolojia ya matangazo. Aina ya mavazi au sare zinazohimizwa kuvaliwa katika taasisi yako, muundo wa rangi rasmi za taasisi, logo ya taasisi pamoja na jina la taasisi linavyohusiana na aina ya bidhaa/taasisi inayotolewa. Mvuto huu wa kibiashara hufanya matangazo ya kiautomatiki yanayokwenda moja kwa moja katika maisha ya kila siku ya mlaji wa mwisho au mteja. Huku mtandaoni tunatumia teknolojia ya SEO kutengeneza mvuto huu. Sasa kufahamu zaidi kuhusu SEO fuatana na makala hii hapa;

5. KUKUZA JINA LA KAMPUNI DUNIANI:

Matangazo ni sauti ya taasisi kuhusu bidhaa/huduma zake kwa wateja wao. Hivyo taasisi inavyofanya matangazo ndivyo inavyozidi kujiongezea wigo wa sauti yake kufika duniani kote. Duniani kuna kadiriwa kuwa na watu zaidi ya bilioni 7, hivyo unapofanya tangazo moja ni ngumu sana kuwafikia watu wote hao zaidi ya bilioni 7 duniani. Hivyo unapofanya matangazo kwa ajili ya wateja wako duniani mara kwa mara, unaimarisha jina la kampuni kitu ambacho huimarisha bidhaa/huduma zako zaidi pia.

6. KUJIKITA KWA WATEJA MAALUM TAASISI INAYODHAMIRIA KUWAPATA:

Kwa kawaida unapojihusisha na biashara ya kuuza nguo kama taasisi, wateja wako wakubwa watakuwa ni wauzaji wa nguo wadogo wadogo, wanamitindo na watu wengine wanaopenda kuvaa nguo za aina mbali mbali kila siku. Hivyo unapofanya matangazo ya taasisi yako, unajiweka kwenye nafasi ya kuwapata wateja haswa wale ambao taasisi imedhamiria kuwafikia.

7. UWEZO WA TAASISI KUHUDUMU:

Kwa kiasi kikubwa matangazo huimarisha uwezo wa taasisi kuhudumu. Hivyo taasisi yako inapofanya matangazo inajiweka kwenye nafasi ya kujiweka tayari kuhudumu kwa wateja wale wote wanaoletwa na matangazo hayo. Hivyo taasisi inayofanya matangazo hujiweka kwenye nafasi ya kuwa na ufanisi zaidi kwenye utendaji wake wa kila siku.

Hivyo kwa ufupi hayo ni baadhi ya mambo muhimu kuhusu Umuhimu wa Ufanyaji wa Matangazo katika taasisi/kampuni au biashara yako. Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi tukupatie usaidizi pale unapohisi kukwama katika biashara zako katika muktadha wa teknolojia ya habari na mawasiliano.

Namna bora ya kuitangaza biashara yako ni kupitia matumizi ya tovuti rasmi ya biashara yako pamoja na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuhakikisha biashara yako inabaki katika akili za wateja wako kila siku. Hivyo pitia makala kupitia links hizo hapo chini ili uzidi kufahamu mambo muhimu kwa ajili ya afya ya biashara yako.

  1. https://rednet.co.tz/kwanini-ni-muhimu-kuwa-na-websitetovuti-rasmi-ya-biashara-yako/ yenye kichwa “KWANINI NI MUHIMU KUWA NA TOVUTI RASMI YA BIASHARA YAKO?”
  2. https://rednet.co.tz/website-inasaidia-vipi-kuimarisha-biashara-yako/ yenye kichwa “WEBSITE INASAIDIA VIPI KUIMARISHA BIASHARA YAKO?” 
  3. https://rednet.co.tz/ifahamu-nguvu-ya-mitandao-ya-kijamii-katika-biashara-yako/ yenye kichwa “IFAHAMU NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO”

Una maoni au lolote kuhusu makala hii ya leo? Tafadhali, acha comment yako hapo chini na changia hoja yako. Karibu sana.

Je umependezwa na makala yetu hii ya leo?

Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?

Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.

Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.

Kwanini uitangaze biashara yako?