Tag: fintech

IFAHAMU TEKNOLOJIA YA QR-CODE KATIKA BIASHARA YAKO

Kwa kasi ya maendeleo ya kiteknolojia inavyozidi kuchanja mbuga, watu wanatumia sana simu janja kwa matumizi mengi zaidi ukiacha kupiga simu na kutuma ujumbe. Uwezo wa kununua bidhaa na kupata huduma haraka umewezeshwa zaidi kupitia ujio wa QR-Codes. Sasa leo ifahamu teknolojia ya QR-Code katika biashara yako. Makinika.

Hizi QR (Quick Response) codes zinaweza kusomwa na kudadavuliwa vyema kwa kutumia Simu janja na vifaa maalum vya kielektroniki (QR-scanners) na hivyo kujenga wepesi kwa watu wa masoko kuingiza maelezo kuhusu majukwaa yao kupitia hizi QR Codes. Yani maisha ya kibiashara yamekuwa mepesi kweli.

QR-codes hizi huweza kuwekwa katika mabango, magazeti, kurasa za tovuti na vyombo vingine vya kimasoko ili kurahisisha usambazaji wa bidhaa na huduma kwa haraka na wepesi zaidi. Matumizi ya QR-Codes yamekuwa yakizidi kutanuka kila uchwao ambapo katika kipindi cha mwaka 2018/19 peke yake, matumizi ya QR Codes duniani yaliongezeka kwa 28% huku ongezeko la muingiliano katika kipindi hicho likikuwa kwa 26% (chanzo: akaunti ya Blue Bite, mtandao wa medium).

QR CODES ZINA TOFAUTI GANI NA BARCODES?

Japokuwa Barcodes zilianzishwa miongo mingi kabla, QR Codes zimekuja na mapinduzi makubwa ndani ya muda mfupi.

1. Kama ulishawahi kununua bidhaa ya kiwandani hasa zile zinazouzwa katika supermarkets, utagundua bidhaa hizo zina alama fulani za vimistari pamoja na namba. Alama hizo ndio huitwa BARCODES. Sasa hizo Barcodes hutumika kuhifadhi maelezo muhimu kuhusu bidhaa husika kama jina la bidhaa, mtengenezaji, bei, kiwango cha ubora n.k. QR Codes kwa upande wake hufanya kazi sawa sawa na hizo Barcodes, isipokuwa tu katika QR Codes, zina uwezo wa kuhifadhiwa data nyingi kwa mamia zaidi katika nafasi ndogo.

2. MUONEKANO: Hii ndio tofauti kubwa katika ya hizi teknolojia mbili. Kwa kutizama tu unaweza kujua ipi ni QR Code na Ipi ni Barcode. Hebu tizama mifano hii hapa chini.

ifahamu teknolojia ya QR-Code katika biashara yako. Makinika.

3. UWEZO WA KUJISAHIHISHA: Kwa utofauti huu, QR Code inakuwa bora zaidi kuliko Barcode na kujitofautisha katika viwango vya matumizi. Muonekano wa QR Code unaifanya iweze kutoa taarifa kuhusu bidhaa/huduma vizuri hata kama ikitokea sehemu za alama hazionekani vizuri au zimechanika tofauti na Barcode ambapo ukifutika mstari mmoja tu Barcode inashindwa kutoa maelezo kamili kuhusu bidhaa/huduma.

QR CODES HUTUMIKA WAPI NA WAPI?

Kimsingi QR Codes hutumika katika kuhamasisha muingiliano katika ya mteja na huduma kupitia alama za kielektroniki kwa uharaka zaidi kwa kutumia simu janja au QR-Code scanners. Hii ni mbinu bora sana ya kimasoko katika kurahisisha utoaji huduma na uwezeshaji wa malipo/miamala ya kifedha. Sasa tuone maeneo ambayo QR Codes zinatumika:

1. KUELEKEZA WATUMIAJI KATIKA KURASA/TOVUTI:

Unaposcan QR Code, inaweza kukuelekeza katika kurasa fulani maalum au tovuti ambayo maelezo yake yamefichwa katika CODE hio. Zoezi hili unaweza kulifanya kwa wepesi kupitia QRCode iliyopo kwenye tangazo hili ambayo itakuelekeza katika fomu maalum ya kujiandikisha kuhudhuria mafunzo yanayojieleza.

2. KUPIGA SIMU NA KUPATA MAWASILIANO:

Katika mikutano ya kibiashara mara nyingi watu hukutana na kubadilishana mawasiliano kwa wingi. Lakini zoezi hilo hufanywa jepesi kwa kutumia QR Code ambapo kitendo cha kuscan tu hukuwezesha kupata mawasiliano yote muhimu kuhusu mtu fulani.

Kinachofanyika ni kujaza taarifa muhimu katika QR Code kisha CODE hio hupachikwa katika Business Card mara nyingi. Hivyo unaposcan unapata mawasiliano yote pasi na kuhangaika kuandika namba moja moja katika simu yako.

simu za michongo Faida za kutumia Google kama Jukwaa la biashara yako.

3. KUPAKUWA APPS MTANDAONI:

Unaposcan QRCode katika masijala za Aplikesheni za mitandaoni, basi unakuwa na uwezo wa kupakuwa App husika kirahisi bila ya kuhangaika kutafuta App hio mitandaoni. Unapoikuta QR Code wewe scan tu, mambo mengine yatajiendeleza yenyewe kirahisi.

4. KUJUA MAHALI BIASHARA ILIPO:

Naam, kupitia ramani za kimtandao kama Google Map, mtumiaji anaweza kuscan QR Code ya biashara na mara hio akaweza kuona mpaka mahali/location biashara hio ilipo. NOTE: Location hio lazima iingizwe kwanza katika QR Code na mfanyabiashara husika.

5. KUFANYA MANUNUZI NA MALIPO:

Pengine hii ndio njia maarufu zaidi ambayo QR Code hutumika. Makampuni ya huduma za mitandao yameingiza na kuboresha sana njia hii katika kufanya manunuzi na malipo. Mara nyingi wafanyabiashara hutumia njia hii katika kutoa punguzo la bei au kufanya matangazo (promo) kwa bidhaa/huduma fulani. Ni mwendo wa kuscan tu na malipo yako unakuwa umekamilika mara hio. Unachotakiwa kufanya kama mfanyabiashara ni kuhakikisha QR Code yako inafanya kazi ile uliyoiamuru (Call-To-Action). Mtumiaji hatakiwi ajiulize afanye nini baada ya kuscan hio code.

HIZI QR CODES ZINAFANYA KAZI VIPI?

Ili uweze kutengeneza au kutumia QR Code ukiiona mahali unatakiwa kuwa na vitu vifuatavyo:

>QR Code Generator: Kuna majukwaa mengi sana mtandaoni ambayo unaweza kuyatumia kutengenza QR Code kwa matumizi yako unavyotaka. Baadhi ya majukwaa hayo Ni pamoja na http://qrcode-monkey.com na http://the-qrcode-generator.com . Katika majukwaa haya unaweza kutengeneza QR Code yako, ukaweza na maelezo kama namba ya simu, tovuti, location nakadhalika. Lakini pia yapo majukwaa ambayo unalazimika kulipia ili uweze kutengeneza QR Code yako.

Majukwaa hayo ni pamoja na KAYWA na ni salama zaidi pale unapotaka kutengeneza QR Code ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kurahisisha malipo yoyote. Vya bure vina madhara sana hasa katika maswala ya kifedha. Kuwa makini hapo.

>QR Code Readers: Hizi ni Apps ambazo unazipata katika simu yako mahsusi kwa ajili ya kutambua QR Code na kukupeleka kule kunapotakiwa kwenda. Kwa watumiaji wa iPhone unaweza kupakuwa App inaitwa i-nigma ambayo inatajwa kama App bora zaidi duniani katika kuscan hizi QR Codes. Kwa watumiaji wa Android unaweza kupakuwa App iitwayo Barcode Scanner (watumiaji wa tekno nao wamo hapa.)

KWANINI UTUMIE QR CODE KATIKA BIASHARA YAKO LEO?

Mwaka 2019 matumizi ya QR Code katika kufanya malipo ya bidhaa na huduma yalipata umaarufu mkubwa sana duniani huku makampuni makubwa kama Mastercard na Paypal yakithibitisha matumizi katika kutambua account za wateja na kuidhinisha malipo.

Tafiti zinaonyesha kuwa wateja wanaolipia kwa kutumia QR Code hufanya manunuzi makubwa zaidi. Sasa leo hizi ndizo sababu zitakufanya ifahamu teknolojia ya QR-Code katika biashara yako. Mwaka 2013 Adobe mobile consumer uliowahusisha wstumiaji wa simu 3,075 ulionesha majibu haya;

•46% ya wateja waliscan ili kupata discount

•42% walitumia QR Code kama tiketi

•67% walishuhudia huduma za QR Code katika maduka ya mtaani.

Mpaka kufikia mwaka 2020 takwimu hizo zinatajwa kuongezeka maradufu zaidi. Lengo kuu hapa ni kuhakikisha QR Codes zinasaidia wateja kufanya shughuli zao kwa wepesi zaidi.

Makala hizi hapa chini zinarandana na somo ulilolipata leo. Zitakusaidia sana ukizipitia zote. Gusa link kisha makinika:

  1. FAHAMU KUHUSU MAPINDUZI YA 4 YA VIWANDA DUNIANI
  2. UMUHIMU WA TAKWIMU KATIKA UTOAJI WA HUDUMA BORA KWA WATEJA
  3. UGUNDUZI WA KITEKNOLOJIA KUELEKEA KATIKA MUSTAKABALI WA SEKTA YA UZALISHAJI MALI

Umejifunza nini kwenye makala ya leo katika ku ifahamu teknolojia ya QR-Code katika biashara yako. Tafadhali toa maoni yako na sambaza hii kwa jirani yako.

Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.

USAFIRISHAJI NA MIUNDOMBINU KATIKA USTAWI WA BIASHARA AFRIKA

Mtandao wa usafiri kwa njia ya nchi kavu barani Africa unajumuisha barabara na reli ambapo kwa wastani umechukua kilomita 6.2 kwa kila eneo la kilomita za mraba 100. Zaidi ya 60% ya mtandao mzima wa barabara haijatengenezwa kwa kiwango cha lami. Zaidi, pungufu ya 40% ya barabara za lami ndizo zilizo kwenye hali nzuri ya kupitika muda wowote. Sasa sekta hii ya usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika inatoa matumaini gani?

Mtandao wa njia za reli umeundwa kwa njia moja (single-track lines) ambazo huanzia maeneo bandarini kuelekea maeneo mbali mbali ya nchi/bara zikijumuisha viungio vichache tu njiani kuunga njia moja ya reli na nyingine (inter-linkages). Muundo huu wa reli zilizopo barani Afrika uliundwa nyakati za ukoloni na tangu wakati huo, ni marekebisho machache tu yameweza kufanyika ili kuwezesha treni ndefu zaidi zinazotumia dizeli kupita ambapo treni nyingi kati ya hizo hazitumiki tena kwa sasa.

Tukiangazia eneo la bandari, chini ya 50% tu ya matumizi ya bandari hutumika ikiwa ni pungufu ya mahitaji sahihi ya bandari hizo, jambo ambalo huchochewa na ucheleweshwaji wa mizigo na taratibu za forodha. Hali kadhalika, Afrika ndio inaongoza duniani katika ukuaji wa sekta ya viwanja vya ndege haswa kufuatia kuazishwa kwa soko huru lililoanzishwa baada ya makubaliano ya YD (Yamoussoukro Decision) yaliyofanyika mwezi November, 1999. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Afrika AU iliyotolewa mwaka 2014.

USAFIRISHAJI BARANI aFRIKA.
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.

Sasa changamoto; Je, sekta hii ya Usafirishaji na Miundombinu inaathiri vipi ukuaji wa biashara barani Africa? Na je, matumizi ya Teknolojia yana mchango gani katika kuboresha sekta hii ili kuinua biashara?

Kutokana na hali duni ya miundombinu na huduma za usafirishaji, gharama za kusafiri barani Afrika ni kati ya gharama ghali zaidi duniani, jambo ambalo linadhoofisha ushindani wa kibiashara katika masoko yote, ya ndani ya nchi na yale ya kimataifa.

Ripoti ya Tume inayoshughulikia Uchumi barani Afrika (ECA) imetaja kwamba nchi zisizo na bandari (landlocked countries) gharama za usafiri zinaweza kufikia robo tatu ya thamani ya bidhaa inayosafirishwa. Kwa mfano kusafirisha gari kutoka Japan mpaka Abijdan nchini Ivory Coast hugharimu US $1,500. Lakini kusafirisha gari hilo hilo kutoka kutoka jijini Abidjan hadi Addis Ababa hugharimu US $5,000. Kufahamu zaidi kuhusu mchango wa Teknolojia katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi kupitia link hii hapa yenye kichwa MAPINDUZI YA KITEKNOLOJIA KATIKA SEKTA YA USAFIRISHAJI NA UCHUKUZI. Ukimaliza hapo tuendelee na mada yetu ya leo.

Changamoto za Usafirishaji barani Africa.
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.

Gharama za usafirishaji zimetajwa kusababishwa na viwango vikubwa vya forodha, tozo za ucheleweshwaji, hasara zitokanazo na ajali pamoja na ukosekanaji wa fursa. Changamoto hizi huchagizwa zaidi na uduni wa miundombinu ya kiuchukuzi pamoja na huduma zinazotokana na nyanja hiyo.

Nayo programu ya maendeleo ya miundombinu barani Afrika (PIDA) katika ripoti yake imeainisha kwamba gharama za kiuchumi zinazosababishwa na changamoto za usafirishaji katika Mtandao wa Miundombinu ya Usafirishaji barani Afrika (ARTIN) zinazidi US $170 bilioni kwa mwaka kufikia mwaka 2014.

Changamoto hizo zimetajwa kusababishwa na;

•Kutokuwa na utendaji wa taratibu za kuwezesha biashara katika majukwaa ya ARTIN (kujumuisha bandari na vituo vya mipakani).

•Sera za nyanja ya usafirishaji ambazo zinapelekea kudhoofika na kuongezeka kwa gharama za usafirshaji kwa njia ya barabara pamoja na viwango duni vya barabara katika nchi nyingi barani Afrika.

• Sera za kiuchumi zinazozuia utendaji mzuri pamoja na utanuzi wa mifumo ya reli.

• Nyanja ya usafiri wa anga na Sera za kiuchumi zinazozuia uanzishwaji wa vituo vya anga vya kikanda, jambo linalotajwa kusababisha kuongezeka kwa gharama za usafiri huo.

Kufuatia changamoto hizo, Je, teknolojia ina mchango gani katika kuimarisha biashara na kupunguza gharama za uendeshaji?

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuelekea mapinduzi ya nyanja zote za kiuchumi. (Yaani tutaendelea kuwa juu kileleni😁). Mapinduzi katika matumizi ya simu kutoka simu za mezani mpaka simu za rununu (smartphones), huduma za kifedha kielektroniki (fintech), biashara za kielectroniki (ecommerce) na kadhalika vimekuwa sehemu muhimu sana katika kurahisisha utendaji wa kibiashara katika sekta ya miundombinu na usafirishaji.

Benki ya Dunia (WorldBank) inaripoti kwamba ubunifu wa kiteknolojia umewezesha sana muingiliano wa kibiashara kwa kuzingatia ongezeko la watumiaji wa Intaneti huduma za simu. Kipimo cha wiani (density) katika matumizi ya huduma za intaneti kwa kila watu 100 waliopo eneo la Kusini mwa jangwa la Sahara, ni watu 17 tu ndio wameonekana kuwa watumiaji wa intaneti katika mwaka 2015.

website inasaidia vipi kuimarisha biashara yako?
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika

Utafiti huo unakolezwa wino na shirika la kimataifa linalodhibiti mawasiliano ya simu GSMA ambapo kwenye ripoti yake ya mwaka 2018 limeangazia kwamba, eneo la kusini mwa jangwa la Sahara lilikua na kasi ya kupenya kwa matumizi ya simu ya 44% kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 kukiwa na watumiaji takriban 444 milioni sawa na 9% ya watumiaji wote wa simu duniani. Vile vile katika kipindi cha mwaka 2017-2022 watumiaji wa simu katika eneo hilo wataongezeka katika kiwango cha CAGR cha 4.8% ambayo ni zaidi ya mara mbili ya kiwango cha ongezeko kwa dunia nzima katika kipindi hicho hicho. Pia kasi ya kupenya kwa matumizi ya simu inatajwa kufikia 50% kufikia mwishoni mwa 2023 na 52% mpaka mwaka 2025.

Kufuatia uchunguzi huo, sekta ya usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara barani Afrika inatajwa kuongezewa nguvu na maboresho zaidi ili kuendana na kasi hio ya ukuaji katika ICT. Matumizi ya GPS katika usafiri wa taxi yamerahisisha zaidi gharama na muda wa kutoka sehemu moja na nyingine, huku maboresho ya miundombinu kama barabara na viwanja vya ndege yakichagiza kasi ya sekta hio.

Zaidi, mtandao wa huduma za Posta na EMS unajumuisha takriban ofisi 30,000 barani ambazo ni muhimu katika kuwezesha e-commerce trade. Kwa kuliona hilo kampuni kama DHL zimejitosa kuhakikisha teknolojia inabadili huduma za posta kuwa rahisi zaidi.

Mfanyabiashara, umejiandaa vipi na jambo hili?

Je umependezwa na makala yetu hii ya leo kuhusu usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika?

Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?

Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.

Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.

USAFIRISHAJI NA MIUNDOMBINU KATIKA USTAWI WA BIASHARA AFRIKA
teknolojia ya huduma za fedha kwa njia ya kielektroniki (fintech)

TEKNOLOJIA YA HUDUMA ZA FEDHA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI (FINTECH)

Uchumi wa Africa mpaka sasa hukua kwa kutegemea sekta za asili kama kilimoufugaji na biashara. Hata hivyo ujio wa teknolojia ya huduma za kifedha kwa njia ya kielektroniki (Fintech) utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendesha uchumi katika kufanikisha maendeleo kiujumla. Sasa tuangalia teknolojia ya huduma za fedha kwa njia ya kielektroniki (fintech), zina mchango gani kwako leo?

Uchunguzi umeonyesha kwamba matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu za mkononi yameongezeka sana ndani ya miaka 10 iliyopita ambapo imeonekana eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara ndio limekuwa kinara wa kubuni na kutumia huduma hizi za kifedha kwa kutumia simu za mkononi duniani kwa sasa.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Fedha duniani (IMF) umebaini kwamba takriban 10% ya pato la taifa katika miamala ya kifedha hufanyika kwa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi. Hii ni matokeo bora zaidi ukilinganisha na 7% ya GDP katoka bara Asia na chini ya 2% ya GDP kutoka sehemu zingine za dunia.

Sasa swali, hii Fintechs ni nini!? Na ina manufaa gani kwa wafanyabiashara walio Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara?

Shirika la EY linaifafanua FinTech kama Shirika/Kampuni inayojumuisha ubunifu katika utendaji wa biashara pamoja na technolojia ya programu za kompyuta katika kubuni, kuwezesha na kusambaza huduma za kifedha. Hizi FinTechs zinaweza kuwekwa kwenye makundi mawili;

i. FinTechs zinatoa huduma za kifedha e.g TALA App.

ii. FinTech zinazowezesha huduma za kifedha Vodacom na MPESA n.k (tutayajadili zaidi kwenye makala zetu zijazo)

Sekta hii ya FinTech katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA) inajumuisha zaidi ya makampuni 260 ambapo 80% katika hizo ni kampuni za ndani na 20% ni kampuni za kimataifa. Vile vile imeonekana idadi ya makampuni haya mapya imeongezeka katika kiwango cha CAGR (Compound Annual Growth Rate) cha 24% ndani ya miaka 10 iliyopita.

Hata hivyo ripoti zinaonyesha kwamba Afrika Mashariki itaendelea kuongoza katika ukuaji wa sekta hii kwa 6.3% ya ukuaji wa uchumi mwaka huu 2019. Hii ni kutokana na Ethiopia, Rwanda, Tanzania na Uganda zote zinatarajia kurekodi pato la Taifa la zaidi ya 6% mwaka huu ambayo ni zaidi ya nchi zilizo maeneo mengine ya Africa. Hii ni kutokana na uwekezaji katika miundombinu na utanuzi wa huduma za kifedha na mawasiliano.

Takriban theluthi moja (1/3) ya michango ya harambee zilizofanyika barani Africa mwaka 2017 iliwezeshwa na kampuni za FinTechs. Hii inatiliwa mkazo kwa kuwa 60% ya akaunti za huduma za kifedha kwa njia ya simu duniani zimegundulika kuwepo katika eneo la SSA. Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanya na benki ya Ecobank.

Pia imeonekana sekta hii ya FinTechinaendelea kuwa imara katika muda wa miaka 3 kutoka makadirio ya dola za kimarekani 200 milioni mwaka 2018 hadi 3$ bilioni mwaka 2020. Kiasi kikubwa cha uwekezaji katika muda huu kimeonekana kuelekezwa KenyaNigeria na Afrika Kusini. Vile vile inategemewa kwamba kufanikiwa kwa Fintechs katika nchi hizo kutatanua mafanikio katika nchi zingine za Kiafrika.

MAENDELEO: Ujio wa FinTechs umebadili sana jinsi ya kufanya biashara duniani. Kutoka Crowdsourcing ambayo ni njia inayotumika kufanya usaili wa miradi mbalimbali mtandaoni kupitia intaneti na kupokea ruzuku, mpaka njia ya huduma za kifedha kwa njia ya simu. Wafanyabiashara na wajasiriamali hawajawahi kupata njia rahisi zaidi kwenye utandaji wa biashara zao kwenye maswala ya fedha kuliko hii.

Kupitia Fintechs sasa wafanyabiashara wanaweza kusambaza bidhaa/huduma kwa watu mbali mbali na kupata malipo ndani ya muda mfupi zaidi. teknolojia ya huduma za fedha kwa njia ya kielektroniki (fintech) inazidi kujisombea watumiaji kwa sababu inaonyesha namna inavyoweza kusaidia katika kujikwamua kwenye maendeleo ya kiuchumi na kiutamaduni.

TEKNOLOJIA YA HUDUMA ZA FEDHA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI (FINTECH) HAINA MIPAKA:

Kutuma pesa nje ya mipaka ya nchi napo imekuwa rahisi zaidi. Mfumo huu ulioondoa mipaka ya kijiografia kwenye kurusha pesa umepunguza gharama kutoka ilivyokuwa mwanzo kwa njia ya benki ambayo ni ghali mno. Hivyo FinTech imewawezesha wajasiriamali na viwanda vidogo kutuma na kupokea pesa kwa gharama ndogo zaidi.

KUONGEZA THAMANI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA KIFEDHA: Eneo hili limetawaliwa na ubunifu ambao unawezesha kuongezeka kwa thamani katika matumizi ya huduma za kifedha. Kwa kuyumia malipo kwa njia ya simu, wateja walioko kusini mwa Jangwa la Sahara wanapata uwezo wa kupata huduma za kibenki kupitia simu za mkononi (mobile banking) pamoja na huduma zingine kama kugungua akaunti, kuchukua mkopo, kupata bima, kupata huduma za mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na masoko ya hisa. Haya yote kupitia FinTech yanawezeshwa kirahisi tuu katika simu yako ya rununu (smartphone) au laptop.

teknolojia ya huduma za fedha kwa njia ya kielektroniki (fintech)

Makala haya ya leo yamelenga wafanyabiasha kujidhatiti kidijitali kwa kutumia teknolojia za kisasa katika biashara zao za kila siku ili kuweza kunufaika vyema na masoko pamoja na fursa kede ndani na nje ya nchi. Umejifunza nini hapa katika teknolojia ya huduma za fedha kwa njia ya kielektroniki (fintech) leo?

Zaidi unaweza kupitia makala hizi hapa chini ili kupata ufahamu mpana kuhusu biashara za mtandaoni:

  1. MAGEUZI YA INTANETI (IoT) KATIKA BIASHARA NA MAISHA
  2. IJUE NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO
  3. UNAFAHAMU NINI KUHUSU BIASHARA ZA KIELEKTRONIKI (e-COMMERCE BUSINESS)?
  4. FAHAMU KUHUSU BIASHARA YA FEDHA ZA KIDIJITALI (CRYPTOCURRENCY BUSINESS)

Ukiwa na lolole, tafadhali unaweza kuwasiliana nasi kupitia comments section hapo chini;