Tag: biashara afrika

UONGOZI vs UTAWALA KATIKA MIRADI/BIASHARA, KIPI KINAFAA ZAIDI?

“Nafikiri Kiongozi mzuri ni yule anayewafanya watu wanaomzunguka kuwa bora zaidi.” Alinukuliwa Dana Brownlee (CEO Professionalism Matters). Vipi kuhusu hali ya kuwa Mtawala, inaathiri vipi biashara?

Tunafahamu ilivyo, ukiwa mjasiriamali/mfanyabiashara huna budi kuvaa kofia nyingi, majukumu kila kona. Ukiwa mfanyabiashara jua unawajibika kujenga na kuimarisha masoko yako, kubuni/kusimamia miradi, kutunza hesabu nakadhalika.

Hata hivyo biashara inavyozidi kukua, vitu vya kusimamia pia vinaongezeka, hivyo mfanyabiashara/mjasiriamali makini lazima aanze kufikiria namna ya kuendesha biashara yake kwa urahisi bila kuathiri shughuli za kila siku. Unahitaji msaada kutoka kwa watu wengine. Wakati huu sasa ndipo anahitajika Kiongozi zaidi kuliko Mtawala, hasa katika biashara.

KIONGOZI ANA SIFA ZIPI?

i. ANAFANYA KAZI NA TIMU YAKE: Ukiwa Kiongozi hili ni jukumu muhimu sana. Usiishie tu kutoa amri na maagizo, hapo utakuwa Mtawala, tena asiyefaa. Kiongozi anafanya kazi bega kwa bega na timu yake, kila anapohitajika kuweka mchango wake anafanya hivyo. Katika biashara za kisasa hii ina maana Kusaidia hatua za uzalishaji zizidi kuwa bora, kuboresha maudhui ya mtandaoni ya kampuni, kuhamasisha viwango katika kazi, kuongea na wateja ili kuboresha huduma. Kiongozi anaelewa vyema watu wote anaofanya nao kazi na wateja anaowahudumia, muda wote yupo updated. Njia bora zaidi ya kuwasiliana na kujua tabia na mwenendo wa watendaji katika timu pamoja na mwenendo wa wateja ni kupitia mitandao ya kijamii. Sasa mitandao ina mchango gani, tafadhali pitia makala yako hii kwenye link https://rednet.co.tz/ifahamu-nguvu-ya-mitandao-ya-kijamii-katika-biashara-yako/ yenye kichwa “IJUE NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO”

ii. KIONGOZI BORA NI MNYENYEKEVU: Hakuna mtu anapenda kufanya kazi na mtu mwenye kiburi, majivuno au mjuaji sana. Hata hivyo inafaa sana kwa Kiongozi kutambua pale anapokosea na kujisahihisha mara moja, vile vile Kiongozi huruhusu timu yake kutambua makosa yao na kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali kwa kadiri zinavyotokea. Unyenyekevu (Being Humble) husaidia kuimarisha morali ya ufanyaji kazi katika miradi/biashara kuliko kiburi na majivuno.

iii. MAWASILIANO WAZI: Katika vitu muhimu vya kufanya katika kufanya biashara/mradi kwa mafanikio ni namna timu inawasiliana kwa uwazi. Kila mtu anayefanya kazi katika timu hujihisi ana umuhimu pale anapokuwa na taarifa kamili kuhusu mambo yote yanayoendelea ndani ya timu yake na pale anapoweza kuwasiliana na yeyote ndani ya timu na kujuzwa mambo kwa uwazi. Unapokuwa na jukumu la kuhudumu ndani ya timu ni muhimu kuwa straight-forward kwa kuwa biashara/kampuni yako ni taswira yako mwenyewe kama Kiongozi. Hivyo, unapokuwa muwazi katika mawasiliano pamoja na kuzingatia maadili ya kiweledi (ethical behaviors) katika utendaji wa shughuli za kila siku, timu nzima unayoiongoza itafuata taswira hio.

iv. KUWA MSIKIVU: Kama Kiongozi ni jukumu lako kusikikiza kwa umakini mara zote mwingine anapozungumza iwe katika timu ama mteja. Usikivu humpa mzungumzaji nafasi ya kusema kile anadhani kinafaa katika kuboresha shughuli za kibiashara/kimradi ambazo ni muhimu sana katika ukuaji wa kampuni/biashara. Usikivu humfanya mzungumzaji kuungana moja kwa moja na wewe kama kiongozi katika kuimarisha mradi/biashara.

Usikivu pia huimarisha Mvuto (impression) wako katika macho na akili za watu ulionao katika mazungumzo. Tafiti zinaonyesha mzungumzaji husema kile kilichopo moyoni mwake kuhusu vile anataka kuhudumiwa au kutoa wazo la kuimarisha biashara pale anaposikilizwa kwa umakini.

v. KUWA NA MTAZAMO CHANYA: Katika kufanya shughuli za kila siku za mradi/biashara, changamoto hazikosekani. Iwe ni changamoto ndogo au kubwa, kama Kiongozi jinsi unavyoshughulika na mazingira hasi katika mradi/biashara yako hutafsiri mengi kuhusu maarifa ya kiuongozi uliyonayo. Robert Mann (mwandishi ya kitabu The Measure of a Leader) ananukuliwa “Look at three positive things about a problem before you identify what makes it dissatisfying. The more you look at the positives in a problem, the more positive people react with one another.”

Katika utafiti wake bwana Mann aligundua kuwa baada ya watu kuona mambo mazuri katika mazingira yenye changamoto, hufikiria namna ya kukabiliana na changamoto hio ili kufikia lile jambo lenye faida. Sawa sawa na vile jinsi Kiongozi anavyotaka kuimarisha mbinu za kiutendaji.

vi. FAHAMU BIASHARA/MRADI WAKO: Njia bora ya kufahamu kitu unachokifanya ni kwa kutumia uchambuzi wa SWOT ambao unakusaidia kufahamu Strength (nguvu/faida ya biashara), Weaknesses(Udhaifu wa mradi/biashara), Opportunities (fursa zinazokuja na biashara hio) pamoja na Threats(matishio yanayoikabili biashara). Kwenye kufanya uchambuzi huu zingatia haya;

STRENGTH (Nguvu/Faida ya biashara/mradi wako): Unaweza kuboresha jambo gani zaidi ya washindani wako? Uongeze malighafi/huduma gani ambazo washindani wako bado hawana? Mteja wako anafuraha?

•WEAKNESSES(Madhaifu ya mradi/biashara): Ni malighafi/huduma gani ambazo washindani wako wanazo ila wewe bado huna? Ni kipi unahitaji kuimarisha katika mradi/biashara yako? Una uzoefu wa kutosha kushindana na wafanyabiashara wengine? Unafanyaje baada ya hapo?

OPPORTUNITIES (Fursa): Unaona fursa gani katika mradi/biashara yako? Sheria za nchi, unaweza vipi kuzitumia vizuri katika kuimarisha mradi/biashara yako? Nje ya biashara/mradi wako kuna jambo/trend gani maarufu linaendelea? Unaweza vipi kulitumia jambo hilo kwa faida yako?

Je, kuna matamasha, matukio ya kijamii katika kalenda yako hivi karibuni? Unaweza vipi kuyatumia matukio hayo kwa faida ya biashara/mradi wako?

•THREATS (Matishio yanayoweza kuikumba biashara/mradi wako): Una changamoto za kifedha? Biashara/mradi wako utajiendesha vipi? Je vyanzo vyako vya kifedha ni vya kuaminika na kutegemeka (reliability)? Biashara/mradi wako unaweza kuhimili maendeleo ya kiteknolojia yanayozidi kushika kasi duniani? Kuna mambo gani binafsi yanayoweza kuathiri biashara/mradi wako? Katika timu yako, kuna mtu anapitia wakati mgumu katika kukabiliana na mambo binafsi kama msiba, ugonjwa au harusi?

Hayo ni baadhi ya maswali ambayo unaweza kujiuliza wewe kama kiongozi pamoja na timu yako ili uweze kuifahamu biashara yako na mazingira inayopitia ili kutengeneza njia nzuri zaidi ya kufanikiwa.

MTAWALA ANAATHIRI VIPI BIASHARA/MRADI?

Mazingira ya biashara/mradi ni sehemu inayohitaji mahusiano mazuri zaidi ili kuhakikisha biashara inakuwa na kudumu kwa miaka mingi zaidi. Lakini unapoingiza Utawala unaingiza ile hali ya kuhitaji zaidi na kuweka mbele matakwa binafsi.

•Mtawala anatoa amri na maagizo pasi na kuangalia hali ya utendaji ya timu yake.

•Si mara zote mtawala anakuwa muwazi kwa timu yake. Jambo linalohatarisha utendaji bora wa timu.

•Kiburi na majivuno humfanya kiongozi bora kuwa mtawala dhalimu ambaye hahitajiki katika biashara.

Hizo ni baadhi ya athari za Uongozi na Utawala katika maendeleo ya Biashara/Miradi. Je unaweza vipi kuyafanya haya katika Mradi/Biashara yako? Makala zifuatazo katika link ni muendelezo mzuri wa somo ulilolipata katika makala hii ya leo. TUJADILI..

 1. https://rednet.co.tz/fanya-maamuzi-sahihi-katika-muda-sahihi/ yenye kichwa “FANYA MAAMUZI SAHIHI KATIKA MUDA SAHIHI
 2. https://rednet.co.tz/ukweli-kuhusu-propaganda/ yenye kichwa “UKWELI KUHUSU PROPAGANDA
 3. https://rednet.co.tz/kwanini-uitangaze-biashara-yako/ yenye kichwa “KWANINI UITANGAZE BIASHARA YAKO?
CHANGAMOTO KATIKA BIASHARA MPYA/INAYOANZA, FUNZO LISILOEPUKIKA.

CHANGAMOTO KATIKA BIASHARA MPYA/INAYOANZA, FUNZO LISILOEPUKIKA.

Bila shaka umeshasikia misemo kama ‘survival for the fittest’ ama ‘Bahari tulivu haizalishi nahodha hodari’, wengine wanakwambia “Mwanzo mgumu”. Sasa kwenye biashara, mambo yapo hivyo hivyo, changamoto haziepukiki. Sasa leo tuazione changamoto katika biashara mpya/inayoanza, hili ni funzo lisiloepukika kabisa. Twende sambamba.

Leo hii, duniani kunaripotiwa kuwapo takriban kampuni/biashara 150 milioni zinazoanza (startups), huku kukiwa na ongezeko la kampuni hizo milioni 50 kila mwaka. Kwa wastani kuna kampuni zinazoanza 137,000 zinaanzishwa kila siku. Hebu niambie, umeshaanzisha biashara ngapi hadi leo? ngapi zimeshakufa? tuambie kwenye comments pale chini.

Lakini swali la msingi ni je, hizi kampuni zinazoanza, zinaweza vipi kuhimili mawimbi makali ya changamoto zilizopo katika ulimwengu wa biashara duniani, haswa eneo la Kusini mwa jangwa la Sahara (ambalo linatajwa kuwa na changamoto nyingi zaidi za kibiashara).

Takwimu zinaonyesha kuwa 80% ya biashara/kampuni zinazoanza hufa ndani ya mwaka wa kwanza tu tangu kuanzishwa kwake. Na katika hizo 20% zilizobaki 10% hufa ndani ya miaka mitano tangu kuanzishwa. Tatizo ni nini? Wafanyabiashara hawa wanakosea wapi? Ni changamoto gani hizo ambazo pengine wafanyabiashara/waanzilisi wa kampuni hizo hawakuwa wanazijua mpaka zinapelekea biashara/kampuni zao kufa kabla hazijafikia ndoto na malengo yale makubwa ambayo waanzilishi walijiwekea mwanzoni.

Sasa leo tuzione changamoto hizo za biashara mpya/inayoanza ili tukomboe biashara tunazopanga kuanzisha;

1. USHINDANI MKALI

Hakuna wakati katika historia ya mwanadamu biashara zimekuwa zikifanyikwa kwa ushindani kama sasa. Yaani usitegemee kuanzisha biashara ambayo haina ushindani. Pia ni ngumu sana kuanzisha biashara ambayo haijawahi kufanyika kabisa hapo kabla. Hivyo jipange.

Ujio wa matumizi ya intaneti umeongeza sana hali ya ushindani ambapo kwa sasa masoko hutafutwa kwa njia za kidijitali zaidi. Biashara zinahamia mtandaoni na hivyo huna budi kuhakikisha unatafuta wateja kwa nguvu sana kwa njia za Digital marketing, social media marketing, affiliate marketing na nyingine nyingi ili kuhakikisha biashara yako inaendelea kupata wateja wapya na kuwafikia wale ulio nao kirahisi zaidi.

Lakini njia rahisi (japo sio nyepesi) ya kuepuka ushindani sokoni ni kuwa MKIRITIMBA (Being a Monopoly). Hii ni ile hali ya kucontrol soko na kukamata wateja wengi kiasi kwamba washindani wako hawana nguvu ya kupambana na wewe sokoni. Zaidi kuhusu ukiritimba fuatilia makala hii hapa

2. WATU SAHIHI

Waswahili wanasema, Biashara ni watu. Hii haiishii kwa watu kwa maana ya wateja peke yake, watu hawa haswa wanangukia kwenye wabia, wafanyakazi na washauri wako katika biashara. Hawa wana mchango mkubwa na muhimu sana katika kuua au kuendeleza biashara yako.

Hii Rednet ni mfano sahihi katika sehemu hii kwa kuwa mwanzoni Rednet Technologies ilihisusha watu 6. Lakini kutokana na kutoshare vision na sababu zingine, Rednet haikuweza kushamiri katika mwaka wake wa kwanza mpaka tulipoamua kupunguza watu mpaka kupata watu sahihi wa kufanya nao kazi kwa maslahi mapana ya kampuni. Unapoamua kuanzisha biashara/kampuni mpya hakikisha unazungukwa na watu sahihi watakaoimarisha zaidi biashara/kampuni hio. Wahenga wanasema “Ndege wanye manyoya yanayofanana, ndio wanaoruka pamoja”. Take that note.

3. MASWALA YA FEDHA

Moja kati ya vitu vinaua biashara/kampuni nyingi ni Kutokujua kutofautisha maswala ya fedha ya kampuni na yale binafsi. Elewa, ukishaingiza pesa kwenye biashara/kampuni, pesa hio sio Binafsi tena. Inatakiwa izunguke mpaka itoe return/faida ambayo ndio inaweza kutumika kwa matumizi binafsi. Hii ni changamoto kubwa na inayohitaji umakini mkubwa ili kuihimili. Lile gepu la masikini na tajiri kwa kiasi kikubwa huwa linapigwa kutokana na uwezo wa kupambana na changamoto hii.

changamoto katika biashara mpya

4. UFINYU WA RASILIMALI

Miongo michache iliyopita kuanzisha biashara/kampuni mpya ilimlazimu mtu kuwa na mtaji mkubwa ama kuwa na uwezo wa kufanya harambee ya kukuza mfuko wa uwekezaji. Kwa wakati huo mawazo mengi yalishindwa kuwa biashara/kampuni zenye tija.

Lakini leo hii kunakadiriwa kuanzishwa takribani biashara mpya 137,000 kila siku duniani kote. Hii ni kutokana na kukua kwa kasi ya teknolojia katika shughuli za kibiashara ambayo imerahisisha sana upatikanaji wa rasilimali. Lakini swala la maarifa ghafi (softskills) bado limekuwa ni changamoto katika uendeshaji wa biashara nyingi ambapo licha ya kuwa na wazo zuri ama mtaji wa kifedha, bado kuwa na maarifa ya kuendesha biashara/kampuni inabaki kuwa ni changamoto. Hivyo ukitoa Wazo, Vifaa vya kufanyia kazi na Pesa ya uwezeshaji, Maarifa ni rasilimali muhimu zaidi.

5. UWEZO WA KUTOA MAAMUZI SAHIHI

Katika kuanzisha biashara/kampuni mpya, moja kati ya Changamoto kubwa zinazowakabili waanzilishi ni Uwezo wa Kutoa maamuzi sahihi kulingana na wakati na hatua biashara/kampuni inayopitia. Moja kati ya changamoto zinazosumbua sana katika biashara.

Ukiwa mfanyabiashara/mbia wa kampuni unalazimika kufanya maamuzi mengi kila siku. Katika maamuzi hayo utajikuta wakati mwingine unafanya makosa kutokana na maamuzi yako, na pengine maamhzi hayo yanaweza kukukatisha tamaa na hata kuua biashara/kampuni yako ndani ya muda mchache.

Usiogope. Hakikisha unajifunza katika kila maamuzi unayochukua hata kama hayakuleta madhara katika biashara/kampuni yako. Wahenga wanasema “Busara hujengwa katika maamuzi”. Note hio, halafu ifanyie kazi kila siku. Kulifahamu hili kwa undani fuatana na makala hii hapa..

6. KUPATA UAMINIFU WA WATEJA

Hebu niambie, ilikuchukua muda gani kupata mteja wako wa kwanza tangu ulipoanzisha biashara/kampuni yako? Cocacola ilichukua mwaka mzima kuuza chupa moja ya soda katika mwaka wake wa kwanza tangu kuanzishwa.

Rednet ilichukua miezi 8 mpaka kumpata mteja wetu wa kwanza tangu tulipoanza shughuli zetu hapo mwaka 2016. Ni wakati mgumu sana katika biashara, lakini wahenga wanasema “Mteja ni mfalme.” Hivyo kupata mfalme wa kuhudumia kwa vyovyote si rahisi. Siku zote kizuri kinajiuza chenyewe ambapo huduma nzuri huvuta wateja zaidi kwa kutumia mbinu ya “Word of mouth”. Mbinu hii huzalisha wateja wa kudumu zaidi ambao huwa mabalozi wazuri wa biashara/kampuni yako. Jinsi ya utendaji katika biashara yako lazima ijengwe kumzunguka na kuridhisha wateja wako. Mteja asiporidhika, bado hujafanikiwa kibiashara. Zaidi tiririka na makala hii hapa kwa ajili yako..

7. USALAMA WA KIMTANDAO

Wakati huu tunaoishi ni wakati wa Kidijitali. Biashara/kampuni nyingi zinazoanzishwa zama hizi hufanyia shughuli zake mtandaoni, hivyo miundombinu ya utendaji katika biashara za kisasa kwa zaidi ya 75% hutegemea Nguvu ya mtandao.

Hata hivyo, Wadukuzi wa kimtandao wanafanya mazingira ya kiutendaji mtandaoni kuwa magumu na yenye kuhofisha. Matukio ya udukuzi na uhalifu wa kimtandao yanazidi kuongezeka kila uchwao. Tafiti zinaonyesha kufukia mwaka 2021 matukio ya uhalifu wa kimtandao yatakuwa yakitokea kila baada ya sekunde 11 duniani kote. Ili kujilinda dhidi ya uhalifu huu wa kimtandao, biashara zinazoanza hazina budi kuwa na miundombinu ya kimtandao ambayo ni imara zaidi kila wakati.

Zaidi kuhusu Usalama wa kimtandao unaweza kupata makala yetu mahsusi kupitia link hii https://rednet.co.tz/kwanini-usalama-wa-kimtandao-cyber-security-ni-muhimu-kwako/ yenye kichwa “KWANINI USALAMA WA KIMTANDAO (CYBER SECURITY) NI MUHIMU KWAKO?”

Kifupi hizo ni changamoto chache ambazo zinazikabili biashara/kampuni inazoanza, ni funzo lisiloepukika kweli kweli. Je, wewe umepitia changamoto zipi wakati unaanzisha hio biashara yako uliyo nayo? Umeshajaribu kufanya biashara ngapi bila mafanikio mpaka kufikia sasa? Tafadhali tushirikishe ili watu wengine wapate kujifunza zaidi. Karibu.

Pia hakikisha unapitia makala hizi tumekuwekea hapa chini ili kuhakikisha unapata muendelezo mzuri kutokana na somo ulilolipata kwenye makala ya leo. Gusa link kisha makinika..

 1. https://rednet.co.tz/kwanini-uitangaze-biashara-yako/ yenye kichwa “KWANINI UITANGAZE BIASHARA YAKO?
 2. https://rednet.co.tz/biashara-yako-inaweza-vipi-kuwa-taasisi-imara/ yenye kichwa “BIASHARA YAKO INAWEZA VIPI KUWA TAASISI IMARA?
 3. https://rednet.co.tz/website-inasaidia-vipi-kuimarisha-biashara-yako/ yenye kichwa “WEBSITE INASAIDIA VIPI KUIMARISHA BIASHARA
 4. https://rednet.co.tz/ifahamu-nguvu-ya-mitandao-ya-kijamii/ yenye kichwa “IJUE NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO

Ni matumaini yangu leo umefahamu kwa undani changamoto katika biashara mpya/inayoanza, funzo lisiloepukika. Utakwenda kukabiliana nazo vipi changamoto hizi za leo? Niambie kwenye comment hapo chini..

Je umependezwa na makala yetu hii ya leo?

Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?

Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu(website design, logo design, Digital consultacy n.k) BILA MAKATO ya miamala.

Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.

Kwanini uwe na website ya biashara yako?

UKIRITIMBA KATIKA BIASHARA, NI ASALI AU SHUBIRI?

Mara nyingi hutokea biashara ndogo hazina rasilimali nyingi kama washindani wao ambao ni Makampuni makubwa. Ile hali ya Biashara kuwa na ushindani mdogo/kutokuwa na ushindani kabisa ndio inaitwa ukiritimba (business monopoly).

Katika dunia hii ya leo ambayo inatawaliwa na sera za kibepari katika nchi nyingi, kitu kinachozingatiwa zaidi ni kuhakikisha FAIDA inazidi kuingia kila siku bila kuchoka wala kujali washindani wako watakuwa kwenye hali gani. Kibinadamu saa ingine hii inawezekana haijakaa sawa, lakini ndio UBEPARI wenyewe huo katika ubora wake. Katika mfumo huu wa maisha, biashara huonekana imefanikiwa pale inapofikia hatua inakuwa na Ukiritimba wa kutosha katika masoko ya Bidhaa/Huduma zake. Kimsingi Ukiritimba sio dhambi, wala sio kosa kisheria. Ni ile jinsi bishara inaweza kutawala soko la bidhaa/huduma fulani katika jamii. Kuna ubaya gani hapo? Mfano kundi la WCB Wasafi kinavyotawala muziki nchini Tanzania. Sio kwamba hakuna ushindani kutoka kwa wasanii wengine, bali kundi hilo limeweza kutengeneza Ukiritimba sokoni na kufaidika zaidi kuliko kundi lingine lolote katika muziki nchini humo.

Kwenye siasa pia kuna Ukiritimba mwingi sana, hasa katika siasa za Afrika ambapo zimekuwa zikitawaliwa katika mifumo ya Kiimla, Utawala wa chama kimoja kwa muda mrefu (mfano CCM nchini Tanzania, kule Rwanda, Mali n.k). Hizi siasa za ukiritimba zimekuwa Asali na Shubiri vilevile katika nchi husika.

Kuhusu Ukiritimba katika siasa za Afrika tutaliona jambo hilo wakati mwingine. Leo twende na Ukiritimba katika Uchumi na Biashara kwanza.

UKIRITIMBA UNATENGENEZWA VIPI?

1. SERA ZA KISERIKALI: Mara nyingi serikali hujaribu kuzuia ukiritimba katika biashara mbalimbali. Lakini, wakati mwingine serikali hio hio huhamasisha sera za ukiritimba au kuutengeneza ukiritimba wenyewe katika baadhi ya mashirika. Mfano Shirika la Ugavi wa umeme (Tanesco) limefanywa kuwa mtoa huduma ya umeme pekee nchini na kutoruhusu mtoa huduma mwingine aingie sokoni.

Pia hapo kabla ya mwaka 2015 barabara ya morogoro jijini Dar es salaam ilikua na daladala nyingi kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali, jambo lililokuwa likitengeneza ushindani mkali katika sekta ya usafiri. Lakini baada ya kuzinduliwa kwa mradi wa mabasi ya Mwendokasi ushindani wa kibiashara katika sekta ya usafiri kupitia barabara ya morogoro umekuwa mdogo sana kiasi kwamba shirika la UDA(serikali) na lile la DART(binafsi) ndio pekee wameungana kulishika soko la usafiri katika barabara hio na hivyo kutengeneza Ukiritimba wa aina yake hapo.

Kwingine ni katika sekta ya madini ambapo sasa Mnunuzi pekee wa madini yanayochimbwa nchini na wachimbaji wadogo ni Serikali. Yaani serikali sasa imechukua dhamana ya kununua madini yote yanayochimbwa kabla hayajauzwa kwa wafanyabiashara wengine nje na ndani ya nchi.

Hii ni kwa mujibu wa sheria ya madini iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2018, 2019 (sikumbuki vizuri mwaka). Hapa nadhani wote mlimuona Bwana Laizer akivuta Hundi yake pale BoT baada ya kuuza mawe yake kupitia Wizara ya Madini. Kwa upande huu unauonaje ukiritimba, asali au shubiri?

2. KUSHUSHA BEI: Bila shaka utakubaliana nami kuwa kama unataka kuuza bidhaa/huduma zako kwa wingi na kuliteka soko, huna budi kushusha bei. Watoto wa mjini wanakwambia, Biashara nzuri na yenye mafanikio hufanyika Uswahilini. Kule ambapo barafu linauzwa 50/-, ice-cream 100/-, Muhogo 100/-, nguo za mitumba 3000/-. Huko ndiko biashara zinapofanyika haswa. Angalia ice-cream za Ukwaju kutoka kwa Bakhresa zinavyouzika halafu linganisha na zile zinazouzwa kwenye maduka ya mlimani city. Au tizama nguo za mtumba zinavyouzika pale Mwenge na Karume halafu linganisha na nguo zinazouzwa kwenye maduka makubwa pale Kinondoni na Tegeta. Utakuja kugundua kuwa Mlimani City, Kinondoni na Tegeta bidhaa zinauzwa lakini si kwa kasi kama zinavyouzika Mwenge, karume na Manzese. Hii ni kwa kuwa punguzo la bei linatengeneza ukiritimba wake hapo.

3. MATUMIZI YA HATIMILIKI: Hii hufanyika kwa msaada wa serikali ambayo ina jukumu la kuunda sheria za kulinda na kudhibiti hatimiliki ambayo humpa mwenye nayo uwezo wa kutumia vizuri Mawazo yake, Ubunifu, Wimbo na Mipango. Mfano wa jambo hili unatoka katika uwanda wa teknolojia ambapo shirika la Microsoft (MSFT) ambalo hutumia hatimiliki za mfumo tendaji wake wa Microsoft Windows kutengeneza ukiritimba katika mifumo tendaji ya kompyuta inayotumia duniani kwa sasa.

Hatimiliki hio inawapa Microsoft haki ya kurekebisha na kuimarisha mifumo tendaji yake ili iendane na matakwa ya wateja wao na hivyo kuweza kutawala soko la mifumo tendaji duniani. Niambie, wewe umeshakutana na watu wangapi ambao kompyuta zao hazitumii microsoft windows? Bila shaka ni wachache sana au hakuna kabisa. Ndio ukiritimba wenyewe huo sasa.

4. KUMILIKI RASILIMALI ADIMU: Moja kati ya njia bora zaidi za kutengeneza Ukiritimba (monopoly) katika masoko ya kibiashara ni hii. Nchini marekani shirika la Standard Oil chini ya uongozi wa John D. Rockefeller ambaye alikua ni kiongozi mwenye maono na bidii, aliweza kumiliki 90% ya njia zote za mafuta (oil pipelines and refeneries) katika nchi nzima ya Marekani. Baada ya kutawala soko la mafuta kwa muda mrefu, serikali ilianza kumpiga vita jamaa na kujaribu kumpokonya sehemu ya umiliki wa soko ambapo ilichukua miaka takribani 20 mpaka ukiritimba wa Kampuni hio ulipopungukiwa nguvu.

Makampuni kama Chevron Corporation (CVX), Exxon Mobil Corp (XOM) na ConocoPhillips Co. (COP) ni kampuni zilizozaliwa baada ya kufa kwa ukiritimba wa Standard Oil ya bwana John D. Rockefeller. (Chanzo mtandao wa Investopedia).

Sasa wewe unamiliki bidhaa/huduma gani ambayo unahisi ni adimu kweli kweli? Ukiijua hio itumie kutengeneza mtandao ukiritimba wa kutosha katika biashara zako.

KWANINI UKIRITIMBA UNATENGENEZWA?

Kama tulivyoeleza hapo mwanzo, mara nyingi serikali hupiga vita swala la ukiritimba lakini serikali hio hio huhamasisha uundwaji wa ukiritimba katika baadhi ya sekta sababu chache zifuatazo:

i. MSAWAZO WA KIUCHUMI: kuhakikisha Uchumi unakuwa katika viwango sawa sawa kutoka sehemu zote (economies of scale) ambapo lengo kuu ni kuwanufaisha wananchi kwa kuhakikisha gharama zinakuwa chini katika huduma za msingi za kijamii kama umeme, maji na usafiri.

Ndio maana unaona mashirika yanayotoa huduma za umeme na Maji (mfano DAWASCO na TANESCO) yanaendelea kuhodhiwa na serikali ili kuhakikisha yanatoa huduma stahiki kwa wanachi. Hebu waza siku kutokee kampuni 10 zinazotoa huduma ya usambazaji wa umeme ambayo kila moja itatakiwa kusambaza nguzo zake na miundombinu yake ya utoaji huduma pamoja na kufanya huduma za marekebisho kila inapohitajika. Huo usumbufu wake utakuaje huko mtaani? Hivyo ndivyo imefanya kuwe na mtoa huduma mmoja tu katika sekta hio ya nishati pamoja na zingine za maji na kadhalika.

ii. KUHAMASISHA UBUNIFU: Hii ni sababu muhimu kwanini ukiritimba unahamasishwa. Sera za Serikali kuhusu Hakimiliki zimeundwa ili kuhakikisha wabunifu na wasanii wanalida kazi zao na kufaidi matunda ya ubunifu wao vile inavyostahili. Kama wabunifu hao wasingekuwa na hakimiliki basi bila shaka juhudi zao, muda wa kujitolea pamoja na sadaka zingine ambazo wamezitoa katika kazi na biashara zao zingekuwa ni kazi bure. Hii ndio maana serikali imeweka sheria kusimamia hatimiliki za wabunifu katika sekta mbalimbali rasmi na zile zisizokuwa rasmi.

Hio ndio Ukiritimba katika Biashara za barani Afrika haswa kusini mwa jangwa la Sahara. Una lolote la kuongezea? Tafadhali tujulishe. Pia hakikisha unapitia makala zetu zingine hizi hapa tumekuwekea ili kuhakikisha unapata muendelezo mzuri wa somo ulilolipata leo. Gusa link kisha makinika:

 1. https://rednet.co.tz/fahamu-siri-ya-kufanikiwa-katika-kuwekeza/ yenye kichwa “FAHAMU SIRI YA KUFANIKIWA KATIKA KUWEKEZA”
 2. https://rednet.co.tz/kwanini-uitangaze-biashara-yako/ yenye kichwa “KWANINI UITANGAZE BIASHARA YAKO?
 3. https://rednet.co.tz/ifahamu-nguvu-ya-mitandao-ya-kijamii/ yenye kichwa “IJUE NGUVU YA MITANDAO YA KIJAMII KATIKA BIASHARA YAKO
 4. https://rednet.co.tz/ifahamu-aina-mpya-ya-udalali-wa-mtandaoni-dropshipping/ yenye kichwa “IFAHAMU AINA MPYA YA UDALALI WA MTANDAONI (DROPSHIPPING)