UMUHIMU WA TEKNOLOJIA BORA KATIKA KILIMO
Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo duniani (FAO) mpaka mwaka 2050 watu wataongezeka mpaka kufikia bilioni 9.1 na kulisha namba hii ya watu, uzalishaji wa chakula duniani utahitajika kukuwa kwa 70% angalau. Kwa Afrika ambayo inatarajiwa kuwa na jumla ya watu bilioni 2 kufikia 2050, uzalishaji wa chakula kupitia sekta ya kilimo inabidi ukue haraka zaidi ya wastani wa dunia ili kupunguza dalili za baa la njaa. Sasa leo tuangazie umuhimu wa teknolojia bora katika kilimo. Teknolojia ina mchango gani? Makinika mpaka mwisho wa makala hii kufahamu.
Mpaka nyakati hizi bado sekta ya kilimo inakumbwa na majanga ambayo hayajapatiwa suluhu ya kudumu kama kudhoofu maendeleo maeneo ya vijijini ambapo kilimo ndipo hufanyika kwa kiasi kikubwa, kutokuwa na soko mbadala kwa mazao yatokanayo na kilimo, miundombinu mibovu, vita vya wenyewe kwa wenyewe, magonjwa kama UKIMWI, majanga ya kiasili pamoja na ukataji ovyo wa misitu.
Sasa katika zama hizi za Kidijitali, Teknolojia ina mchango gani katika kukuza sekta ya kilimo na kuboresha uchumi wa mkulima?
Simu za rununu (smartphones), mfumo wa GPS, vifaa vya RFID na barcode scanners ni baadhi ya vifaa vinavyotumika katika sekta ya kilimo katika juhudi za kuboresha uzalishaji ambapo picha za satelaiti kwa mfano, huweza kutumika kupima ukubwa wa eneo sahihi la kufanyia shughuli za kilimo kwa ubora wa hali ya juu. Vile vile vifaa maalum vinavyoweza kuhisi hali ya udongo (soil sensors) hutumika kujua ni aina gani ya mazao inafaa kulimwa kuendana na udongo wa mahala husika. Zaidi mamlaka za hali ya Hewa pia hutoa mrejesho bora kuhusu utabiri wa hali ya hewa kwa kutumia vifaa vya kisasa na teknolojia bora kwenye vipimo vyao.
Ugunduzi wa Programu za kompyuta na Applications za simu unaongeza chachu zaidi katika kufanya kilimo cha kisasa na kudhibiti taarifa muhimu katika utendaji wa hatua kwa hatua, kufanya miamala ya kifedha pamoja na kutafuta masoko. Applications maalum ziitwazo Mobile App for Agriculture and Rural Development (m-ARD) hutumika kwa usahihi katika kufanya miamala na kudhibiti maswala ya kifedha katika ufanyaji wa kilimo. Kupitia MPESA nchini Kenya, taasisi ya kilimo ya Kilimo Salama Agriculture Insurance imeongeza thamani ya bidhaa za wakulima kwa wastani wa 50% kwa bidhaa za kilimo, sawa na $150 kwa mwaka.

Je, wajua kwamba takribani theluthi moja (1/3) ya mazao yote yanayovunwa duniani kwa mwaka hupotea kwa kushambuliwa na wadudu waharibifu, magugu na magonjwa?
Sasa kwa kuligundua hili wataalam walibuni mbegu maalum katika maabara za kisayansi kwa kuboresha vinasaba (DNA) Za mazao na kufanikiwa kupata kitu walichoita Genetic Modified Organism (GMO). Kitaalam mbegu na mimea itokanayo na GMO imekuwa na faida nyingi katika kilimo zikiwemo; kuwa na uhakika wa kupata mazao mengi kwa kutumia mbegu kidogo tu. Vilevile GMO hizi zimetengenezwa zikiwa na ustahimilivu dhidi ya wadudu waharibifu na magonjwa jambo linalozipa uhakika wa kukuwa, kumea na kuzaa ipasavyo. Hata hivyo kinga hio dhidi ya wadudu waharibifu haiwazuii wadudu kama nyuki, vipepeo, minyoo wa ardhini na baadhi ya bakteria ambao huwa na jukumu muhimu katika uchavushaji wa mimea na hivyo kuleta mazao stahiki. Faida zingine ni kutunza na kuboresha rutuba ya udongo pamoja na kusaidia kuhifadhi maji ardhini, mambo ambayo yanaondoa hatari ya kutokea kwa baa la njaa duniani lakini zaidi, kuboresha uchumi wa mkulima.
Je unaamini kwamba wingi ni Faida?
Sasa majibu ya wataalam wa maswala ya kilimo duniani ni kwamba si mara zote wingi unaweza kuleta faida. Hii inajidhihirisha katika matumizi ya mbolea zinazotengenezwa maabara kiteknolojia katika kufanya kilimo ambapo kiasi kikubwa cha mbolea huweza kupelekea kudhoofisha mimea na kutishia kufifia kwa mazao kutokana na mlundikano wa kemikali zilizopo kwenye mbolea ambazo zikizidishwa ni hatari. Hivyo inashauriwa mbolea inayotumika iendane sawia na aina ya udongo, kiasi cha maji katika umwagiliaji na aina ya mazao yanayolimwa ili kuhakikisha mazao yanayotoka yanakuwa bora zaidi. Hata hivyo taarifa nyingi kuhusu matumizi ya mbolea za kisasa hupatikana kupitia applications za simu mahsusi kwa shughuli za kilimo ziitwazo m-ARD’s.
Shirika la maswala ya kilimo la M-Farmer Initiative Fund lilianzishwa mwaka 2011 kwa ushirikiano wa Mfuko wa hifadhi ya jamii wa Bill and Melinda Gates Foundation ili kuratibu, kufadhili na kukuza sekta ya kilimo barani Afrika. Shirika hili limepanga kufikia wakulima walioko katika nchi za Ethiopia, Malawi, Rwanda, Kenya, Zambia na Tanzania.
Hilo ni mojawapo la mashirika makubwa kuonyesha nia ya dhati katika kuendeleza shughuli za kilimo duniani, kuchochea umuhimu wa teknolojia bora katika kilimo na kupunguza baa la njaa, kuboresha biashara za mazao ya kilimo pamoja na kukuza uchumi wa mkulima mmoja mmoja. Mashirika hayo yanazindua mifumo ya kimtandao ya malipo, mikopo na bima za kidijitali. Kwa mfano shirika la FarmDrive la nchini Kenya limezindua huduma za kifedha mahsusi kwa ajili ya wakulima ambapo kupitia shirika hilo wakulima hata wasio na akaunti za benki na wakulima wadogo kabisa hupata mikopo huku ikisaidia taasisi za kifedha kuongeza huduma za mikopo ya kilimo kwa gharama nafuu.
Kwa wafanyabiashara na kampuni zilipo ukanda wa Afrika Mashariki hii ni fursa kwao kuelekeza macho yao katika sekta ya kilimo kama inavyofanya FarmDrive nchini Kenya na shirika la kimataifa la M-Farmer.
Unalionaje hili? (tafadhali share kwenye comments) Hivyo kupitia jitihada za mashirika hayo, wakulima sasa wanaweza kupata mbolea, mbegu bora na mifumo mizuri ya umwagiliaji ili kukuza shughuli zao. Mchakato huo huboresha kasi ya uzalishaji katika kilimo na kupunguza changamoto kwa kutumia takwimu sahihi katika utendaji wa shughuli za kilimo kwa kutumia data za kisayansi na hivyo, umuhimu wa teknolojia bora katika kilimo unazidi kuonekana. Kwa mfano matumizi ya vifaa vya umwagiliaji vinavyotumia nishati ya jua kusukuma maji kutoka katika chanzo chake kama mto, ziwa, bwawa au bahari. Vifaa hivi vimerahisisha sana swala zima la umwagiliaji.
Vilevile kwa kuzingatia ukweli kwamba mashamba mengi yapo maeneo ambayo ni mbali na huduma za mitandao ya simu na intaneti, hivyo kufanya huduma hizo kuwa hafifu, nchi kama Ethiopia imerusha satelaiti yake na kufanya wakulima kuwa katika nafasi nzuri kunufaika na mradi huo. Serikali za nchi zingine za Afrika Mashariki zinakwama wapi kwenye hili?

Hata hivyo zama hizi kutokana na kuimarika kwa miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji, pamoja na maendeleo katika sekta ya sayansi na teknolojia ya Habari na mawasiliano, imekuwa rahisi sana kupata taarifa kuhusu Hali ya Hewa, Hali ya soko na ushindani, mazingira ya miundombinu ya uchukuzi, mfumuko wa bei na uelekeo wa mahitaji ya wateja. Kilimo kimeja kufanyika katika namna rahisi sana katika kuuza mazao baada ya kuvuna, shukrani umuhimu wa teknolojia bora katika kilimo cha kisasa na chenye tija.
Kufahamu zaidi namna unavyoweza kuimarisha shughuli zako za kilimo kwa kutumia teknolojia tafadhali pitia makala zilizomo kwenye links hizi hapa: