Tag: maamuzi sahihi

FANYA MAAMUZI SAHIHI KATIKA MUDA SAHIHI

Hebu piga hii hesabu hapo chap. Kwa mwezi unaingiza kiasi gani kama faida kutoka kwenye biashara yako? Tuseme 500,000/-. Na matamanio yako ni kuingiza kiasi gani kila mwezi? Jiambie hapo “Nataka niwe naingiza kiasi flani kila mwezi.” Tuseme 2,000,000/- kwa kukadiria.

Sasa kwa kuzingatia mfano huo hapo juu, ukweli ni kwamba kila mwezi unavyoshindwa kufikia matamanio yako unagharamika kiasi cha shilingi milioni 1.5 kwa kutofanya maamuzi sahihi kwa wakati na kuimarisha biashara yako.

MAAMUZI SAHIHI NI YAPI?

Wahenga walishasema “Kupanga ni kuchagua.” Lakini zaidi unapochelewa kuchukua uamuzi sahihi, fahamu kuwa unajiandaa kushindwa.

“Liwezekanalo leo lisingoje kesho” wanaongezea wahenga, Hii kwenye biashara ina maana kubwa sana, hasa kama wewe ni mtu makini unayetamani kuiona biashara yako ikikua na kuzidi kufanikiwa kila siku. Sasa leo ukimaliza kusoma makala hii utakuwa umepata mbinu sahihi za kukuza faida maradufu katika biashara yako. Hakikisha unazifanyia kazi mbinu hizi:

1. TAFUTA WATEJA WAPYA

Hii ni dhahiri kabisa. Lakini inatajwa kuwa ndio mbinu ngumu zaidi kuifanyia kazi. Kupata mteja mpya sio kazi ndogo. Wateja ndio moyo wa biashara yoyote ile. Tafiti zinaonyesha hugharimu mpaka mara 8 ya pesa kumpata mteja mpya zaidi ya kiasi kinachotumika kwa mteja aliyezeoleka/wa kudumu. Njia bora ya kupata wateja wapya ni kuhakikisha unajenga ukaribu na wateja wako wote hasa waliopo kwa kuwa Kizuri chajiuza chenyewe. Wengine wanaita Network Marketing, lakini watu wa mjini wanaita Connections. Hivyo, ukitaka kuongeza wateja hakikisha unakuza Connections zako.

2. BADILI MASHABIKI KUWA WATEJA

Hivi umeshawahi kuona huku kwenye mitandao (facebook, twitter, instagram nk) kuna mtu ana followers wengi 50k, 100k, 500k lakini bado anahangaika kupata wateja pindi akitangaza biashara yake fulani. Changamoto hii imekua ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na mambo kama kununua account za mitandao ya kijamii. Mfano wewe unauza viatu halafu kwa kuwa huna followers ukatafuta account yenye followers wengi uinunue ukidhani ndo itaboost biashara yako ya viatu. Lakini bahati mbaya account uliyokuja kununua ni ya mtu aliyekuwa anapost picha za nusu uchi au maudhui ya kilimo. Unafikiri utatoboa hapo? Ni ngumu kwa kuwa awali watu walifollow accounts hizo kutokana na muendelezo wa maudhui yake. So ukinunua account kwa kigezo cha kuongeza wigo wa biashara yako, hakikisha maudhui yaliyokuwepo kabla yanaendana na unachokifanya. Hapo kutoboa ni rahisi zaidi.

3. BADILI UTARATIBU WA UENDESHAJI

Unahitaji kuongeza mapato ya biashara yako huku ukipunguza gharama za uendeshaji kwa kadiri inavyowezekana. Ili kuongeza mauzo yako hakikisha unaongeza bidhaa/huduma za ziada zinazoendana na bidhaa/huduma kuu. Yani kwa mfano unauza chakula, tengeneza na juisi/ongeza na matunda hapo. Kama unatoa huduma za kisheria basi ongeza na machapisho kuhusu sheria mbalimbali na madiliko yake mara kwa mara. Ongeza ujazo wa malighafi za biashara yako. Yani hakikisha mteja wako anakuganda kwa kuwa anafaidi zaidi ya pesa anayolipa kupata huduma/bidhaa zako. Fanyia kazi hii.

4. TANUA WIGO WA SOKO LAKO

Hapa utake usitake, Teknolojia ya ICT lazima ichukue nafasi yake. Njia bora zaidi za kisasa kuhakikisha unafikia soko kubwa zaidi duniani na kwa haraka ni kutumia Huduma za Kimtandao kama matumizi ya mitandao ya kijamii kama facebook, twitter, instagram na LinkedIn na matumizi ya blogu na tovuti(website). Majukwaa haya ya kimtandao yamekuwa madhubuti katika kutengeneza soko kwa bidhaa/huduma mbalimbali dunia nzima. Kujua zaidi kuhusu umuhimu wa tovuti katika biashara unaweza kutembelea link hii https://rednet.co.tz/kwanini-ni-muhimu-kuwa-na-websitetovuti-rasmi-ya-biashara-yako/ yenye kichwa “KWANINI NI MUHIMU KUWA NA WEBSITE(TOVUTI) RASMI YA BIASHARA YAKO?” . Katika kutanua wigo wako huu wa kimasoko unaweza kutengeneza magroup ya facebook au LinkedIn ili kuonyesha bidhaa/huduma zako mpya na umuhimu wake kwa wateja wako, podcasts, tutorials na demos. Pima njia ipi inakufaa na yenye gharam ndogo zaidi.

5. TIZAMA BEI ZAKO TENA

Ukichunguza utagundua kuwa mteja siku zote anataka kupata huduma/bidhaa bora kwa bei nafuu. Upande wako kama mfanyabiashara unataka kupata faida zaidi kwa kila bidhaa/huduma unayomfikishia mteja. Hivyo hapo lazima busara na ushawishi wa hali ya juu utumike ili kuhakikisha kila upande unanufaika. Huu mchezo hauhitaji hasira. Angalia sokoni kwa watu wanaofanya biashara kama unayofanya wewe, angalia bei zao, angalia huduma wanazotoa, rudi kwako sasa ili kujua utaongeza/kupunguza kitu gani ili uweze kuhimili ushindani wa soko. Ikiwezekana katika vipindi fulani katika mwaka (sabasaba, eid, nanenane, Pasaka, Christmass, Mwaka Mpya, Nyerere Day) weka punguzo la bei (discount) kwa wateja wako. Hakikisha unawaweka karibu muda wote yani. Hii itakupa nafasi kubwa ya kutengenezea biashara yako uaminifu na uthubutu wa kununua kwa mtu yeyote.

6. KUWA NA MUENDELEZO MZURI (CONSISTENCY)

Unaweza kufanya yote tuliyojadili tangu mwanzo, lakini unapokosa muendelezo hapo unajisumbua tu. Hii dunia imejaa ushindani na tambua hauko peke yako unayefanya biashara hio unayoifanya. Hivyo cha msingi ni kuhakikisha unasurvive sokoni. Ukikaa kimya, hakuna mtu atakujua, hutapata wateja wapya, hata wale waliopo wataanza kukutilia shaka. Tambua pia, gharama za uendeshaji(umeme, maji, mafuta nk) huwa hazipungui kirahisi, lakini mapato ya biashara yanategemea juhudi yako ya kuuza. Usipouza huli. Zingatia hili.

7. FANYA KAZI

Hata kwenye Biblia imeandikwa, “asiyefanya kazi na asile.” Yani hakikisha mambo haya yote tuliyojadili hapa unayaweka kwenye uhalisia. Yasiishie kwenye makaratsi tu, toka nje, kutana na watu, onyesha umuhimu wako na jiuze kibiashara kwa kadiri inavyowezekana.

Ukiona matukio kama NyamaChomaFestival au TOTBonanza, hakikisha unashiriki ili kujijenga kibiashara na kuimarisha Connections zako. Mimi binafsi hizi mambo hazinipitagi ndio maana leo najivunia kukutana na watu mbalimbali kama kaka Togolani Mavura, Debora Da Silva kutoka Amici Designs, Angelika Farhan, wataalam kutoka TOTTech na wengineo wengi na kujenga ukaribu nao katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi, Teknolojia na Uchumi. Kuna nguvu kubwa katika kujumuika. Hakikisha kila unapojumuika na watu mbalimbali unaitumia fursa hio kwa manufaa zaidi. Usiache nafasi hizo zikakupita hivi hivi.

Tayari tumekuwekea makala hizi hapa chini katika links ili kusudu zikusaidie kuelewa somo la leo kwa undani zaidi. Gusa link kisha makinika:

  1. https://rednet.co.tz/fahamu-siri-ya-kufanikiwa-katika-kuwekeza/ yenye kichwa “FAHAMU SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA”
  2. https://rednet.co.tz/ifahamu-teknolojia-ya-qr-code-katika-biashara-yako/ yenye kichwa “IFAHAMU TEKNOLOJIA YA QR CODE KATIKA BIASHARA YAKO”
  3. https://rednet.co.tz/website-inasaidia-vipi-kuimarisha-biashara-yako/ yenye kichwa “WEBSITE INASAIDIA VIPI KUIMARISHA BIASHARA YAKO?”

Unalo lolote la kutushirikisha? Tafadhali usisite kuwasiliana nasi muda wowote utakapohisi umekwama. Tupo hapa kukuhudumia. Karibu.