Biashara nyingi zimekuwa zikiendeshwa katika mtindo wa “Kujiajiri” ambapo wajasiriamali wengi huteseka wakifanya kazi kwa bidii usiku na mchana lakini hujikuta siku moja tu wasipofanya kazi basi biashara inashindwa kuzalisha. Yaani mfanyabiashara unajikuta unakuwa mtumwa kwenye biashara yako mwenyewe? Hio dhana ya kujiajiri inakuwa na maana gani sasa? Leo sasa tuangalie Biashara yako inaweza vipi kuwa taasisi imara inayojitegemea? Makinika mpaka mwisho wa makala hii.
Septemba 21 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Amani. Sasa katika Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (UN), Lengo Na. 16 limekazia katika kudumisha Amani, Haki na Taasisi Imara. Amani ni mbolea muhimu katika ukuaji wa uchumi mahali popote. Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa uliokaa mwaka 2001 ulithibitisha kuweka Siku maalum ya kutafakari na kudumisha Amani, Haki na Taasisi Imara duniani, ambapo siku hio ni September 21 kila mwaka.
Hii ni kutokana na vitendo vya uvunjifu wa amani, taasisi dhaifu na kukosekana haki si za kidemokrasia katika utendaji, serikali hizi ambazo mara nyingi huwa ni za kidikteta au za kifalme, mara nyingi huendeshwa kwa sheria zinazokandamiza upande mmoja na kuimarisha kikundi kidogo cha watu kwa maslahi yao binafsi.
Jambo hili hutokea pale viongozi (watu wanaopewa dhamana) kushindwa kuwajibika kwa wanachi na hivyo kujiundia sheria ambazo zinawapa mamlaka ya kutumia rasimali za nchi huku zikiwaacha wanachi katika hali ya upofu wasiwe na nguvu ya kuuliza na kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali zao. Hili ni jambo baya na linalopaswa kuagamizwa mahali popote kwanzia ngazi ya familia, biashara, kampuni, shirika mpaka serikalini.
Mwandishi mahiri Robert Kiyosaki katika kitabu chake cha CASH FLOW QUADRANT amefafanua kwanini Matajiri huendelea kuwa matajiri huku Watu wa Uchumi wa kati wakiendelea kukimbia mbio za panya na masikini wakizidi kuwa masikini. Kwa haraka haraka, katika Njia 4 za kuingiza mapato ambazo zimeonyeshwa kwa herufi za E, S, B na I, zimetajwa kuwa ndio chanzo kikuu cha mapato ya watu duniani.
SEHEMU ZA KUIFANYA BIASHARA YAKO KUWA TAASISI IMARA?
Waswahili wanakwambia “Kila mbuzi atakula kwa urefu wa kamba yake” lakini katika uwanda wa kiuchumi na biashara duniani, kila mtu anao uwezo wa kubadilika na kufanya uchaguzi ulio bora zaidi kwa maisha yake ya kiuchumi na kijamii. Na hii ni kwa kujifunza na kufanya kazi tu.
E = EMPLOYEE (MWAJIRIWA): Kitu cha kwanza ambacho kipo kichwani kwa mwajiriwa yeyote ni uhakika wa kibarua chake (job security). Mwajiriwa hufanya kazi kwa bidii ili apate mkate wa kila siku na zaidi awe na hakika kuwa ataendelea kupokea mshahara kila mwisho wa mwezi kwa miaka mpaka atakapostaafu au kumaliza mkataba wake. Dhana ya kuwa majiriwa huathiri ubunifu wa mtu katika kutaka kujaribu shughuli nyingine itakayoimarisha uchumi wake zaidi ya ajira.
Mwajiriwa anapohitaji kukua kiuchumi hutafuta ajira itayomlipa zaidi na si fursa za biashara mpya.

S= SELF-EMPLOYED (KUJIAJIRI): Hii ni njia ya mateso makubwa, japokuwa vijana wengi eti ndio hupenda kufanya shughuli za kujiajiri wakihisi kuwa huko kuna uhuru mkubwa na pesa nyingi. #VijanaWenzangu acheni kujidanganya. Unapojiajiri fahamu kuwa utajinyima uhuru wako binafsi ili biashara yako iweze kuwa hai. Wewe ndio unakua CEO, sales manager, mhasibu wewe, mtu wa masoko wewe, yaani wewe ndio unakuwa kila kitu. Hata hivyo kwa biashara inayoanza si vibaya kupitia katika hatua hii japo hutakiwi kukaa muda mrefu hapa, lazima biashara ivuke hiki kiunzi.
B=BUSINESS OWNER (MMILIKI WA BIASHARA): Tofauti na walio katika Chumba “S” Mtu anayemiliki biashara sio lazima awe anafanya kazi katika biashara hio. Yeye anamiliki mfumo wa utendaji au bidhaa ambayo ndio huzalisha pesa muda wote hata asipokuwepo. Mfano, mtu anayemiliki kiwanda cha kutengeneza nguo. Sio lazima awe ndio mtendaji mkuu wa kutengeneza nguo, hata hivyo yeye anaweza kuajiri watu wa kiwandani na kuwalipa ili waendelee kuzalisha bidhaa zitazoendelea kuingiza pesa.
I=INVESTOR (MUWEKEZAJI): Huyu ndiye mtu mwenye uelewa mkubwa zaidi kati ya wote ambao tumewajadili hapo juu. Mtu huyu hutafuta Mali (Assets) zaidi kuliko madeni (Liabilities). Mara nyingine hutumia pesa za watu wengine (mkopo) ili kuhakikisha anapata Mali itakayozalisha (asset). Ukitaka kufahamu kwa undani kuhusu Uwiano unaofaa wa Mali na Madeni katika biashara gusa link hii Uwiano wa Mali (assets) na Madeni (Liabilities) kwenye biashara.
Mtu huyu hutumia faida anayopata kutoka kwenye assets zake kununua assets nyingine nyingi zaidi, na hujikuta akifurahia maisha ya kuingiza kipato kutoka kwenye assets kuliko vyanzo vya matumizi (liabilities). Kama ulikua hufahamu basi Matajiri unaowajua duniani wote ni Wawekezaji huku wakitumia kanuni ya 70% kwa 30% katika shughuli zote za kifedha. Kiufupi kanuni hio hutumika katika kupanga matumizi ya mapato ambayo hugawanywa katika mafungu matatu ya:
i. 70% Matumizi ya kawaida (Normal Expenses including taxes, rents, food, accomodations etc)
ii. 30% (20% Servings + 10% Charity) Mwekezaji anapohitaji pesa hutafuta assets zaidi kuliko kufanya matumizi yanayofyonza pesa za biashara.
Sasa basi, hayo yote niliyoyaeleza, hayatakuwa na maana kama hayatafanyika katika muundo wa Taasisi Imara.
BIASHARA KAMA TAASISI IMARA INA SIFA ZIPI?
Taasisi Imara ni ile jumuiya ya kiuchumi/Kijamii ambayo inaendeshwa kwa mujibu wa katiba katika utendaji wake wa kila siku. Jumuiya hio inaweza kuwa ni Serikali, Shirika, Kampuni, Chama, Biashara au Familia. Familia (Ndoa) ndio Taasisi ya kwanza kabisa kuwahi kuanzishwa na binadamu duniani. Ndio maana wahenga wanakwambia “Maendeleo yanaanzia nyumbani.”
Maendeleo ya taasisi hutegemea uwepo wa sheria zitakazokuwa muongozo wa kila kinachofanyika kila siku ndani ya taasisi hio. Hata hivyo ili iwe taasisi imara inapaswa kuwa na sifa hizi:
1. SHERIA MBELE, MTU NYUMA: Taasisi imara hutambua na kutekeleza matakwa ya kisheria na kamwe si matakwa ya mtu binafsi. Sheria hizi huandikwa katika mfumo wa Katiba (constitution/memorandum/articles of assosciation, Taratibu (regulations) na sheria ndogondogo (by-laws). Taasisi zinazoongozwa vema kwa mujibu wa sheria bila kumuogopa mtu huwa imara sana kiutendaji na hufikia malengo yake kiurahisi zaidi.
2. UTAMADUNI: Katika utendaji bora, Utamaduni huzingatiwa kama silaha bora zaidi katika uzalishaji/utoaji huduma wenye viwango vya juu vinavyitakiwa. Wahenga walishasema “Culture eats strategy for breakfast” yani, hakuna mbinu ambayo itaweza kufanya kazi kwa mafanikio isipofanywa kama sehemu ya utamaduni. Hivyo Taasisi imara hufanya shughuli zake katika Utamaduni uliotengenezwa kwa muda mrefu katika kufikia malengo yaliyowekwa. Mfano, utamaduni wa kupongeza mtendaji bora, utamaduni wa kumhudumia mteja kwa njia ya mtandao na utamaduni wa kuzingatia viwango.
3. UWAJIBIKAJI: Ili iwe Taasisi imara lazima watendaji wawajibike katika majukumu ya kila siku. Watendaji wanapaswa kuwajibika kwa Kupongezwa, Kujiuzulu au Kuongeza kiwango cha uzalishaji/utoaji huduma kwa wateja wao. Taasisi imara haipaswi kufumbia macho swala la uwajibikaji.

4. KWELI NA HAKIKA: Hakuna Taaasisi Imara ambayo haijiendeshi katika namna ya Ukweli na Uhakika kwa wateja wake. Hata hivyo, hakuna mifumo ya Taasisi inayofanya kazi kwa ubora wa 100%, ni vema kuhakikisha jambo hili linazingatiwa.
Tulizoziona leo ni baadhi ya sifa zinazotengeneza Taasisi Imara. Kwa mujibu wa malengo Endelevu ya kimataifa ya UN, imepangwa kutimiza lengo la kuwa na Taasisi Imara ifikapo mwaka 2030 (#Agenda2030). Tujadili kupitia Replies, Retweets na Share ili watu wengi zaidi wanufaike.
Tuungane kwa pamoja kuhakikisha Biashara yako inaweza vipi kuwa taasisi imara. Endelea kupata makala muhimu kuhusu Biashara, Uchumi na Teknolojia kupitia links hizi hapa: