Tag: ecommerce

mapinduzi ya viwanda

FAHAMU KUHUSU MAPINDUZI YA 4 YA VIWANDA KATIKA BIASHARA DUNIANI

Japokua ilipitwa na zama 3 tayari, lakini sasa Afrika imedhihirisha kwamba haitaki kupitwa tena katika Mapinduzi ya 4 ya viwanda Duniani. Hii ni kutokana na kukua na kuimarika katika sekta za Afya, Elimu, Biashara, Teknolojia pamoja na Mahusiano na Muingiliano wa kijamii ikichagizwa na maendeleo katika miundombinu, usafirishaji na mitandao ya kijamii. Leo tuta fahamu kuhusu Mapinduzi ya 4 ya viwanda katika biashara duniani. Ni nini na yanaashiria nini kwenye maendeleo ya biashara zingine? Makninika mpaka mwisho.

Mwezi September, 2019, jijini Cape Town Afrika Kusini ulifanyika mkutano wa kiuchumi wa WEF (World Economic Forum) ambao unazishirikisha nchi mbali mbali duniani, wafanyabiashara pamoja na wadau wa uchumi.

Mwaka huo 2019 viongozi waliokutana kujadili mustakabali wa Afrika walikua na jambo la msingi sana ambalo linatumainiwa kuleta maendeleo katika uchumi barani ambalo ni Utekelezaji wa Kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara Barani (African Continental Free Trade Area AfCFTA). Baada ya miaka mingi ya mazungumzo, makubaliano yamefikiwa ya jinsi ya kuvunja vikwazo vya kibiashara, kukuza uchumi na kuunganisha nchi ambazo katika historia zilikuwa na mahusiano mazuri ya kibiashara na bara Ulaya, Amerika na Asia. Kufahamu zaidi gusa hapa chini:

Changamoto; Afrika (wafanyabiashara, kampuni na mashirika) imejifunza nini katika Kongamano hilo la Kiuchumi (WEF)? Na zaidi, Afrika inajiandaa vipi na Mapinduzi ya 4 ya viwanda yanayoendelea duniani?

Kufikia mwaka 2018 Afrika peke yake iliripotiwa kuwa na vijana takribani milioni 200 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24. Na namba hio inatajwa kuongezeka mara mbili kufikia mwaka 2050.

Sasa “Kuwa na bara lililosheheni vijana ni fursa adhimu sana, lakini vile vile ni tishio kubwa.” alitahadharisha Albert Zeufack, Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia barani Afrika. “Ni tishio kama hatutohakikisha idadi hio ya vijana hawaanzi kufanya kazi inavyotakiwa.” Sasa kufikia Mapinduzi ya 4 ya viwanda, maeneo kadhaa yaliangaziwa na kituo cha mabadiliko ya kiuchumi barani (Africa Center for Economic Transformation, ACET) kwa niaba ya Benki ya maendeleo barani AfDB.

africa na mapinduzi ya viwanda

1. MACHINE LEARNING/ARTIFICIAL INTELLIGENCE/ROBOTICS;

Fikiria kuhusu gari inayojiendesha bila dereva na kufuata sheria na alama za barabarani ipasavyo ikijumuisha foleni. Watu wengi wangesita kupanda katika gari inayojiendesha yenyewe bila dereva, lakini hayo ndio mapinduzi halisi ya viwanda kupitia teknolojia.

Pia eneo hili limeshuhudiwa na ubunifu mwingi ukiwemo; mashine za kisasa za kuvuna na kupembua nafaka na madini, mifumo ya kiautomatiki inayoendesha ndege, meli pamoja na Teknolojia ya kupima udongo. Ni wazi mashine zinaweza kufanya kazi zifanywazo na binadamu katika zama hizi za mapinduzi ya 4 viwanda.

Swali, umejiandaeje kulinda taaluma yako dhidi ya zama hizi za mashine kujifunza (machinelearning) pamoja na teknolojia ya akili isiyo ya asili (ai)?

2. INTERNET OF THINGS (IoT);

Vifaa vingi vya kielektroniki vinavyotumiwa na mwanadamu sasa vinao uwezo wa kuingiliana na vifaa vingine kirahisi katika kurahisisha utendaji. Fikiria pale unarudi nyumbani na kuwasha feni yako kwa kutumia simu yako ya rununu (smartphone). Au kuweza kuendesha jokofu lako kwa kutumia teknolojia ya RFID. Kuunganishwa vifaa vya kielektroniki na huduma za intaneti imerahisisha sana mfumo wa mawasiliano na manunuzi ambao umeinua uchumi japo faida zake bado hazijasambaa sana barani Afrika.

Fikiria vile unaweza nunua bidhaa katika duka bila kumwona hata muuzaji. Hii inawezeshwa na teknolojia za biashara za kielektroniki (ecommerce) ambapo mteja anaweza kulipia kwa kutumia kadi yake ya benki au huduma za kifedha za simu ya mkononi kama MPESA na tigopesa. Katika bara ambalo muingiliano ni mkubwa kama Afrika, hili ni jambo la kutilia maanani sana, haswa wakati huu ambapo unajaribu ku fahamu kuhusu Mapinduzi ya 4 ya viwanda katika biashara duniani. (Ambapo sisi kama Rednet Technologies ni wadau wakubwa kuhakikisha hupitwi na huduma za kisasa kwa kutumia teknolojia).

Kufahamu mapinduzi ya IoT katika biashara na maisha kwa ujumla tayari tumekuwekea makala maalum kupitia link hii hapa MAGEUZI YA INTANETI (IoT) KATIKA BIASHARA NA MAISHA

3. DATA MINING/DATA SCIENCE TECHNOLOGIES;

Kituo cha ACET katika mwaka 2018 kiligundua kwamba “kuvua taarifa nyingi mtandaoni, kwa kutumia kompyuta zenye uwezo mkubwa na kanuni za mifumo ya Akili isiyo ya Asili (AI), huwezeshwa kupatikana kwa ripoti bora ya taarifa sahihi.” Fikiria mifumo ya tiketi za ndege, hoteli, mifumo ya kulipa kodi na taarifa za mteja wa benki.

Sekta ya Takwimu inafurahia sana ujio wa teknolojia ya Kuvua/Kuvuna Taarifa na Sayansi ya Taarifa. Jinsi ya utendaji katika teknolojia hii ni fursa adhimu sana katika kuimarisha biashara kwa kutumia takwimu sahihi zilizovunwa kutokana na taarifa mbalimbali za watu. Mifumo ya tiketi za ndege, Usajili wa vyumba vya Hoteli, taarifa za wateja wa benki na hata mfumo wa Kulipa kodi (Tax returns), hivi ni baadhi ya vyanzo vya ukusanyaji wa taarifa muhimu katika kufanya Uvunaji wa Data na Sayansi ya Data. Serikali za Africa zinamiliki kiwango kikubwa cha taarifa hizi. Je, italeta manufaa kwa Umma au itafanywa kama biashara na wajasiriamali? (Tafiti na ripoti tunazokuwekea kwenye makala zetu hizi zitakupa majibu.😋)

4. 3D PRINTING;

Ama kwa hakika mapinduzi ya viwanda yanakuja na mengi. Hebu buni bidhaa yako kwenye kompyuta halafu ichapishe kama ilivyo. Kutoka ubunifu uliotengenezwa kimchoro mpaka uhalisia katika kuchapisha tu, hii inakwenda kubadili hata namna ya uendeshwaji wa viwanda barani Africa ambapo ugunduzi huu unaleta matumaini katika uwanda wa ubunifu na ujenzi ambao unatazamiwa kuleta maendeleo katika nchi za Afrika. Viwanda vinawezaje kuendana na teknolojia hii ya Uchapishaji? Vimal Shah mkuu wa shirika la viwanda vya BIDCO nchini Kenya mwaka 2017 alinukuliwa akitania, “Tunaweza kuchapisha pizza wakati ujao.”😂

Sasa watunga sera na sheria barani walishaona uhalisia huu kama kuchapisha mfano wa kitu halisi (3D-Printing) katik mipango yao ya muda mrefu?

5. BLOCKCHAIN/TRUST TECHNOLOGIES;

Mwaka 2018 kituo cha ACET kiligundua kwenye uchunguzi wake kwamba teknolojia ya Blockchain inawafanya watu hata wasiaminiana au kujuana, kuweza kushirikiana bila ya kuwa na haja ya kwenda kwenye mamlaka za serikali. Yaani Blockchain ni jalada huru linalosajili miamala ya kifedha kati ya watu wawili au zaidi kwa usahihi na njia bora zaidi. (Tulishaelezea kuhusu Blockchain na cryptocurrencies kwenye makala zetu zilizopita). Sasa itakuaje kwa huduma za kibenki, wanasheria, wakala wa fedha (brokerage firms) na wahusika wa kiserikali katika maswala ya kifedha? Kitawakuta nini, tutajadili kwenye athari ya mapinduzi ya viwanda mbeleni.

mapinduzi ya viwanda

Si ajabu, teknolojia ya Blockchain inaonekana kama mkombozi dhidi ya vitendo vya Rushwa kutokana na undeshwaji wake ulio sahihi na wa haki. Kwa inavyoonekana teknolojia hii ya Blockchain inakwenda kuwa pigo kubwa kwa watu wenye misuli ya kiutawala, madikteta wa waendeshaji wa siasa chafu. Itakapofika siku Teknolojia hii imefikia matumizi yale yaliyonuiwa wakati inaanzishwa, basi wahafidhina na mawakala wa kifedha wa serikali na mashirika binafsi watapoteza nguvu zao. Hakutakuwa na haja ya mihuri, wala sahihi, wala zile nenda urudi kesho tukuhudumie. Blockchain itakwenda kuiweka Afrika huru dhidi ya kero za huduma za kifedha na usalama wake kuwa katika ukuaji mzuri. Haya ndio mapinduzi ya 4 ya viwanda duniani.

5. BIOPHYSICS AND BIOENGINEERING;

Eneo la 5 ambalo kituo cha ACET imeliacha ni kuhusu mtandao wa mifumo ya kibaolojia na kifizikia. Utahitaji mkono wa bandia unaoweza kuendeshwa na ubongo wako kwa usahihi ikitokea mkono wako halisi umekatika? Hebu fikiria hapo. Tunakubali kwamba asili ni bora sana kuliko sisi, hivyo ni bora kujifunza kwayo, kwasababu mapinduzi haya ya viwanda kwa kuchagizwa na ukuaji wa kiteknolojia duniani yatafanya taaluma ziweze kunyumbulika kwa namna nyingi sana hapo baadaye. Je, mifumo ya elimu imejiandaa na hili katika maandalizi ya mitaala yake ya muda mrefu?

Sasa tumeshajua yanayokuja na Mapinduzi ya 4 ya viwanda duniani. Afrika, bara ambalo ajira bado ni tatizo kubwa kwa vijana, wataweza vipi kupambana na athari za mapinduzi haya? Kuna nadharia tatu (3) katika kukabiliana na hali hii;

1. Afrika inaweza kuketi chini na kubaki kutizama dunia nzima ikipambana katika Mapinduzi haya. Hii ilishafanyika katika zama 3 zilizopita za Mapinduzi ya viwanda ambapo Mapinduzi ya Kwanza yaliegemea katika kutengeneza mifumo ya Kimekanika na matumizi ya Injini za mvuke katika kutengeneza bidhaa kama nguo.

Mapinduzi ya pili yakiwa ni kuhamasisha Uzalishaji mkubwa (mass production) wa bidhaa viwandani yakichagizwa na Henry Ford na awamu ya 3 ya mapinduzi ikiwa ni zama za kidijitali katika uzalishaji.

Ukitizama elimu ya msingi ya kuunda Injini ni ile ile iliyokuwepo tangu mwanzo, lakini bado Afrika haijaweza kutengeneza magari yake yenyewe.

2. Afrika inaweza kufanya kile ilichokifanya katika kuingia kwenye zama za Kidijitali, mtindo wa kuruka kama chura (leapfrog). Kwa mfano nchini Kenya watu hawakuwa na huduma za simu za mezani miaka ya 1990’s kurudi nyuma, hali kadhalika ilikuwa hivyo nchini Tanzania pamoja na nchi nyingi za kusini mwa jangwa la Sahara katika ku fahamu kuhusu Mapinduzi ya 4 ya viwanda katika biashara duniani.

Lakini baada ya mwaka 2000 watu wengi katika eneo hilo wameweza kumiliki simu za mkononi hata kama hawakuwahi kumiliki simu za mezani. Simu za mkononi zimekuja na teknolojia kubwa zaidi baada ya kuunganishwa na huduma za kifedha kama MPESA, huduma za internet, GPS na ramani, huduma za kiafya pamoja na biashara za kielektroniki ecommerce.

Mazingira ya Uchumi jumuishi (social economy) yanafanya iwe rahisi kukaribisha zama za Mapinduzi ya 4 ya viwanda. Watu wengi duniani hawapendi kusoma vitabu, hivyo sasa tunaweza kuziachia mashine kufanya kazi mbalimbali badala yetu. Kama Blockchain inatazamwa kwenda kuangamiza kabisa changamoto ya rushwa, Teknolojia ya 3D-Printing itafanya hata nyumba zetu kuwa viwanda vidogo katika kubuni bidhaa mbalimbali.

Taarifa zote zilizo kwenye mashirika ya Serikali na binafsi ikijumusha taasisi za dini zinaweza kuvunwa kwa ajili ya kupata takwimu mbadala katika chunguzi mbalimbali. Hii inatazamwa kuwa njia mbadala kuyafikia mapinduzi ya viwanda ya 4. Unahitaji kuLeapfrog biashara yako (kuepuka gharama kubwa za matangazo)? Tunalo suluhisho, wasiliana nasi mara moja tukupatie.

3. Vile vile, Afrika inaweza kukuza thamani ya uzalishaji na ubunifu wake ili kuwa mshindani halisi duniani katika kutengeneza na kusambaza bidhaa na huduma za kiteknolojia, kama inavyofanyika mahali kwingine duniani.

Japan imeweza kufanya hivyo katika sekta ya magari na India inafanya vizuri katika sekta ya Famasia na Programu za Kompyuta. Sasa kwanini Tanzania isiwe kinara katika Sayansi ya Data(Data Science) duniani. (maana mbongo mpe picha tuu, vingine utaona atakapovipata😂. Natania.) Sekta hizi za teknolojia zinataka matumizi ya akili zaidi, sio kama viwanda vya saruji na chuma ambavyo vinahitaji mtaji mkubwa wa kifedha.

Mfanyabiashara, umejiandaa vipi kuyapokea Mapinduzi haya ya 4 ya Viwanda katika eneo lako la biashara? Pitia makala hizi ili kupata taarifa zaidi:

  1. IFAHAMU NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO
  2. BANDO LAKO NI MTAJI
  3. FAHAMU SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA
  4. KUANZISHWA KWA ENEO HURU LA BIASHARA BARANI AFRIKA, KUNA MANUFAA GANI KWAKO?

Je umependezwa na makala yetu hii ya leo?

Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?

Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.

Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.

mapinduzi ya 4 viwanda katika biashara duniani

TEKNOLOJIA KATIKA KUKUZA BIASHARA KUPITIA SEKTA YA UTALII

Inasemekana binadamu anajua zaidi mazingira ya mwezini kuliko ajuavyo mazingira ya ndani/chini ya bahari. Sasa kampuni ya usafirishaji ya Uber tarehe 23 May 2019 ilizindua manuwari ndogo iitwayo ScUber kwa ajili ya kutalii ambapo mradi huo umeanzia jijini Queensland, Australia. Moja kati ya sababu ikiwa ni kutoa fursa kwa wageni/watalii kuweza kuzuru eneo maarufu la bahari liitwalo The Great Barrier Reef nchini humo. Sasa tunaweza vipi kutumia teknolojia katika kukuza biashara kupitia sekta ya utalii? Kumbuka Tanzania ina vivutio vingi sana vya utalii na vijana wengi wamejikita katika kuhudumia watalii hao, watumieje teknolojia kujiletea manufaa? Twende sambamba mpaka mwisho wa makala hii kufahamu zaidi.

utalii na teknolojia

Turudi Australia, manuwari hio ndogo yenye uwezo wa kubeba watu watatu kwa wakati mmoja ni ya kwanza kabisa duniani kufanya shughuli za kutalii kwa mtu yeyote anayehitaji kufanya hivyo na ambayo huduma yake inapatikana kirahisi kupitia Application ya Uber inayopatikana Playstore ya Google na Appstore ya iOS (Je, wewe ni mmoja kati ya wale waliozoea kuziona manuwari kwenye muvi na kusikia manuwari za kivita tu? 😂). Haya ni mapinduzi makubwa katika kufanya biashara kupitia nyanja nyingine ya kichumi (kutoka usafirishaji mpaka utalii).

Sekta ya utalii inatajwa kuwa ni sekta muhimu sana katika ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira duniani kote. Sekta hio inatajwa kujumuisha 8.8% ya ajira zote duniani, sawa na watu milioni 258. Vile vile 9.1% ya wastani wa pato la taifa GDP inatokea katika sekta hii ambayo ni sawa na $6 trilioni. Zaidi, 5.8% ya bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi (exports) huhusishwa na sekta hii ambayo ni takribani $1.1 trilioni. Hata hivyo, sekta hii ya utalii huchochea sana uwekezaji ambapo 4.5% ya uwekezaji wote unaofanywa duniani hupitia katika sekta hii ambayo ni sawa na $652 bilioni za kimarekani.

Tukiangazia eneo la kusini mwa jangwa la Sahara inakadiriwa kwamba ajira 3.8 milioni zikijumuisha ajira 2.4 ambazo si za moja kwa moja (indirect jobs) zinakadiriwa kutengenezwa katika miaka 10 ijayo. Hii ni kwa mujibu wa Baraza la usafiri na utalii duniani (WTTC).

Sasa changamoto; Sekta hii ya utalii inachangia vipi katik kukuza biashara barani Afrika? Teknolojia inachangia vipi katika maendeleo haya ya utalii na biashara?

Kutoka ziara za watalii 6.7 milioni mwaka 1990, nchi za ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara zilitembelewa na watalii 33.8 milioni kufikia mwaka 2012 kwa pamoja ambapo stakabadhi za wageni mwaka huo 2012 peke yake zilionyesha zaidi ya dola za kimarekani 36 bilioni zilipatikana huku mchango wa moja kwa moja ukiwa ni 2.8% katika pato la ndani la taifa GDP (Jumla ya mchango ikiwa ni mchango wa moja kwa moja na ule usio wa moja kwa moja, ilifikia 7.3% ya GDP). Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya baraza la WTTC mwaka 2013.

Lakini, ili kufanikiwa zaidi katika kufanya Utalii na kuendeleza biashara, ukanda huo wa SSA (Subsaharan Area) inabidi ujidhatiti katika mambo yafuatayo; upatikanaji wa ardhi, ruhusa ya wawekezaji katika maswala ya fedha, matangazo ya utalii, kodi za uwekezaji katika utalii, utaalamu na ujuzi katika utalii, ulinzi na usalama, maswala ya afya, mahitaji ya viza na ukiritimba. Sasa teknolojia inaleta mchango gani katika kukuza biashara kwa kupitia utalii? Kuhusu namna unavyoweza kuitangaza biashara yako katika nyanja hii ya utalii fuatana na makala hii hapa

Tuzione baadhi ya njia za kiteknolojia zinazotumika katika nyanja hio;

E-TOURISM:

Huduma za intaneti zimeleta mapinduzi makubwa sana kwenye sekta hii ya utalii ambapo watalii na wageni sasa wanaweza kupata taarifa muhimu kuhusu mahali wanapotaka kwenda kutalii kama mbuga za wanyama, bidhaa za kiasili na utamaduni, hoteli, majumba ya makumbusho na historia mbalimbali kwa kutumia vifa vyao vya kielekroniki vilivyoungwa na huduma za intaneti kama simu za rununu na kompyuta mpakato (laptop). Matokeo yake wageni na watalii wamekuwa na mahitaji makubwa kwa bidhaa za kiasili na utamaduni pamoja na kujali thamani ya pesa zao pamoja na thamani ya muda wao. Hii imerahisisha sana ufanyaji wa biashara haswa kupitia majukwaa ya ecommerce (ambayo unaweza kuyapata kwetu Rednet Technologies kirahisi sana., gusa link hii kupata huduma zetu zenye ubora Our Services🙋).

E-HOSPITALITY;

Teknolojia ya ICT imepenya mpaka katika mifumo ya huduma kwa wageni kwa haraka mno, huku ikizama katika utendaji wa hoteli, kuunda upya shughuli za masoko, kukuza huduma kwa wateja, kuimarisha huduma za kifedha, huduma za usafiri wa anga pamoja na huduma za kuwezesha ufanyaji wa biashara mtandaoni. Hii imeleta mafanikio zaidi baada ya kugunduliwa mifumo ya Computerized Reservetion Systems (CRS‘s) kuchukua nafasi ya mfumo wa zamani wa kuandikisha wageni katika mahoteli na katika vituo vya afya.

E-TRAVEL AGENCIES:

Teknolojia ya ICT imeleta maendeleo makubwa katika uendeshaji wa shughuli za taasisi mbalimbali na wakala wa kusafirisha na kutembeza wageni na watalii ambapo imeimarisha sana shughuli za ndani kama uhasibuukaguzi na rasilimali watu pamoja na shughuli za nje kama huduma kwa wateja, mifumo ya tiketi na mawasiliano ya wabia. Licha ya kuwa na 15% ya idadi yota ya watu duniani, Afrika ilikuwa ikihudumia 4% tu ya abiria wa safari za ndege duniani. Hata hivyo huduma hio ilipanda kufikia 6.5% katika kipindi cha mwaka 1998-2009 huku Carpe Verde, Msumbiji, Ethiopia na Tanzania(kabla ya kuimarishwa kwa AirTanzania) zikikuwa kwa makumi ya asilimia (WorldBank report). Maendeleo haya yanaakisi ukuaji wa matumizi ya teknolojia katika eneo hilo ambapo kumekuwepo pia na matumizi ya mifumo ya kudhibiti tiketi (OTS) na mifumo ya kuwasiliana na wateja (CRM‘s). Zaidi mifumo ya kudhibiti tiketi imekuwa muhimu katika kuratibu idadi ya wageni pamoja na kudhibiti maswala ya fedha kiteknolojia.

E-DESTINATION:

Hii ni maalum kwa waendeshaji wa Hoteli, Nyumba za wageni (Guest Houses & Lodges) pamoja na migahawa ya chakula. Sasa teknolojia imeleta mifumo mahsusi kwa ajili ya kurahisisha huduma katika kutafuta soko na kusajili wageni/watalii kirahisi wakiwa popote duniani kwa kutumia simu za rununu au kompyuta. Mfumo wa Destination Management System (DMS) umekuwa muhimu sana licha ya 10% tu ya vyumba vya hoteli 390,000 zinazopatikana katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara kuwa na hadhi ya kimataifa, huku Afrika Kusini ikishikilia nusu ya vyumba hivyo. Hata hivyo Kenya, Mauritius, Shelisheli na Tanzania zinaonyesha kuwekeza zaidi katika huduma za hoteli na teknolojia.

E-COMMERCE:

Jukwaa maarufu zaidi duniani katika kufanya biashara kwa njia ya mtandao kielektroniki. Hii ni muhimu kwa wafanyabiashara wa bidhaa za kiasili na kitamaduni kama shangavinyago na batiki ambapo sasa wanaweza kuweka bidhaa zao katika majukwaa hayo na kufikisha bidhaa zao duniani kote kirahisi zaidi, hivyo kukuza mauzo yao (Majukwaa haya ya ecommerce yanapatikana hapa Rednet Technologies, pitia tovuti yetu kwa kugusa link hii Rednet Technologies).

Kufahamu zaidi kuhusu e-commerce tafadhali fuatilia makala hii hapa kwenye link https://rednet.co.tz/unafahamu-nini-kuhusu-biashara-za-kielektroniki-e-commerce-businesses/ yenye kichwa “UNAFAHAMU NINI KUHUSU BIASHARA ZA KIELEKTRONIKI?”

Una la zaidi? Tafadhali, weka comment yako hapo chini ili tuweze share mawazo na hoja kuhusu makala haya juu ya unaweza vipi kutumia teknolojia katika kukuza biashara kupitia sekta ya utalii? Kazi kwako mfanyabiashara.

Je umependezwa na makala zetu zilizomo katika website yetu hapa?

Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?

Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) na QR CODE ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.

Tumia LIPA NAMBA kwenye picha hapa muda wote 24/7.

Kwanini uwe na website ya biashara yako?
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.

USAFIRISHAJI NA MIUNDOMBINU KATIKA USTAWI WA BIASHARA AFRIKA

Mtandao wa usafiri kwa njia ya nchi kavu barani Africa unajumuisha barabara na reli ambapo kwa wastani umechukua kilomita 6.2 kwa kila eneo la kilomita za mraba 100. Zaidi ya 60% ya mtandao mzima wa barabara haijatengenezwa kwa kiwango cha lami. Zaidi, pungufu ya 40% ya barabara za lami ndizo zilizo kwenye hali nzuri ya kupitika muda wowote. Sasa sekta hii ya usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika inatoa matumaini gani?

Mtandao wa njia za reli umeundwa kwa njia moja (single-track lines) ambazo huanzia maeneo bandarini kuelekea maeneo mbali mbali ya nchi/bara zikijumuisha viungio vichache tu njiani kuunga njia moja ya reli na nyingine (inter-linkages). Muundo huu wa reli zilizopo barani Afrika uliundwa nyakati za ukoloni na tangu wakati huo, ni marekebisho machache tu yameweza kufanyika ili kuwezesha treni ndefu zaidi zinazotumia dizeli kupita ambapo treni nyingi kati ya hizo hazitumiki tena kwa sasa.

Tukiangazia eneo la bandari, chini ya 50% tu ya matumizi ya bandari hutumika ikiwa ni pungufu ya mahitaji sahihi ya bandari hizo, jambo ambalo huchochewa na ucheleweshwaji wa mizigo na taratibu za forodha. Hali kadhalika, Afrika ndio inaongoza duniani katika ukuaji wa sekta ya viwanja vya ndege haswa kufuatia kuazishwa kwa soko huru lililoanzishwa baada ya makubaliano ya YD (Yamoussoukro Decision) yaliyofanyika mwezi November, 1999. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Afrika AU iliyotolewa mwaka 2014.

USAFIRISHAJI BARANI aFRIKA.
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.

Sasa changamoto; Je, sekta hii ya Usafirishaji na Miundombinu inaathiri vipi ukuaji wa biashara barani Africa? Na je, matumizi ya Teknolojia yana mchango gani katika kuboresha sekta hii ili kuinua biashara?

Kutokana na hali duni ya miundombinu na huduma za usafirishaji, gharama za kusafiri barani Afrika ni kati ya gharama ghali zaidi duniani, jambo ambalo linadhoofisha ushindani wa kibiashara katika masoko yote, ya ndani ya nchi na yale ya kimataifa.

Ripoti ya Tume inayoshughulikia Uchumi barani Afrika (ECA) imetaja kwamba nchi zisizo na bandari (landlocked countries) gharama za usafiri zinaweza kufikia robo tatu ya thamani ya bidhaa inayosafirishwa. Kwa mfano kusafirisha gari kutoka Japan mpaka Abijdan nchini Ivory Coast hugharimu US $1,500. Lakini kusafirisha gari hilo hilo kutoka kutoka jijini Abidjan hadi Addis Ababa hugharimu US $5,000. Kufahamu zaidi kuhusu mchango wa Teknolojia katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi kupitia link hii hapa yenye kichwa MAPINDUZI YA KITEKNOLOJIA KATIKA SEKTA YA USAFIRISHAJI NA UCHUKUZI. Ukimaliza hapo tuendelee na mada yetu ya leo.

Changamoto za Usafirishaji barani Africa.
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika.

Gharama za usafirishaji zimetajwa kusababishwa na viwango vikubwa vya forodha, tozo za ucheleweshwaji, hasara zitokanazo na ajali pamoja na ukosekanaji wa fursa. Changamoto hizi huchagizwa zaidi na uduni wa miundombinu ya kiuchukuzi pamoja na huduma zinazotokana na nyanja hiyo.

Nayo programu ya maendeleo ya miundombinu barani Afrika (PIDA) katika ripoti yake imeainisha kwamba gharama za kiuchumi zinazosababishwa na changamoto za usafirishaji katika Mtandao wa Miundombinu ya Usafirishaji barani Afrika (ARTIN) zinazidi US $170 bilioni kwa mwaka kufikia mwaka 2014.

Changamoto hizo zimetajwa kusababishwa na;

•Kutokuwa na utendaji wa taratibu za kuwezesha biashara katika majukwaa ya ARTIN (kujumuisha bandari na vituo vya mipakani).

•Sera za nyanja ya usafirishaji ambazo zinapelekea kudhoofika na kuongezeka kwa gharama za usafirshaji kwa njia ya barabara pamoja na viwango duni vya barabara katika nchi nyingi barani Afrika.

• Sera za kiuchumi zinazozuia utendaji mzuri pamoja na utanuzi wa mifumo ya reli.

• Nyanja ya usafiri wa anga na Sera za kiuchumi zinazozuia uanzishwaji wa vituo vya anga vya kikanda, jambo linalotajwa kusababisha kuongezeka kwa gharama za usafiri huo.

Kufuatia changamoto hizo, Je, teknolojia ina mchango gani katika kuimarisha biashara na kupunguza gharama za uendeshaji?

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuelekea mapinduzi ya nyanja zote za kiuchumi. (Yaani tutaendelea kuwa juu kileleni😁). Mapinduzi katika matumizi ya simu kutoka simu za mezani mpaka simu za rununu (smartphones), huduma za kifedha kielektroniki (fintech), biashara za kielectroniki (ecommerce) na kadhalika vimekuwa sehemu muhimu sana katika kurahisisha utendaji wa kibiashara katika sekta ya miundombinu na usafirishaji.

Benki ya Dunia (WorldBank) inaripoti kwamba ubunifu wa kiteknolojia umewezesha sana muingiliano wa kibiashara kwa kuzingatia ongezeko la watumiaji wa Intaneti huduma za simu. Kipimo cha wiani (density) katika matumizi ya huduma za intaneti kwa kila watu 100 waliopo eneo la Kusini mwa jangwa la Sahara, ni watu 17 tu ndio wameonekana kuwa watumiaji wa intaneti katika mwaka 2015.

website inasaidia vipi kuimarisha biashara yako?
Usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika

Utafiti huo unakolezwa wino na shirika la kimataifa linalodhibiti mawasiliano ya simu GSMA ambapo kwenye ripoti yake ya mwaka 2018 limeangazia kwamba, eneo la kusini mwa jangwa la Sahara lilikua na kasi ya kupenya kwa matumizi ya simu ya 44% kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 kukiwa na watumiaji takriban 444 milioni sawa na 9% ya watumiaji wote wa simu duniani. Vile vile katika kipindi cha mwaka 2017-2022 watumiaji wa simu katika eneo hilo wataongezeka katika kiwango cha CAGR cha 4.8% ambayo ni zaidi ya mara mbili ya kiwango cha ongezeko kwa dunia nzima katika kipindi hicho hicho. Pia kasi ya kupenya kwa matumizi ya simu inatajwa kufikia 50% kufikia mwishoni mwa 2023 na 52% mpaka mwaka 2025.

Kufuatia uchunguzi huo, sekta ya usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara barani Afrika inatajwa kuongezewa nguvu na maboresho zaidi ili kuendana na kasi hio ya ukuaji katika ICT. Matumizi ya GPS katika usafiri wa taxi yamerahisisha zaidi gharama na muda wa kutoka sehemu moja na nyingine, huku maboresho ya miundombinu kama barabara na viwanja vya ndege yakichagiza kasi ya sekta hio.

Zaidi, mtandao wa huduma za Posta na EMS unajumuisha takriban ofisi 30,000 barani ambazo ni muhimu katika kuwezesha e-commerce trade. Kwa kuliona hilo kampuni kama DHL zimejitosa kuhakikisha teknolojia inabadili huduma za posta kuwa rahisi zaidi.

Mfanyabiashara, umejiandaa vipi na jambo hili?

Je umependezwa na makala yetu hii ya leo kuhusu usafirishaji na miundombinu katika ustawi wa biashara Afrika?

Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?

Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.

Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.

USAFIRISHAJI NA MIUNDOMBINU KATIKA USTAWI WA BIASHARA AFRIKA

UNAFAHAMU NINI KUHUSU BIASHARA ZA KIELEKTRONIKI (e-commerce BUSINESSES)?

Japokuwa imechelewa, lakini kwa sasa Africa ndio inaongoza mbio katika kufanya mapinduzi ya kidijitali kuliko sehemu yoyote duniani. Namna ya kufanya biashara inazidi kubadilika ikionyesha nia ya dhati kufanya maendeleo ya kiuchumi, miundombinu na maswala ya kijamii. Mwaka 2018 nchi wanachama wa Umoja wa Africa walipiga hatua kubwa katika mfumo wa kufanya biashara na muingiliano wa kiuchumi baada ya kuanzisha Eneo Huru la Kufanyia Biashara barani (Continental Free Trade Area AfCFTA). Eneo hili lililoanzishwa linashirikisha nchi 22 zilizoweka sahihi tayari na utekelezwaji wake ulipangwa kuanza mwaka 2019 (tayari umeshaanza).

Hata hivyo mazungumzo bado yanaendelea kuweza kuzishirikisha nchi ambazo bado si wanachama wa eneo hili jipya, inatarajiwa eneo hili kufikia soko la watu takribani bilioni 1.2 barani wakiwa na jumla ya pato la ndani la taifa (GDP) la dola za kimarekani trilioni 2.5 kwa pamoja, kwa mwaka. Hii inatarajiwa kuwa ni mapinduzi makubwa zaidi kuwahi kutokea kwenye nyanja ya uchumi wa Afrika.

Sasa, swali linakuja; Afrika(wafanyabiashara, makampuni/mashirika na Serikali) imejiandaa vipi na mapinduzi haya ya uchumi wa kidijitali? Na zaidi, watunga sera/sheria wataangalia vipi biashara za kielektroniki (e-commerce) kama mada muhimu katika eneo hilo jipya la kufanya biashara huru barani?

Tume ya kudhibiti uchumi wa Africa ya Umoja wa Mataifa (ECA) ikishirikiana na Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) pamoja na Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo ya kibiashara (UNCTAD) mwaka huu 2019 imechapisha ripoti yake ikiangazia maendeleo ya Afrika kiujumla katika nyanja za kiuchumi, siasa na kijamii.

URAHISI: Imeonekana kwamba e-commerce inaweza kufanya biashara ya bidhaa na huduma kwa urahisi zaidi ambapo itarahisisha mwenendo mzuri wa biashara kati ya wazalishaji, wafanyabiashra na walaji pamoja na kumbukumbu zao na miamala ya kifedha.

MITANDAO YA KIJAMII: Pia imeonekana kwamba e-commerce inapatikana na kufanyika kirahisi katika mitandao ya kijamii kama facebook na Instagram ambapo ndipo mahali kuna watumiaji wengi zaidi wa Intaneti duniani (zaidi ya watu bilioni 2 kati ya watumiaji bilioni 4 wa intaneti).

KUTOKUWA NA MIPAKA: Mfumo wa uchumi wa Kidijitali kiasili umetengenezwa kuepuka mipaka ya kijiografia katika kufanya biashara na kubadilishana fedha ambapo mabadiliko haya ya kiteknolojia yataongeza umakini zaidi katika mwenendo wa masoko na gharama. Lakini bado wimbi kubwa la watu watakaoshiriki kwenye soko barani wanaonekana wataachwa nyuma kutokana na kutokuingiliana kwa lugha na vita/ghasia za mara kwa mara katika baadhi ya jamii/nchi.

BIASHARA: Kwa mujibu wa UNCTAD mwaka 2016 kwa dunia nzima e-commerce iliweza kupitisha mauzoya takribani dola trilioni 26 ambapo 90% ilikuwa ni Biashara kwa Biashara (B2B e-commerce) na 10% ilikuwa ni Biashara kwa Mlaji (B2C e-commerce). Hata hivyo kupima mwenendo wa e-commerce katika baadhi ya nchi zinazoendelea imekuwa ni changamoto kupata data na takwimu, haswa katika nchi za Afrika.

IMPORTATION: Takwimu za Shirika la Fedha Duniani (IMF) zinaonyesha kwamba Biashara kati ya nchi na nchi imekua kwa kiasi kikubwa Afrika ambapo zimechagizwa na vituo vichache vya kiteknolojia (Hubs) ambavyo vimerahisisha mno mwenendo wa biashara. Biashara kati y nchi na nchi (Intraregional import) imekuwa zaidi ya mara 3 katika miongo miwili iliyopita kufikia 12%- 14% sawa na dola bilioni 100 ikichagizwa na uwepo wa jumuiya za kiuchumi barani (Subregional Economic Communities REC‘s).

UZOEFU: Hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na umri wa Jumuiya hizi za Kimaendeleo barani Afrika ambapo uzoefu huo hutumika kuongeza jitihada katika kuboresha namna ya ufanyaji biashara kuelekea uchumi wa kidijitali kiteknolojia. Uzoefu huo pia hutumika kuunganisha jumuiya moja na nyingine (mf, SADC na COMESAna EAC) ambapo zitazalishwa nafasi nyingi zaidi za kufanya biashara kati ya nchi wanachama na ripoti zinaonyesha 75% ya biashara hizi ndani ya jumuiya barani Afrika zimefanyika mwaka 2017 peke yake na nusu ya biashara hizo zilifanyika katika jumuiya ya SADC.

Chini ya mwavuli wa AfCFTA nchi wanachama zinatarajia kufuta tozo/ushuru kwa 90% ya bidhaa zote zitakazopitishwa na kufanyiwa biashara katika eneo hilo. Hii itaruhusu uwezekano wa kupunguza mlolongo wa kodi au kuongeza idadi na thamani ya bidhaa na huduma zitakazohusishwa. Matokeo yoyote katika punguzo hilo linalotarajiwa katika muktadha wa biashara kidijitali yataleta picha tofauti. Kupunguza mlolongo wa tozo za mipakani baina ya nchi na nchi kutapungua kwa 15% pekee ikitegemea thamani ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi husika. Hii ni kwa mujibu wa Tume inayoshughulikia Uchumi wa Afrika kutoka Umoja wa Mataifa (UNECA) mwaka 2018.

Sasa mwaka 2018 Jumuiya ya COMESA ilibuni mfumo wa kudhibiti eneo huru la kibiashara kidijitali (Digital Free Trade Area DFTA). Mfumo huu umeundwa na mambo yafuatayo;

•E-trade: Hili ni jukwaa mahsusi kwa ajili ya kufanya biashara za kimtandao na kuwezesha malipo ya kielektroniki, mobile apps kwa ajili ya wafanyabiashara walioko katika Jumuiya hio.

•E-logistics: hili ni jukwaa maalum kwa ajili ya kuwezesha biashara ya usafirishaji wa mizigo baina ya nchi wanachama wa jumuiya.

•E-legislation: huu ni mfumo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara rasmi ambao unawawezesha kufanya miamala na malipo kielektoniki.

Mfumo huu uliobuniwa na Jumuiya ya COMESA umelenga kutangaza biashara za wanajumuiya katika nchi wanachama ikijumuisha kupitia majukwaa ya e-commerce. Mfumo huu ulikuwa ni mfanano wa mfumo uliotengenezwa na kuzinduliw na nchi ya Malaysia mwaka 2017 katika muktadha wa kufanya biashara huru ndani ya eneo maalum.

Makala haya ya leo yamelenga wafanyabiasha kujidhatiti kidijitali kwa kutumia teknolojia za kisasa katika biashara zao za kila siku ili kuweza kunufaika vyema na masoko pamoja na fursa kede ndani na nje ya nchi.

Makala hizi hapa zinarandana na somo ulilolipata leo. Zitakusaidia sana, shuka nazo:

  1. https://rednet.co.tz/fahamu-kuhusu-biashara-ya-fedha-za-kidijitali-cryptocurrency-business/ yenye kichwa “FAHAMU KUHUSU BIASHARA YA FEDHA ZA KIDIJITALI (CRYPTOCURRENCY BUSINESS)”
  2. https://rednet.co.tz/teknolojia-ya-huduma-za-fedha-kwa-njia-ya-kielektroniki-fintech/ yenye kichwa “TEKNOLOJIA YA HUDUMA ZA FEDHA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI (FINTECH)”
  3. https://rednet.co.tz/fahamu-siri-ya-kufanikiwa-katika-kuwekeza/ yenye kichwa “FAHAMU SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA”

Ukiwa na lolole, tafadhali unaweza kuwasiliana nasi kupitia;

e-mail: info@rednet.co.tz

tovuti: https://rednet.co.tz

Simu:+255765834754