D.R.C NDANI YA E.A.C, MFANYABIASHARA ANAFAIDIKA VIPI?
Hatimaye tar29 March Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ilipata kibali cha kuwa mwanajumuiya wa Afrika Mashariki (EAC) na mwezi July mwaka huo 2022 DRC iliingia rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuwasilisha matakwa yote makao makuu ya jumuiya hio jijini Arusha. Hii ni baada ya kuendesha mchakato uliodumu kwa takriban miaka minne. Sasa DRC inapoingia ndani ya EAC mfanyabiashara anafaidika vipi?
DRC inakuwa mwanachama namba 7 wa EAC huku ikiwa ndio nchi kubwa zaidi kijiografia katika ukanda huo. Inasemekana DRC ndio nchi yenye rasilimali (madini, mafuta, misitu n.k) nyingi zaidi duniani. Pia nchi hio ina idadi ya watu takribani milioni 90 ambao ni mtaji muhimu kiuchumi.
MAMBO 10 USIYOYAJUA KUHUSU D.R.C:
Kukubalika kwa DRC kunamaanisha kwamba soko la Afrika Mashariki linatanuka na kuwafikia watu zaidi ya milioni 300 waishio ndani ya jumuiya hio tu, huku uchumi wa jumla ukiwa na thamani ya 250$ bilioni. Sasa DRC ina nini cha ziada usichokijua?
1. MIPAKA YA KIJIOGRAFIA:
Ikiwa ndio nchi ya pili kwa ukubwa wa jiografia barani, DRC inapakana na nchi zingine 9. Nchi hizo ni Angola, Burundi, Jumhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Jamhuri ya Congo (Brazaville), Sudani Kusini, Uganda, Zambia na Tanzania. Muingiliano wa kibiashara ni mkubwa sana hapa.
Zaidi upande wa magharibi mwa jiji la Kinshasha inapakana na bahari ya Atlantiki. Sasa Kongo kupakana na nchi 9 na kuwa na ufukwe wa bahari ya Atlantiki kunaifanya iweze kutanua fursa kwa wafanyabiashara kupitisha mali kwenda nchi nyingi zaidi barani na hata nje ya bara.

2. KUHUSU VIVUTIO VYA UTALII:
Mbuga ya wanyama kongwe zaidi barani ipo DRC, inaitwa Virunga. Hapo utawakuta wale Sokwe wakubwa (Gorillas), simba na tembo. Lakini mbuga hii ipo kwnye tishio la kutoweka kwa sababu kuna mafuta na kampuni ya Uingereza ya Soco tayari imetia timu kuanza kuchimba mafuta hapo mbugani.
Hawa gorilla ni kivutio kizuri sana cha utalii lakini miaka ya hivi karibuni wamekuwa adimu na kutokana na shughuli za mwanadamu, wanyama hawa wapo kwnye tishio la kutoweka kabisa. Je, DRC kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kutadhibiti hatari ya sokwe hawa kutoweka?
Kuhusu namna utalii unaweza kuleta manufaa katika biashara tafadhali fuatana na makala hii hapa chini:
3. KUHUSU MTANDAO WA BARABARA NA MIUNDOMBINU:
Ni 1.8% tu ya barabara nchini DRC ndio ina kiwango cha lami, huku chini ya 10% ya nyumba za makazi ndio zina umeme. Hii ni hali mbaya sana katika kukuza uchumi wa Taifa. Hata hivyo Benki ya Dunia imetangaza kifurushi za 1$ bilioni kwa ajili ya miundombinu ya DRC.
Moja kati ya vitu vinavyorudisha nyuma juhudi za wajasiriamali na mashirika kuwekeza nchini DRC ni maendeleo duni ya miundombinu. Ukizingatia ukubwa wa nchi hio, imekuwa ni nafuu kusafiri kwa njia ya anga kuliko barabara. Sasa @jumuiya itachangia vipi maendeleo ya miundombinu?
4. BIASHARA ZA NJE YA NCHI (EXPORTS):
Muziki wa DRC ndio mali inayouzwa zaidi nje ya nchi (export). Kuanzia miaka ya 90 muziki wa Bolingo ndio ulikua unasikilizwa na kupendwa zaidi bara zima la Afrika. Ndio maana wasanii kama Fally Ipupa na Koffi Olomide ni matajiri sana. Madini na malighafi zingine zote chali.
5. LUGHA INAYOTUMIKA ZAIDI:
Jiji la Kinshasa ni la pili kwa matumizi ya lugha ya Kifaransa likitanguliwa na jiji la Paris. Yaani Wakongo hawa wanaongea kifaransa zaidi kuliko hata miji ya nchini Ufaransa. Hata hivyo hii inachangiwa na idadi ya watu wanaoishi kwenye jiji hilo, watu milioni 10 mchezo!
Ukiacha Kifaransa raia wa Kongo pia wanazungumza lugha zingine kama Kilingala, Kiingereza, Kiswahili na lugha za makabila asilia. Hivyo ukiwa kama mfanyabiashara na moja kati ya lugha tajwa unazifahamu vyema basi nafasi ni yako kuingia DRC na kutanua biashara zako.
6. KUHUSU UGONJWA WA EBOLA:
Kwamba kupata Ebola nchini DRC ni rahisi kama kupata mafua ukiwa sehemu nyingine? HAPANA. Baada ya ugonjwa huo kufumuka mwaka 1995 na kuua watu zaidi ya 200, milipuko mingine ya ugonjwa huo imekuwa ikidhibitiwa kwa kiwango kikubwa. Hivyo Congo ni salama.
7. KUHUSU MADINI:
Lile bomu la atomiki lililodondoshwa kwenye miji ya Hiroshima na Nagasaki katika WWII lilitengenezwa kwa madini ya Uranium kutoka mgodi wa Shinkolobwe, mkoani Katanga nchini DRC. Hata hivyo mgodi huo ulifungwa mwaka 2004 kutokana na kuishiwa madini ukiiacha DRC patupu.
Kongo imenyonywa sana katika madini yake. Hali kadhalika nchi zingine katika Jumuiya zimepitia hali hio. Hivyo itakapowekwa sera ya pamoja ya kulinda na kusimamia rasilimali zilizopo ndani ya Jumuiya, bila shaka madini na rasilimali ambazo zipo DRC zitakuwa na manufaa sana.
8. HISTORIA YA UNYONYAJI:
Mfalme Leopold II wa Ubelgiji alijitangazia Kongo kuwa mali yake binafsi kuanzia mwaka 1870. Koloni hilo ndio lilikua mali binafsi kubwa zaidi kuwahi kumilikiwa na mtu mmoja kwenye historia. Umiliki huo ulisababisha vifo vya watu milioni10. Huu ndio mwanzo wa nchi kuharibika.
Mfalme Leopold II aliagiza watu kukusanya zao la mpira ambalo kwa kipindi hiko ndio lilikua zao bora zaidi la kibiashara. Wale walioshindwa kukusanya zao hilo kama kodi waliadhibiwa kwa kunyimwa chakula na kukatwa mikono yao. Ukatili huo ulikua mbaya sana dhidi ya ubinaadam.
9. HALI YA USALAMA NA VITA:
DRC imekuwa ikikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na migogoro isiyokwisha ambayo imepelekea vifo vya watu takriban milioni 6. Hali hio ya vita visivyokwisha imepewa jina la “Vita vya Dunia vya Afrika”.
Vita hivyo kwa sehemu kubwa vimekuwa vikisababishwa na vikundi fulani (kampuni, mashirika na raia wa kawaida) kugombania rasilimali katika eneo fulani. Huyu anataka kuchimba, raia wanataka kunufaika. Je, DRC kuingia kwenye @jumuiya itasaidia kumaliza janga la vita visivyokwisha?
10. KUHUSU MTO CONGO:
Ukiwa na urefu wa kilomita 4,700, mto Congo ndio mto mrefu wa pili barani Afrika ukitanguliwa na mto Nile. Pia huo ndio mto wenye kina kirefu zaidi duniani. Cha kufurahisha zaidi, Mto Congo na Mto Nile yote inapatikana katika EAC. Inakupa picha gani hii kiuchumi?
Je, EAC itaweza kuzalisha umeme wa pamoja kupitia sehemu za mto huo? Je shughuli za kiuchumi kama uvuvi, usafiri, utalii biashara ya mazao ya misitu zitaweza vipi kusimamiwa na Jumuiya kuhakikisha faida zinarudi kwa wanachi wa Kongo na wa jumuiya nzima kiujumla?
ZIADA: MSITU WA CONGO
Msitu wa pili kwa ukubwa duniani, msitu wa Congo unapatikana nchini DRC. Hata hivyo msitu huo ni mkubwa kiasi kwamba umeingia kwenye nchi zingine kama Cameroon, Jamhuri ya Afrika Ya Kati, Jamhuri ya Congo(Brazaville), Guinea ya Ikweta na Gabon. Msitu huu ni utajiri mtupu.

Katika msitu huo kuna fursa nyingi zikiwamo biashara ya magogo, madawa ya kutibu watu, mazao na wanyama, mbao, karatasi na bidhaa zote zitokanazo na misitu. Ukiwa kama mfanyabiashara ambaye sasa una uhuru wa kwenda kuwekeza DRC kirahisi, utaitumiaje fursa hii?
Sasa hayo ni baadhi ya mambo ambayo pengine ulikua huyafahamu kuhusu DRC. Mambo hayo kama yakifanyiwa kazi ipasavyo ndani ya @jumuiya basi ni wazi kutapunguza hali ya umasikini na kuimarisha amani kwa watu wa Kongo na kuimarisha uchumi wa Jumuiya nzima. Mapema mwaka 2021 jumuiya ya nchi za Afrika kwa kauli moja ilianzisha eneo huru la biashara barani (AfCFTA) ambapo nchi wanachama wanaweza kufanya biashara kwa uhuru bila ya vizuizi vya mipakani. Zaidi soma hapa chini
Jumuiya hii inatoa uhuru kwa wanachi wake kuishi na kufanya biashara popote ndani ya nchi wanachama. Jambo hili linatoa fursa kwa Wajasiriamali wa aina zote kuzurura na kutafuta masoko yao kirahisi. Ukiweza vema kutumia majukwaaa ya kimtandao kama websites, mitandao ya kijamii ujue unayo nafasi ya kuwafikia watu milioni 300 waishio ndani ya Afrika Mashariki. Sasa tuambie wewe mtu wa Teknolojia, website designer, mtaalam wa kutengeneza android app, mkulima, engineer nk, unataka ufaidike vipi hapa? Tuambie..
Je umependezwa na makala yetu hii ya leo?
Unataka kufanya malipo kwa huduma zetu bila kuhofia makato ya miamala?
Sasa tumekuletea huduma ya LIPA NAMBA ya M-PESA (TILL NUMBER) – 5432715 ambapo unaweza kututumia TIP ya kutupongeza kwa kazi nzuri au Kulipia huduma unazozipata kutoka kwetu BILA MAKATO ya miamala.
Tumia LIPA NAMBA yetu muda wowote yaani 24/7.
