Tag: bitcoin

FAHAMU KUHUSU BIASHARA YA FEDHA ZA KIDIJITALI (CRYPTOCURRENCY BUSINESS)

Waswahili wanasema “Nyakati ngumu hazidumu bali watu wagumu ndio hudumu.” Na pia “Baada ya dhoruba huja shwari.” Sasa mnamo mwaka 2008 uchumi wa dunia ulikumbwa na mtikisiko mkubwa zaidi kuwahi kutokea baada ya ule Mtikisiko wa kiuchumi wa mwaka 1933. Katika mdororo huo taasisi na mashirika ya kifedha duniani yalijikuta yakishindwa kuzuia hali duni ya uchumi katika bei za bidhaa ghafi kama mafuta na mikopo ya aina mbali mbali ambapo ilipelekea huduma hizo muhimu kupatikana eidha kwa tabu sana au kwa bei isiyokidhi usawa wa soko.

Hivyo ni katika hali hio ya mdororo wa kiuchumi ndipo lilipoibuka jina la Satoshi Nakamoto ambalo linasadikiwa kuwa ni jina la kifumbo la mtu mmoja au kikundi cha watu wasiofahamika hadharani mpaka sasa ambao ndio waliotengeneza sarafu ya kwanza kabisa ya mtandaoni na wakaiita BITCOIN. Pia mtu/watu hao ambao wanasadikiwa kuwa na asili ya Kijapani walitengeneza mfumo wa kwanza wa database ya Teknolojia ya Blockchain kwa kupitia kiunzi (ledger) cha kimtandao ambacho hakitegemei hifadhi moja. Yaani taarifa za miamala ya kifedha katika BITCOIN hufanyika kupitia Miundombinu ya Blockchain ambayo huwa ni ya siri mno na iliyotawanyika duniani kote na hivyo kuzifanya sarafu za mtandaoni zisiweze kudhibitiwa na taasisi na mashirika ya kifedha au hata vyombo vya kiserikali.

Kwanini ikawa hivi? Fuatana nasi kujua zaidi..

Kwa mujibu wa tovuti za study.com na Investopedia, Sarafu za mtandaoni au Cryptocurrency ni sarafu za kidijitali zinazoakisi thamani ya fedha ambapo kukua au kudorora kwa thamani hio hutegemea na uhitaji wa sarafu hio duniani kwa muda huo. Mfano wa sarafu hizi ni kama bitcoin, ethereum, Litecoin, Libra na kadhalika. Mpaka kufikia tarehe 20 June, 2019 BITCOIN thamani yake ilikuwa ni dola za kimarekani 9,259.37 na ETHEREUM ikapatikana kwa dola 269.11, Litecoin ikapatikana kwa dola 136.29 na kadhalika. Inakadiriwa mpaka kufikia February, 2019 tayari mtandaoni kulikuwa na sarafu 2500 tofauti tofauti za kimtandao ambapo pia iliripotiwa kuwa na miamala au mizunguko ya Bitcoin peke yake zaidi ya milioni 17.53 ambayo thamani yake inakadiriwa kuwa ni takribani dola bilioni 63.

Hata hivyo mpaka sasa soko la sarafu za mtandaoni limekua mpaka kufikia zaidi ya dola bilioni 120 huku sarafu ya Bitcoin peke yake ikichukua zaidi ya nusu ya thamani ya soko zima.

DHUMUNI LA KUANZISHWA CRYPTOCURRENCIES:

Neno Cryptocurrency ni mjumuisho wa maneno mawili, ‘Crypto’ na ‘currency’. Yaani sarafu iliyobadilishwa katika ulinzi wa kimtandao uitwao cryptography ambao huipa sarafu thamani yake ya kipekee na pia kuweza kuifanya sarafu hio isiweze kudukuliwa kirahisi.

Kutengeneza urahisi zaidi wa kulipia huduma na bidhaa mtandaoni, huduma za hoteli, migahawa, kurusha fedha kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa uhuru na wepesi zaidi na pia kubadilisha fedha katika masoko ya kimtandao ya kubadili fedha. Hizi ni baadhi ya sababu za kuanzishwa kwa sarafu hizi za mtandaoni, lakini sababu kubwa ni kuhakikisha ulinzi madhubuti na uhuru wa mtu kuhifadhi na kutumia fedha zake katika muda wowote atakaohitaji bila kufuatiliwa na taasisi au mashirika ya kifedha au vyombo vya serikali. Yaani kuwa na uhuru halisi juu ya fedha zako.

ZINAFANYAJE KAZI SARAFU HIZI?

Cryptocurrency zinafanya kazi kwa mfanano kama kadi ya benki ambayo huruhusu kufanyika miamala mbalimbali ya kutuma na kupokea fedha katika mfumo tata wa kielektroniki wa kifedha. Utofauti na utendaji wa kadi ya benki ni inaweza kufuatiliwa na taasisi za kifedha na mashirika ya kiserikali na pia huhifadhi kumbukumbu za wateja mahali pamoja.

Miamala hutumwa baina ya kompyuta washirika kwa kutumia programu ziitwazo “cryptocurrency wallets” ambapo mtu anayefanya muamala hutumia programu hio ya wallet kutuma fedha kutoka akaunti moja kwenda akaunti nyingine. Hata hivyo, ili kuweza kutuma au kupokea fedha katika mfumo huu, huna budi kuwa na nywila(password) au ufunguo binafsi ambayo inahusiana na akaunti yako. Miamala hio inayohusisha kompyuta washirika hufichwa katika msimbo wa kimtandao (encryption) halafu hutumwa katika mtandao wa sarafu hizo duniani ambapo huorodheshwa katika forodha ya jumla iliyohifadhiwa mtandaoni. Kiasi cha miamala inayopitishwa huwa ni wazi, lakini anayetuma muamala huo hufichwa, hii huitwa pseudo-anonymous ambapo ambapo kila muamala huwa na seti ya kipekee ya nywila (keys/passwords) na yeyote anayemiliki nywila hizo ndiye anayemiliki sarafu zote zilizo ndani ya akaunti hio. Kama ilivyo tuu kwamba anayemiliki akaunti ya benki ndiye anamiliki fedha zote zilizo ndani ya akaunti hio.

UNAWEZAJE KUWEKEZA KWENYE CRYPTOCURRENCY?

Sababu kuu ambayo huvutia watu wengi kuwekeza katika cryptocurrency ni kuweza kupata fedha nyingi zaidi muda mchache tuu baada ya kuwekeza mtaji. Hata hivyo kwa mujibu wa mtandao wa Forbes haya hapa chini ni baadhi ya mambo ya msingi zaidi ya kuzingatia kabla hujaamua kuweka fedha zako kama mtaji katika biashara hii:

1. AMUA AINA IPI YA CRYPTOCURRENCY UNGEPENDA KUSHUGHULIKA NAYO ZAIDI: Kama ilivyo muhimu kujua kujua kiasi cha mtaji unachokwenda kuwekeza, vile vile ni busara kuwa na mipango mizuri katika kuelewa misingi ya cryptocurrency hiyo kwa kuwa itachangia kwa kiasi kikubwa jinsi ya kujikinga na matishio yajayo ya kiuchumi.

2. AMUA UTATAKA KUWA NA UWEKEZAJI WA NAMNA GANI: Kwa kawaida utalazimika kuwa na mpango kama unataka kuingia katika masoko ya cryptocurrency. Swali ni mipango yako inaweza kuwa ya muda mrefu, wastani au ya muda mfupi. Hii itategemeana na fedha ulichonacho.

3. KUMBUKA, TAKWIMU ZA SOKO NI MUHIMU ZAIDI: Soko la sarafu za crypto ni tete muda wote. Huweza kubadilika hata kwa asilimia 20 kwa siku, hivyo ni muhimu kufuatilia taarifa za soko kwa ukaribu zaidi.

Umejifunza jambo gani kwenye makala haya? Tafadhali pitia makala tumekuwekea hapa chini ambazo zinarandana na somo ulilolipata kwenye makala hii ya leo kisha, acha maoni yako chini hapo kwenye sehemu ya comments..

  1. https://rednet.co.tz/teknolojia-ya-huduma-za-fedha-kwa-njia-ya-kielektroniki-fintech/ yenye kichwa “TEKNOLOJIA YA HUDUMA ZA FEDHA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI (FINTECH)”
  2. https://rednet.co.tz/unafahamu-nini-kuhusu-biashara-za-kielektroniki-e-commerce-businesses/ yenye kichwa “UNAFAHAMU NINI KUHUSU BIASHARA ZA KIELEKTRONIKI?”
  3. https://rednet.co.tz/fahamu-kuhusu-mapinduzi-ya-teknolojia-ya-5g-katika-biashara-na-uchumi-wa-afrika/ yenye kichwa “FAHAMU KUHUSU MAPINDUZI YA TEKNOLOJIA YA 5G KATIKA BIASHARA NA UCHUMI WA AFRIKA”
  4. https://rednet.co.tz/unawezaje-kutumia-ujasusi-katika-biashara-yako-business-intelligence/ “UNAWEZAJE KUTUMIA UJASUSI KATIKA BIASHARA YAKO (BUSINESS INTELLIGENCE)?