LIPA KODI KWA FAIDA YA BIASHARA YAKO
Wamiliki wengi wa biashara huanza katika Biashara binafsi (machinga/sole proprietor). Baadae hukua kufikia partnerships, wabia wa kampuni mpaka mashirika. Kadiri unavyotengeneza mifumo ya biashara yako ndivyo inakuwa rahisi kulipa kodi.
Kodi huja katika namna nyingi, unapofanya kazi, unalipwa ujira/mshahara, hapo utalipa “Income Tax”. Kutegemea na kiasi cha pesa unacholipwa, asilimia fulani hukatwa na muajiri wako na kulipwa kwenye Mamlaka za Kodi, % hio huitwa “Withholding Tax”, hii hutaiona kwenye paycheck yako kwani hulipwa na mwajiri moja kwa moja kwenda kwa Mamlaka za kodi.
Ukinunua bidhaa, fahamu kuna kodi pale unalipa ambayo inajumuishwa katika bei ya bidhaa hio. Kodi hio huitwa “VAT” ambayo ni kodi maarufu na yenye kuingiza mapato makubwa sana katika mamlaka za Kodi. Kama unamiliki mali/ardhi unalipa Kodi iitwayo “Property Tax” kulingana na thamani ya mali/ardhi yako hio.
Kulipa kodi ni wajibu wa kizalendo, lakini zaidi ni matakwa ya kisheria. Usipolipa kodi unajiweka kwenye mazingira ya kulipishwa faini au adhabu kwa mujibu wa sheria. Kodi unayolipa inakwenda sehemu mbalimbali za kiserikali kama mishahara ya watumishi wa serikali, polisi, jeshi la zimamoto na uokoaji, kuimarisha miundombinu, sekta ys afya n.k.
UNAEPUKA VIPI RUNDO LA KODI KWA MANUFAA?
Kuendesha biashara kunajumuisha gharama nyingi sana. Na katika kila gharama kuna kiasi cha kodi unatozwa. Fahamu, Ukinunua unalipa kodi, Ukiuza unamlipisha mtu kodi. Jambo hili linafanyika ukiwa unajua na hata bila ya wewe kujua.
1. MANUNUZI
Kodi ya VAT (Value of Added Tax/Kodi ya Ongezeko la Thamani) ambapo unaponunua bidhaa/huduma yoyote unakuwa unanunua kitu chako pamoja na kukilipia kodi yake ya VAT hapo hapo. Kodi hiyo huwa ni 18% ya thamani kamili ya bidhaa/huduma inayouzwa. Mfano unaponunua umeme wa 2,000/-, hapo unakuwa umelipia na kodi yake ambayo imejumlishiwa kwenye hio 2,000/- (indirect tax). Hali kadhalika katika bidhaa/huduma zingine kama mafuta, vocha, computer, chakula, gesi n.k. Kila unachonunua kina kodi yake, Hivyo kama mfanyabiashara hakikisha manunuzi yako yote yahusuyo gharama za uendeshaji (umeme, maji, chakula, mafuta, maintenance, usafi) yanakuwa na risiti zake halali. Risiti zako hueleza kodi zile ulizokatwa “withheld” katika manunuzi/matumizi ya biashara yako. Hivyo jambo hili litakupa unafuu katika kulipa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
2. MAUZO
Wafanyabiashara huwalipisha wateja wao VAT lakini wengi hawapendi kulipa kiasi hiko cha kodi katika Mamlaka ya Kodi. Jambo hili ni kinyume na sheria na linaweza kukuweka kwenye mikono ya kisheria yanayoweza kukufilisi mali, kukupeleka gerezani au vyote vikakupata.
Hivyo unapofanya mauzo katika biashara yako hakikisha unatoa risiti halali ili bidhaa unazouza ziwe kwenye uwiano mzuri wa thamani na Mamlaka za kodi
CHANGAMOTO:
i. Tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya 70% biashara hazilipi kodi. Hii inachochewa na upungufu wa elimu ya kodi pamoja na morali ya wananchi katika kulipa kodi.
ii. Pia kumekuwepo na sekta ambazo hazilipi kodi ipasavyo, mfano sekta ya madini, uvuvi, misitu na utalii. Hii imetokana na kutokuwepo na njia bora za ukusanyaji wa kodi katika maeneo hayo, hivyo kudidimisha mapato yao katika kodi.
iii. Kuwepo kwa misamaha mikubwa ya kodi (tax exemptions) kwa wawekezaji wa ndani na wale wa nje. Mbinu hii iliwekwa ili kuwavutia wawekezaji wazidi kumininika lakini matokeo yake yamekuja kudhoofisha sekta zingine za biashara kutokana na kutokuwepo kwa usawa katika makusanyo.
iv. UFISADI: Inarudisha maendeleo nyuma sana hali ya kutokuwepo kwa makusanyo ya kodi. Hali hii kwa kiasi kikubwa huchochewa na kukithiri kwa vitendo vya Ufisadi katika Mashirika ya Umma pamoja na Mamlaka za Kodi. Watu huishiwa morari ya kulipa kodi pale wakiona kodi zao zinaishia mifukoni mwa watu wachache tena kwa manufaa binafsi. Jambo hili ni baya sana katika maendeleo ya biashara. Likemewe kwa nguvu zote.
MATUMIZI YA ICT KATIKA MFUMO WA KODI:
Teknolojia ya ICT imekuja kuwa mkombozi katika mifumo ya mapato na kodi katika biashara na Mamlaka za Kodi katika kutunza kumbukumbu za walipa kodi. Teknolojia imeleta afadhali katika kukusanya kodi kupitia matumizi ya mashine za EFD ambayo hutumika kukusanya taarifa za kodi, mauzo na manunuzi katika biashara.
Mashine hizi za EFD zilianza rasmi kutumika mwaka 2013 zikiwa na lengo la kusajili wafanyabiashara wote pamoja na miamala yote ya mauzo na manunuzi nchini Tanzania. Mwaka 2014/15 Halmashauri ya manispaa ya jiji la Arusha ilianza kutumia mfumo wa LGRCIS (Local Government Revenue Collection Information System). Zaidi kuhusu mfumo wa mapato ya serikali za mitaa unaweza kupata kupitia makala kwenye link hii https://rednet.co.tz/ufahamu-mfumo-wa-kodi-na-mapato-ya-serikali-za-mitaa/ yenye kichwa “UFAHAMU MFUMO WA KODI NA MAPATO YA SERIKALI ZA MITAA”
Kuanzia hapo Halmashauri 8 nchini Tanzania zilianza kutumia mfumo huo wa LGRCIS kama mfumo mkuu wa makusanyo ya kodi katika Halmashauri zao. Hata hivyo mwaka 2016 mifumo yote ya makusanyo iliunganishwa katika mfumo mkuu wa makusanyo ya kodi wa TRA.
Lakini bado mpaka sasa mfumo wa LGRCIS unaendelea kutumika ktika kukusanya mapato ya halmashauri ikijumuisha Ushuru, Tozo na kodi za leseni za biashara. Mfumo huo umerahisisha malipo ya kodi kupitia njia za malipo ya kielektroniki kama MPESA, Bank transfer, Tigopesa n.k.
Hivyo, katika mifumo ya kodi kupitia makala haya ni matumaini yangu umejifunza kitu muhimu katika namna unavyoendesha biashara yako kwa faida bila kukwaruzana na Mamlaka za Kodi. Una maoni yoyote? Tafadhali weka comment yako hapa chini. Pia unaweza kushare link ya makala hii ili kuhakikisha inawafikia watu wengi zaidi kwa faida ya biashara zetu.
Sasa tumekuandalia makala hizi hapa chini zenye lengo la kukuimarisha katika namna ya kulipa kodi na kuifahamu mifumo yake zaidi. Zitakusaidia sana ukizisoma zote. Gusa link kisha makinika:
- https://rednet.co.tz/ufahamu-mfumo-wa-kodi-nchini-tanzania/ yenye kichwa “UFAHAMU MFUMO WA KODI NCHINI TANZANIA”
- https://rednet.co.tz/unafahamu-nini-kuhusu-urasinishaji-harmonization-katika-biashara/ yenye kichwa “UNAFAHAMU NINI KUHUSU URASINISHAJI (HARMONIZATION) KATIKA BIASHARA”
- https://rednet.co.tz/ukiritimba-katika-biashara-ni-asali-au-shubiri/ yenye kichwa “UKIRITIMBA KATIKA BIASHARA, NI ASALI AU SHUBIRI”